Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imezindua maadhimisho ya miaka 30 ya utoaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika tiba ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996. Uzinduzi huo umeambatana na Ibada Maalumu ya Shukurani ya miaka 30 ya taasisi hiyo, ambapo uongozi umeahidi kuendelea kuboresha huduma na kuzisogeza karibu zaidi na wananchi nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amewapongeza watumishi wa MOI kwa mchango wao mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi na kuifanya taasisi hiyo kuwa kinara wa huduma za kibingwa ndani na nje ya Tanzania. Amesema mafanikio hayo yanatokana na kujituma kwa watumishi pamoja na uwekezaji uliofanywa katika sekta ya afya.
Dkt. Shekalaghe amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano miongoni mwa watumishi wa kada zote, kuanzia ngazi za juu hadi za chini, ili kuhakikisha huduma bora, salama na endelevu zinaendelea kutolewa kwa wagonjwa na wananchi kwa ujumla. Aidha, ameitaka MOI kuimarisha ushirikiano wake na Jeshi la Polisi pamoja na wadau wengine katika kuelimisha jamii kuhusu kinga dhidi ya ajali."Nipo tayari kuendelea kutoa ushirikiano wangu kwa MOI katika juhudi mbalimbali za kuboresha afya za wananchi na kuhamasisha elimu ya kinga dhidi ya ajali," amesema Dkt. Shekalaghe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema katika kipindi cha miaka 30 taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za afya, utafiti na mafunzo. Ameeleza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha MOI kuwa moja ya taasisi muhimu za tiba ya kibingwa nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amebainisha kuwa MOI imeendelea kubuni na kutekeleza huduma mbalimbali za kibunifu, ikiwemo huduma za mkoba na programu ya Back Stopping, inayolenga kuanzisha na kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali za mikoa mbalimbali nchini. Mikoa inayonufaika na mpango huo ni pamoja na Arusha, Mara, Kagera, Njombe na Ruvuma, hatua inayolenga kupunguza safari za wagonjwa wanaohitaji huduma hizo na kuongeza upatikanaji wa matibabu karibu na maeneo yao.



0 Comments