RC TABORA :MADIWANI SAIDIENI MAPATO YANAYOKUSANYWA KWA WINGI

NA TIGANYA VINCENT RS-TABORA

MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kuhakikisha wanasimamia Watendaji katika maeneo yao ili kuongeza juhudi katika makusanyo kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ili waweze kufikia au kuvuka lengo la asilimia 80 waliopangiwa.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili bajeti ya mwaka wa fedha ujao wa 2018/19.

Alisema kuwa kila Halmashauri hapa nchini imepangiwa kuhakikisha kuwa inafikisha au kuvuka kiwango cha asilimia 80 ya lengo katika makusanyo yake.

Mwanri alisema kuwa ili kufikia lengo hilo Madiwani wanalojukumu la kuhakikisha fedha zote kwa kutumia mashine za Kieletroniki (EFDs) ili kuhakikisha kuwa hakuna mianya ya upoteaji wa mapato ya Serikali kwa kutumia stakabadhi za kuandika.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alilitaka Baraza hilo kwa kushirikiana na Watendaji kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa ajili ya kuiongezea Halmashauri hiyo fedha ili iweze kuboresha huduma zaidi kwa wakazi wake.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Peter Nzalalila alisema kuwa hadi kufikia hivi sasa wameshakusanya asilimia 55 ya lengo walilopangiwa. Alisema kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha wanatarajia kufikia lengo walilopangiwa. Mwaka jana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Majaliwa Kassim Majaliwa akiwa katika ziarani mkoani Tabora alisema kuwa Halmashauri yeyote itakayoshindwa kukusanya mapato juu ya asilimia 80 itawachukulia hatua viongozi wahusika.

Post a Comment

0 Comments