KISARAWE KURINDIMA NUSU FAINALI JAFO CUP

Timu nne zinatarajiwa kushuka dimbani mwishoni  mwa wiki ikiwa ni katika mchezo wa  nusu fainali ya michuano inayoendelea ya 'Jafo Cup' Wilayani Kisarawe  Mkoa wa Pwani 

Akizungumza  na Waandishi wa Habari kwenye mkutano uliofanyika leo tarehe  16,Januari, 2025 Mwenyekiti wa  Kamati ya Maandalizi  Ally Mkomwa  amezitaja  timu  hizo kuwa ni Kisarawe , Kirui, Chole na  Marui .

"Michuano ya Jafo Cup imeanza mwaka jana 2024 na imeshirikisha  timu kutoka kata zote 17, vijiji 65 na Vitongoji 232 huku lengo kuu la michuano hii ni kuvumbua vipaji vya vijana na kuviendeleza kwa ujumla" amesema Mkomwa.

Mkomwa amesisitiza kuwa  mbali ya kukuza vipaji pia ni moja ya mchakato wa kuunda kikosi  cha timu itakayokuwa na jina la Mheshimiwa  Jafo    ambaye pia ndiyo Mbunge wa Jimbo hilo pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara. 

"Nusu fainali hizo  zitachezwa katika mtindo wa mechi ya nyumbani na ugenini huku Januari 17 timu ya Kisarawe itashuka dimbani kukipiga na Kirui kwenye Uwanja wa Manerumango  na Januari 18 siku ya Jumapili  timu  ya Chole  itacheza na  Marui  amesema Mkomwa.
Amezitaja zawadi wa washindi waliofuzu kuingia  nusu fainali  kila timu itapewa kitita cha 300,000  na jezi huku kwenye fainali  mshindi ataondoka na donge nono  kiasi cha Mil.2 pamoja na pikipiki mbili huku mshindi wa pili ataondoka na Mil.1 pamoja na pikipiki moja huku timu zitakazoshika nafasi ya nne na ya tano wapewa mipira.
Mjumbe wa Bodi chama Cha Mpira wa miguu na Mbunge wa Jimbo la kisarawe na Waziri wa Viwanda Selemani Jafo ametoa jezi seti nne na mipira 180 katika vijiji 65 na kata 17 vyote vya jimboni kwake  Kisarawe .

 Michuano hii  ipo katika hatua za lala salama 
kutoka katika makundi  matano kila Tarafa watakaocheza kwenye nusu fainali ambapo zitapatikana timu mbili zitakazocheza kwenye fainali ya michuano hiyo ya Jafo Cup.
Muamuzi Mkongwe na Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano ya Jafo Cup Ally Mkomwa akimkabidhi mpira na  jezi Kocha wa timu wa Kisarawe Muada Semkiwa Mhando kwenye hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi  wa mikutano  wa Halmashauri ya Kisarawe Mkoani Pwani leo Januari  16,2025.
Wakati huohuo  Afisa Michezo Wilaya ya Kisarawe  Dalidali Rashid ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo kwa moyo wake  na jinsi anavyojitoa katika kusaidia  michezo  kwenye ngazi mbalimbali  Jimboni kwake sambamba na  kutoa hamasa ya wapenda michezo wote nchini kujitokeza kwa wingi siku ya fainali ya Jafo Cup  itakayochezwa Manerumango  Februari 2 mwaka huu Wilayani Kisarawe  Mkoa wa Pwani. 

Mhe.Jafo ni Mjumbe wa Bodi Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoani Pwani.

Post a Comment

0 Comments