Na Okuly Julius , DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Dr. Paul Lawala ,amesema waandishi wa habari, wajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa inajenga jamii ambayo inatambua na kuthamini afya ya akili.
Dr. Lawala ameyasema hayo leo Agosti 30 ,2024 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu afya ya akili.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuboresha uelewa na ujuzi wa waandishi wa habari kuhusu masuala ya afya ya akili kupitia mawasilisho yatakayofuatiwa na mijadala , ili kuoanisha afya ya akili na utoaji taarifa sahihi kwa jamii kupitia vyombo vya Habari.
“Waandishi wa habari mna nafasi ya kipekee na ya muhimu katika jamii. Kupitia kazi zenu, mnatoa habari, elimu, na burudani, na kwa kufanya hivyo, mnaathiri kwa hasi au chanya jinsi watu wanavyofikiria, wanavyotenda, na wanavyojihusisha na masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na afya ya akili,”amesema Dr. Lawala
Ameongeza kuwa :”Kwa hivyo, tunapokutana hapa leo, ni muhimu kutambua kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu sana katika kuelimisha umma kuhusu afya ya akili na kupunguza unyanyapaa unaohusishwa na afya ,changamoto na magonjwa ya akili,”
Akizungumzia kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo alisema afya ya akili ni sehemu muhimu ya afya ya jumla ya mtu binafsi na jamii kwa kuwa Afya ya Akili ni Afya,Afya ya akili inamhusu kila mtu na hakuna afya bila afya ya akili.
Amefafanua kuwa hali hiyo imechangia kuwepo kwa unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya wale wanaopambana na changamaoto za Afya ya Akili na magonjwa ya akili.
Katika hatua nyingine amesema waandishi wa habari wanaweza kusaidia kubadilisha hali hii kwa kutoa taarifa sahihi, zinazoelimisha, na zenye uwiano uliotafitiwa kuhusu afya ya akili.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwapa ninyi, waandishi wa habari, maarifa na ujuzi unaohitajika ili kuripoti kwa usahihi na kwa uwajibikaji kuhusu afya ya akili,”amesema
Ameongeza kuwa :”Tunataka kuhakikisha kwamba mnakuwa na uwezo wa kutambua habari sahihi, kuzuia kusambaza habari zilizopotoshwa, na zaidi ya yote, kuweza kutoa taarifa kwa njia ambayo inaondoa unyanyapaa na kuongeza uelewa katika jamii,”
Baadhi ya Waandishi wa habari Mkoani Dodoma, Walioshiriki semina ya Afya ya Akili iliyotolewa na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe leo Agosti 30,2024 jijini Dodoma.Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe Dr. Paul Lawala, akizungumza leo Agosti 30, 2024 jijini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya Afya ya Akili iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Hospitali hiyo.
0 Comments