Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akizunguma na Mtukufu Dk. Sheikh Sultan Bin Mohammed Al Qasimi alipofika katika makaazi yake kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake katika Nchi za Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu.
ZANZIBAR na Sharjah zimekubaliana kuendelea
kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao uliopo katika kuimarisha sekta mbali
mbali za maendeleo zikiwemo elimu na biashara,
Katika mazungumzo
yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Makaazi ya Mtukufu Dk. Sheikh Sultan Mohammed Al
Qasimi mjini Sharja, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein na kiongozi huyo wote kwa pamoja walisisitiza haja ya
kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kwa lengo la kuimarisha sekta hizo
muhimu za maendeleo.
Rais Dk. Shein kwa upande
wake alimpongeza Dk. Sultan kwa hatua zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuimarisha miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji.
Pamoja na hayo, viongozi
hao walizungumza jinsi ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuimarisha
sekta ya elimu hasa ikizingatiwa kuwa Sharjah imeweza kupata mafanikio katika sekta hiyo kutokana
na kuwa na miundombinu mizuri ya elimu vikiwemo vyo vikuu.
Aidha, Dk. Shein
alieleza haja kwa Sharjah kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar katika sekta ya
elimu kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), jambo ambalo Dk. Sheikh
Sultan Mohammed Al Qasimi ameliunga mkono.
Pia, viongozi hao kwa pamoja,
wameeleza namna ya pande mbili hizo kushirikiana katika sekta ya biashara hasa
ikizingatiwa kuwa kuna bidhaa ambazo ziko Zanzibar na zinatumika sana nchini
Sharjah vikiwemo viungo ambapo nchi hiyo wamekuwa wakinunua kutoka nchi za mbali
ikilinganishwa na masafa kati ya Zanzibar na Sharjah.
Dk. Shein, pia alitumia
fursa hiyo kumueleza Dk. Sultan hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Zanzibar
katika kuimarisha sekta ya utalii zikiwemo uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar
ambapo tayari serikali imejenga ukuta wa kuzuia athari za maji ya bahari katika
eneo la Mizingani kuelekea katika bustani ya Forodhani.
Kwa upande wake Dk.
Sheikh Sultan nae alimueleza namna Sharjah ilivyokuwa na uhusiano na ushirikiano
na Zanzibar kwa muda mrefu jambo ambalo amehakikisha ataliendeleza na
kuliimarisha kwa lengo na manufaa ya pande zote mbili.
Pia, Dk. Sheikh Sultan
alimuleza Rais Dk. Shein namna Sharjah ilivyopiga hatua katika sekta ya elimu
sambamba na inavyotoa fursa za ufadhili wa masomo na kusisitiza kuwa kuna kila sababu na Zanzibar nayo ikafaidika na fursa
hizo.
Aidha, Dk. Sultan
alimueleza Dk. Shein fursa mbali mbali za kibiashara zilizopo Sharjah na
kusisitiza haja ya kuwepo mashirikiano kati ya pande mbili hizo ili sekta hiyo
ilete manufaa kwa pande zote mbili hizo.
Katika kuendeleza na
kukuza sekta ya biashara na utalii kati nchi mbili hizo, Dk. Sultan alimueleza
Rais Dk. Shein umuhimu wa kuwepo usafiri wa ndege wa moja kwa moja kati ya Zanzibar
na Sharja na kusisitiza kupitia Shirika la ndege la Sharjah hilo atahakikisha
analiweka katika vipaumbele vyake katika kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo.
Katika ziara yake mjini
Sharja Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea eneo la shughuli za uvuvi la ‘East
Fishing Processing LLC”, lililoko Al Jurf
katika eneo la Ajman na kupata
maelezo juu ya namna ya eneo hilo lenye kiwanda kikubwa cha kisasa cha samaki jinsi
kinavyosarifu na kuhifadhi samaki pamoja
na kuwaweka katika mfumo maalum wa kwa ajili ya kuuzwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi
Mkuu wa Kampuni hiyo inayolishirikisha kundi la Kampuni ya THOMSUN, K.V. Thomas
alimueleza Rais Dk. Shein namna na kiwanda hicho kinavyosarifu samaki wa aina
mbali mnali wakiwemo kamba kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Tanzania.
Dk. Shein kwa upande
wake alipendezewa na namna kiwandaa hicho kinavyofanya kazi na kutokana na
juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
sekta ya uvuvi na viwanda vya samaki pamoja na azma ya kuanzisha Kampuni ya
Uvuvi,
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja ili
Zanzibar ipate kupanua wigo katika sekta hiyo.
Kutokana na kiwanda
hicho kutumia teknolojia ya kisasa katika kusarifu samaki wa aina mbali mbali
pia, soko la ajira limeonekana kuchukua fursa yake kutokana na kuajiri vijana
wengine hatua ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kupambana na
changamoto iliyopo katika suala zima la ajira.
Wakati huo huo, Dk. Shein na
ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein walitembelea katika shamba la ngombe wa maziwa la Al Rawabi, ambapo
pia eneo hilo lina viwanda vya vinywaji vya matunda pamoja na bidhaa nyengine
zinazotokana na maziwa.
Akiwa katika eneo hilo
la Al Rawabi, Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wake ambapo Mkuu wa Kampuni
inayosimamia Shamba hilo Abdalla Eleweis alimkaribisha Dk. Shein na ujumbe wake
na kumueleza namna eneo hilo linavyofanya shughuli zake za ufugaji wa ngombe
pamoja na uendelezaji wa viwanda vya matunda.
Nae Meneja Mkuu wa
Shamba hilo Dk. Ahmed Eltigani Al Mansour alimueleza Rais Dk. Shein na ujumbe
wake jinsi ya shamba hilo linavyofuga ngombe kwa kutumia teknolojia ya kisasa
ikiwemo kuwawekea viyoyozi na mafeni maalum kutokana na mazingira ya hali ya
hewa ya ukanda huo.
Kwa mujibu wa maelezo ya
Dk. Ahmed shamba hilo lina ngombe 12,500 ambapo kwa kila ngombe mmoja kwa siku
hutoa lita 60 za maziwa na kutoa lita 250,000 kwa siku huku akitumia fursa hiyo
kueleza siri ya mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na utafiti mkubwa walioufanya
kabla ya kuazisha ufugaji huo.
Dk. Ahmeda alieleza kuwa
ufugaji wanaoufanya ni ufugaji bora duniani na pia ni eneo lililopata mafanikio
makubwa ikifananishwa na ufugaji unaofanyika katika maeneo mbali mbali zikiwemo
nchi za Afrika na hata nchi zilizoendelea ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa
wingi.
Akimaliza ziara yake
katika eneo hilo, Rais Dk. Shein aliuhakikishia uongozi wa Al Rawabi kuwa
Zanzibar itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mashirikiano yanakuwepo
katika sekta hiyo ya ufugaji ikiwa ni pamoja na kupanua wigo na kujifunza jinsi
ya mafanikio hayo yalivyopatikana.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 Comments