Na Mwandishi wetu, Ndutu Ngorongoro.
Kwa wale waliozaliwa zamani kidogo wanajua historia ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa akina mama wajawazito kwenda kujifungua, kama ingekuwa ni hosptali eneo la Ndutu ndani ya hifadhi ya Ngorongoro lingefananishwa na hospitali hiyo kwani katika eneo hilo maelfu ya wanyama hao humiminika kwenda kuzaa.
Kama wasemavyo wahenga mwenda kwao si mtumwa, baada ya kushika mimba kutoka katika harakati zao za mizunguko kwenye hifadhi mbalimbali ,ikifika wakati wa kuzaa nyumbu huamua kurudi nyumbani eneo la Ndutu kwa ajili ya kujifungua na kupata malisho yenye virutubisho vinavyosaidia makuzi ya haraka kwa watoto wao.
Kitu cha kikubwa cha kuvutia kwa nyumbu ni kwamba hushika mimba kwa wakati mmoja na hurudi pamoja katika eneo salama kwa ajili ya kuzaa, na eneo kubwa ambalo nyumbu wanalitumia ni tambarare za Ndutu zilizopo katika kivutio namba moja cha utalii barani Afrika (Eneo la hifadhi ya Ngorongoro)
Dkt. Dickson Wambura ni mtaalam wa wanyama kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, anaeleza kwamba nyumbu wana mpangilio wa kushika mimba na kuzaa kwa pamoja hasa kwa wale wanaotoka ikolojia ya mfumo wa Serengeti ambapo majike hushika mimba kati ya April na Mei kila mwaka na ikifika mwezi Januari hadi machi ni wakati wa kuzaa.
Ndutu ni eneo salama la kujifungulia kutokana na chakula kinachopatikana kwenye eneo hilo kuwa na virutubisho ambavyo mtoto wa nyumbu humfanya awe na nguvu na anapozaliwa tu hunyanyuka na kuanza kukimbia, eneo hilo pia lina nyasi za wastani ambazo kwao ni rahisi kuwaona wanyama wakali kama vile Simba, chui, Fisi, duma na mbweha.
Kwa mujibu wa Dkt. Wambura maisha ya nyumbu yametawaliwa na umoja, ujasiri na akili, ingawa baadhi ya watu huamini kuwa nyumbu hawana akili kumbe kukimbizana kwao kwa pamoja ni ishara muhimu ya kuwa penye wengi hapaharibiki jambo.
Hiyo ndiyo historia ya nyumbu katika maisha yake ya uzazi ambapo watazunguka kila kona ya ikolojia ya Serengeti, Pololeti na Masai Mara lakini ikifika wakati wa kuzaa watarudi Ndutu na hii inadhihirisha usemi usemao titi la mama ni tamu.




0 Comments