Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amehitimisha Kampeni za Chama Cha Mapinduzi Zanzibar na kutangaza sekta 11 za kipaumbele katika awamu ijayo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 26 Oktoba 2025, alipohitimisha Kampeni za Chama Cha Mapinduzi katika Uwanja wa Mnazi Mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wa wananchi kwa dhamira ya kuleta maendeleo zaidi.
Ameeleza kuwa licha ya kazi kubwa iliyofanywa katika ujenzi wa miundombinu, awamu ijayo itaendeleza ujenzi wa bandari, barabara na viwanja vya ndege ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Pemba ambao ujenzi wake tayari umeanza, kuimarisha zaidi Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, pamoja na Bandari za Mangapwani na Fumba ili ziweze kupokea meli nyingi zaidi.
Eneo jingine alilotaja ni ujenzi wa miundombinu ya barabara kuu ikiwemo barabara ya Tunguu hadi Makunduchi, na ujenzi wa madaraja ikiwemo Daraja la Chwaka na Charawe, ili kuunganisha mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja.
Kuhusiana na sekta ya elimu, amesema Serikali ijayo itaendelea kujenga skuli zaidi za ghorofa za msingi na sekondari katika wilaya na mikoa yote nchini.
Akizungumzia sekta ya afya, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ina dhamira ya kujenga hospitali kubwa ya kutibu saratani katika eneo la Binguni, ujenzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja pamoja na Hospitali ya Rufaa na ya Kufundishia Binguni.
Kwa miradi ya maji, ameeleza kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 55 kwa ajili ya mradi wa kusambaza maji katika Mkoa wa Kusini Unguja na mradi mkubwa wa maji wa Mkoa wa Mjini Magharibi, ambao utahusisha ujenzi wa matangi makubwa yenye ujazo wa lita milioni moja ya kuhifadhia maji.
Akizungumzia sekta ya ajira, Dkt. Mwinyi ameahidi kuzalisha ajira zaidi ya 350,000 katika awamu ijayo, ikiwemo ajira za Serikali, sekta binafsi, na programu za kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe.
Kuhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi, amesema Serikali itaendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa wakulima wa mwani na wajasiriamali ili kuwainua kiuchumi.
Akizungumzia suala la chakula, ameahidi kuwa Serikali itajenga maghala maalum ya kuhifadhia chakula kwa ajili ya kukabiliana na mfumuko wa bei na kuhakikisha upatikanaji wa chakula wakati wote.
Kuhusu sekta ya kilimo, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kuwapatia wakulima mafunzo, pembejeo za kilimo, mbegu bora, na ujenzi wa skimu za umwagiliaji pamoja na mikopo isiyo na riba.Rais Dkt. Mwinyi amehitimisha hotuba yake kwa kuwaomba wananchi kumchagua tena kwa kura nyingi ili aendelee kuiongoza Zanzibar kwa awamu nyingine, na kuwashukuru wananchi pamoja na wanachama wa CCM kwa kuendesha kampeni za kiistarabu.




0 Comments