WATOA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA WATAKIWA KUWAPA MIKATABA WANANCHI WANAOWAKOPESHA.

Wananchi  wa Mji Mdogo Mikumi Mkoani Morogoro wakimsikiliza kwamakini   Afisa wa UTT Bi Grace Muyaiza

Na. Ramadhani Kissimba, WF, Morogoro

Watoa huduma ndogo za fedha  na vikundi vya kijamii nchini  vinavyojihusisha na huduma za mikopo vimetakiwa kuwapatia nakala ya mkataba wananchi wanaowakopesha mikopo.
 
Akizungumza katika program ya elimu ya fedha kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Mikumi, Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Grace Muiyanza, alisema kuwa watoa huduma wanatakiwa kutoa mikataba kwa wanaowakopesha kwa mujibu wa sheria iliyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
 
Aidha Bi Muiyanza alisema mkataba ni mafungamano kati ya pande mbili ya mkopeshaji na mkopaji hivyo ni lazima kila upande uridhie makubaliano hayo kabla ya kuchukua mkopo na kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza changamoto zinazojitokeza wakati wa kurejesha mkopo na pia mkataba utakuwa ndio njia pekee ya kila mmoja kupata haki yake itakapotokea mgongano baina yao.
 
Pia, Bi. Muiyaza aliwasihi wananchi kabla ya kusaini mkataba wa mkopo ni vizuri kila mmoja akapata nafasi ya kuusoma na kuelewa masharti ya mkataba huo ili usije ukamfunga kwa vipengele ambavyo vitasababisha ugumu wa kurejesha mkopo wake.
 
‘’Mkataba ni masharti ya pande mbili, hakikisha umeusoma na kuuelewa mkataba, na hata kama ujui kusoma nenda kwa maafisa wa maendeleo ya jamii wakueleweshe masharti yaliyomo kwenye mkataba huo maana ukiamua kusaini bila ya kuuelewa utakuwa umeshakubaliana na masharti na utakuwa umesaini masharti yatakayokuja kukufunga baadae’’. Alisema Bi Muiyaza
 
Awali akifungua mafunzo hayo Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Mikumi Bi. Edith Mlay, aliwataka wananchi wa Mikumi kuitumia fursa hiyo ya kujifunza masuala ya fedha ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo kutoka kwa baadhi ya watoa huduma za fedha. 
 
Bi. Mlay aliongeza kuwa elimu ya fedha ni muhimu sana kwa wananchi wa Mikumi kwa sababu mji huo umekusanya makundi muhimu ya kijamii yakiwemo ya wakulima na wafugaji, hivyo elimu hiyo itawasaidia wananchi hao kutumia fursa ya uwekezaji zilizopo katika sekta ya fedha baada ya kuuza mazao yao.
 
Wizara ya Fedha na washirika wa sekta ya fedha nchini imehitimisha program maalum ya elimu ya fedha kwa umma kwa Mkoa wa Morogoro ambapo elimu hiyo ilitolewa katika Halmashauri saba (7) ambazo ni Halmashauri ya Morogoro Mjini, Morogoro vijijini, Kilosa, Mvomero, Ifakara, Mlimba na Gairo.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha – Morogoro)
Afisa Masoko  Mwandamizi kutoka Kampuni ya UTT Bw. Rahim Mwanga  akiongea na washiriki  wa program  ya elimu ya fedha kwa umma (Hawapo pichani) iliyotolewa  katika Mji Mdogo Mikumi Mkoani Morogoro. 
Afisa Usimamizi kutoka Wizara ya  Fedha Bi Grace Muiyaza akizungumza katika akiongea na wananchi  katika Programu  ya fedha yaliyotolewa  kwa wanannchi na  Mamlaka ya Mji  Mdogo  wa Mikumi Mkoani Morogoro. 

Post a Comment

0 Comments