Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini Tanzania, William Mwamalanga, ametoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika kulinda na kudumisha amani ya nchi, aeisisitiza kuwa amani ni hitaji la msingi kwa kila mwananchi bila kujali tofauti zao za kisiasa, kijamii au kidini.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa amani nchini, Askofu Mwamalanga amesema viongozi wa dini na wadau mbalimbali wanaendelea na kampeni za kuhamasisha vijana kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha utulivu na mshikamano.
Kauli hiyo inaendana na misimamo yake ya muda mrefu ya kutetea amani na maadili katika jamii.
“Ushauri wetu kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Katambi, ni kwamba kila Mtanzania awajibike kutunza amani. Sisi tupo kwenye kampeni ya kuhamasisha vijana kusitawisha amani katika kila eneo. Amani ni hitaji la kila mwananchi,” alisema Askofu Mwamalanga.
Ameeleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya amani na utulivu, huku akiwataka vijana kutumia nguvu zao katika shughuli za maendeleo badala ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.
Aidha, Askofu huyo amesema viongozi wa dini wataendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria, maadili na haki za wengine ili kuimarisha umoja wa Watanzania.
Amesisitiza kuwa jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anachangia kwa maneno na matendo yanayojenga mshikamano na kuzuia migawanyiko katika jamii.
Kauli ya Askofu Mwamalanga imekuja wakati ambapo viongozi mbalimbali wa dini na jamii wamekuwa wakitoa wito wa kuendeleza amani, wakieleza kuwa ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini.

0 Comments