WAZIRI CHANA AZITAKA TAASISI ZA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUSHIRIKIANA KATIKA UTENDAJI KAZI

Waziri wa Maliasili na Utalii  Mhe. Balozi,Dkt Pindi Chana amezitaka taasisi zilizoko chini  ya Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi hizo.

Balozi Chana ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 oktoba, 2024 wakati akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika kikao kilichofanyika jengo la kitega uchumi la Ngorongoro jijini Arusha.

Amesisitiza kuwa kama kuna huduma ambazo zinatolewa na taasisi mojawapo zilizopo ndani ya Wizara hiyo ni muhimu kushirikiana ili kurahisisha utendaji kazi na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji katika sekta ya uhifadhi na utalii.

“Fuateni sheria na taratibu zilizopo ili kuongeza ushirikiano wa taasisi zote, nawasisitiza pia kujenga utamaduni wa kutembeleana kwa lengo la kujifunza, na  kama kuna uwezekano wa kusaidiana vifaa vya kufanyia kazi katika maeneo mbalimbali saidianeni ili kuondoa changamoto katika taasisi fanyeni hivyo .” amesema waziri Chana.

Aidha, Balozi Dkt Pindi Chana imeipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongo kwa kuweza kukusanya jumla ya shilingi bilioni 96.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024/25  ukilinganisha na robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya shilingi bilioni 68.
Mapema Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema Doriye alimweleza Waziri Chana kwamba mamlaka inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa umakini ili kuhakikisha kuwa inafikia malengo iliyojiwekea ya kuboresha shughuli za uhifadhi na kuongeza idadi ya watalii ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.

Mhe. Chana yupo jijini Arusha kutembeleza taasisi mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo ameongozana na Naibu Katibu Mkuu (Utalii)  Bw.Nkoba Mabula pamoja na Mkurugenzi wa Utalii Dkt.Thereza Mugobi

Post a Comment

0 Comments