
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Serukali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeanza mchakato wa kuhakikisha hakuna mgonjwa anayesafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Mchakato huo utakamilika mara baada ya kujengwa hospitali nyingine mbili zinazotoa huduma bora za matibabu ya kibingwa kwa maradhi ya moyo, saratani, ubongo na uti wa mgongo.
Akizungumza 13 Oktoba 2025 wakati wa kutia saini mkataba wa ujenzi, ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja kati ya SMZ na Kampuni ya Jiangxi International, Rais Dkt. Mwinyi alisema kukamilika kwa hospitali hizo kutafanya huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana Zanzibar kwa ubora na viwango vya kimatataifa.
Alisema kutajengwa Hospitali ya Matibabu ya Magonjwa ya Saratani na Mifupa na nyingine ya Rufaa na Kufundishia Watendaji wa Sekta ya Afya ambayo itakayojengwa eneo la Binguni.
“Kukamilika kwa hospitali hizo kutaiwezesha Zanzibar kuondokana na utaratibu wa kusafirisha wagonjwa nje ya nchi” alisema Dkt. Mwinyi ambaye pia anawania awamu nyingine ya nafasi ya Rais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
Alisema mkataba huo uliosainiwa ni ishara ya dhamira ya serikali kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini na Hospitali ya Mnazi Mmoja inaenda kubadilika na kuwa mpya kabisa yenye hadhi ya kisasa.
“Sekta ya afya ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa, kwani wananchi wenye afya bora ndio msingi wa ujenzi wa uchumi imara na uimarishaji wa utoaji wa huduma bora za kisasa” alisema.
Rais alibainisha kuwa baada ya serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali kuanzia ngazi ya msingi, wilaya na mkoa hatua inayofuata sasa ni kujenga hospitali tano za rufaa moja kila mkoa, zinazotoa huduma zote za kisasa zenye viwango vya kimataifa na kuendeshwa kitaalamu.
Zanzibar pia inatekeleza mpango wa matibabu bila malipo kwa wananchi wake wote na wanatekeleza marufuku ya kuwapelekea wagonjwa vyakula hospitalini kutoka majumbani kwa waliolazwa kwani vinatolewa bure kwa ushauri wa daktari kulingana na changamoto ya mgonjwa husika.
Ujenzi wa miundombinu hiyo pia umelenga utalii wa matibabu ambao utawezesha wagonjwa kutoka nchi zingine kuja nchini kwa ajili utatibu, madaktari wan je na ndani kufanya mafunzo na utafiti hali ambayo itaongeza tija na mapato ya serikali.

0 Comments