JITEGEMEE SEKONDARI(JKT MGULANI) KUBORESHA MIUNDOMBINU YA SHULE HIYO

Uongozi wa shule ya Sekondari ya Jitegemee JKT ya Jijini Dar es Salaam wamesema wapo kwenye mkakati wa kuboresha miundombinu ya Shule hiyo ikiwa ni pamoja na kuondoa majengo yaliyochakaa ili kuwa na shule ya Jitegemee JKT mpya na kuongeza ufaulu.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa (SUMA JKT) Brigedia Jenerali Petro Ngata wakati wa mahafali ya 40 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Jitegemee JKT iliyopo Mgulani. 

Amesema ukarabati huo utafanyika kwa kuboresha madarasa, maabara na miundombinu yote ya Shule hiyo kwa ushirikiano wa uongozi wa Shule na Shirika la JKT ili kuboresha mazingira ya Shule hiyo.

"Tunataka Shule yetu ya Jitegemee JKT iwe na sura mpya, muonekano mpya hivyo wote tunawajibu wa kuchangia maendeleo ya Shule yetu kwa kuguswa kuchangia kuboreshaji huo kwa maendeleo shule yetu hii " amesema.

Amesema kuwa wanaendelea na ukusanyaji wa fedha za ukarabati huo sambamba na kuendelea kusimamia ufaulu wa Wanafunzi Shuleni hapo kwa kubadilisha mfumo wa kusoma na ufundishaji.

Aidha amewataka Wahitimu hao wa kidato cha nne nchini kote kuacha mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha badala yake watumie rasilimali za nchi kuongeza pato la Taifa.

Ngata amesema baadhi ya vijana wamekuwa na mawazo ya kwenda nje ya nchi kutafuta maisha mazuri na kuacha rasilimali zilizopo ambazo mataifa ya nje wanazifuata.

"Msitamani kwenda majuu kwani walioko huko wanatamani kuja huku kutumia rasilimali zetu ambazo Mungu ametubariki kuwa nazo na hazipo kokote kule zaidi ya Tanzania hivyo tumieni maarifa mliyopata hapa Shuleni  na  kuzitumia ipasavyo "amesema Ngata.
Naye Mkuu wa Shule hiyo Kanali Robert Kesi amesema kuwa wamewaandaa vizuri wanafunzi kwa kufanya mitihani mingi ya majaribio yenye hadhi ya kitaifa kwa nadharia na vitendo na wameiva. 

Awali akisoma risala ya wahitimu Shekha Said amesema kuwa moja ya mafanikio waliyopata ni kujifunza elimu ya ujasirismali ambapo wanaweza kutengeneza sabuni, kilimo cha mbogamboga, kutengeneza balbu zilizoungua na kurudi kufanya kazi kama zamani jumla ya wahitimu 89 wameagwa shuleni hapo.

Post a Comment

0 Comments