DKT. KIGWANGALLA AMWAGA CHECHE, AFUTA UTARATIBU WA UTOAJI WA VIBALI VYA UWINDAJI WA KITALII, AAPA KUTOYUMBISHWA NA RUSHWA NA FITNA

NA HAMZA TEMBA - WMU - DODOMA
...................................................................................
Katika kile alichoeleza kuwa ni kuimarisha sekta ya maliasili na utalii iweze kutoa mchango unaostahili kwa jamii na taifa kwa ujumla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amesitisha utaratibu wa kuhuisha upya vibali vyote vya makampuni ya uwindaji wa kitalii ambavyo vilitolewa mwaka huu mwezi Januari ili kupisha utaratibu mpya wa utoaji wa vibali hivyo kwa njia ya mnada.

Dk. Kigwangalla ametangaza uamuzi huo jana mjini Dodoma katika mkutano alioutisha wa wadau wa sekta ya maliasili na utalii ambao ulilenga kukusanya maoni, kero na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo muhimu nchini kwa ajili ya kuzitafutia utatuzi wa haraka.

“Kwa mamlaka niliyopewa na sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, nimeamua bila kushawishiwa na mtu yeyote yule wala kushauriwa na mtu yeyote yule zaidi ya kusikiliza tu ushauri wa kitaalamu na ushuari wa ndugu yangu Mhe.  Naibu Waziri, lakini  sasa hivi ninavyotamka haya sijamshirikisha mtu yeyote yule, nimeamua kwa mamlaka yangu, nasitisha vibali vyote  vya uwindaji wa makampuni ambavyo vilitolewa mwaka huu mwezi Januari kwa maana ya ‘kurenew’ (kuhuisha).

“Nasitisha ili kupisha mchakato wa kutengeneza taratibu mpya za kuendesha ugawaji wa vitalu kwa njia ya mnada, tunataka twende kwenye ‘auction’ (mnada) ya vitalu, na auction (mnada) iwe ya wazi, iwe na faida kubwa  zaidi, na natoa siku sitini utaratibu huo uwe umekamilika ili tuweze kuendesha ‘auction’ (mnada) kabla ya muda wa kuanza kwa awamu ya miaka mitano ambayo ni january 2018 mpaka 2022.

“Kwahiyo ndani ya siku sitini, wataalam mkae mniletee utaratibu wa namna bora zaidi ya uwazi inayotoa haki ya kugawa vitalu lakini pia yenye faida kubwa zaidi kama tunavyoelekezwa na mpango wa taifa wa miaka mitano kwamba ni lazima vitalu vyote vifanyiwe ‘auction’ (mnada)”. alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema utaratibu huo hautahusisha vitalu vilivyopo kwenye maeneo yenye migogoro ya ardhi kwa sasa mpaka pale migogoro hiyo itakapomalizika.

“Ni mwiko kugawa vitalu kwenye maeneo yenye mgogoro, kuna maeneo kama vitalu vilivyopo Loliondo, kuna mgogoro, ni mwiko kugawa vitalu, kuna maeneo kama Lake Natron kuna mgogoro, mwiko kugawa vitalu, mpaka tutatue migogoro kwanza, Kama kuna mtu alipewa kibali huko nyuma ajue hicho kibali cha renewal  kimekufa leo na mimi ndio nimekiua” alisema Dk. Kigwangalla.

Kuhusu uwindaji wa Wenyeji kwenye maeneo ya wazi uliosimamishwa kwa muda wa miaka miwili sasa, Dk. Kigwangalla alitoa muda wa siku sitini kwa watendaji wa wizara yake kukamilisha masharti mapya ya uendeshaji wa biashara hiyo na kuyawasilisha kwake aweze kuyasaini ili kufungulia biashara hiyo.

“Natoa siku sitini, wataalam wetu mnaohusika na utoaji wa vibali vya uwindaji wa wenyeji mkamilishe masharti mapya mniletee nisaini tutoe vibali, hatuwezi kuzuia wenyeji wanufaike na rasilimali ambazo ziko huko vijijini alafu tukaruhusu makampuni ya watu kutoka nje kuja kuwinda wakaondoka na nyama, ni lazima tutoe haki kwa wazawa kama wapo wanaovunja masharti sisi tudhibiti na tusimamie sheria” alisema Dk. Kigwangalla.

Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mej. Jen. Gaudence Milanzi kuwasiliana na Msajili wa Hazina kwa ajili ya kuanza mchakato wa kuzirudisha serikalini hoteli za kitalii kumi zilizobinafsishwa miaka 1990 kufuatia kushindwa kutimiza masharti ya mkataba wa uendeshaji.

“Niagize Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii uwasiliane na mamlaka ambayo ina dhamana ya kushikilia mali zilizokuwa za Serikali ambazo ziliuzwa kwa maana ya msajili wa hazina, umueleze nimetoa agizo kwamba hizi hoteli zote ambazo zimekiuka masharti na hivyo kuathiri utendaji wa sekta ya utalii nchini na hivyo kuathiri uchumi mpana wa taifa letu, zichukuliwe na zirudi kuwa mali ya serikali ili serikali ipate fursa ya kuzitangaza upya na kutafuta waendeshaji wapya watakaoweza kuendesha hoteli hizi  kwa tija na ufanisi kwa maana ya kukuza sekta ya utalii ambayo inachangia asilimia 17 ya pato la taifa.

“Nimetoa agizo hoteli hizi 10 ambazo zimeshindwa kukidhi masharti ya mikataba ya mauziano, mchakato wa kuzirudisha Serikalini uanze mara moja na ukamilike ndani ya siku sitini.

Alisema kumekuwepo na changamoto kubwa ya uhaba wa vyumba katika sekta ya utalii hali iliyosababishwa na ubinafsishaji wa hoteli 17 za Serikali uliofanywa miaka 1990 kwa nia njema ya kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa hoteli hizo kupitia sekta binafsi lengo ambalo halikufikiwa kwa baadhi ya hoteli hizo.

“Baada ya kufanya uchunguzi katika hoteli zote 17 tulizouza ni saba tu zinafanya vizuri, hoteli zinazofanya vizuri na zimekidhi masharti yote ambayo yalikuwepo kwenye ile mikataba ni Kilimanjaro Hotel, Kunduchi Beach Hotel, Mt. Meru Hotel, New Africa Hotel, New Safari Hotel, Mafia Highland Hotel na Hotel 77.

“Hoteli 10 zimeshindwa kukidhi masharti ya mikataba ya mauziano na mwaka ulioisha Serikali ilifanya uchunguzi kwenye hoteli nyingine nne kati ya hizo 10 ambazo ni Robo Wildlife Lodge, Seronera Wildlife Lodge, Ngorongoro Wildlife Lodge na Lake Manyara Hotel, na zote zilionesha zipo chini ya kiwango na hazikidhi mahitaji.

“Kwa kuwa watu hawa wamekiuka masharti ya ubinafsishaji kama walivyopewa wakati wananunua hizo hoteli ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kuvunja hii mikataba kuzichukua hizi hoteli na kuzibinafsisha kwa watu wengine watakaoweza kuziendesha kwa faida lakini pia kuziendesha kwa tija zaidi” alisema Dk. Kigwangalla.

Awali akijibu baadhi ya hoja za wadau wa mkutano huo kuhusu wizara yake kuwa na vishawishi vingi vya rushwa na fitna ambazo husababisha viongozi wengi kutodumu kwenye nafasi zao, Dk. Kigwangalla alisema kamwe hatoruhusu hali hiyo ijitokeze kwa kuwa hata aliyemteua anamjua vizuri kuwa ni muarobaini wa changamoto hizo.

“Mimi nipo hapa kwenye hiki kiti, na nitakuwepo kama sababu ni hiyo ya maslahi, Mimi sihongeki, sinunuliki, na sishawishiki, najua hata aliyeniweka hapa ananijua vizuri, kwahiyo alivyoniweka hapa alishajua hii ni dawa, muarobaini.

“Watu wote humu ndani tuna njaa, lakini njaa yangu nabaki nayo mwenyewe, bora nife kwa heshima zangu kuliko kuaibika na kudharaulika kwa kuchukua rushwa ama kwa kutokutenda haki ama kwa kumuonea mtu.

“Hilo nina uhakika nalo, kwa maana ya rushwa, maslahi ya kibiashara hapana, hutonikuta mimi huko, na kama kuna mdau mmoja anadhani kuna siku anafkiria anaweza kuja kuongea na mimi kwa maslahi binafsi akaweka mbele mazingira ya rushwa, sana sana ataona nimemuaga na kikao chetu kimeishia hapo, kwahiyo ukija kwangu njoo na ishu ambayo ipo straight maslahi ya umma yapo ndani yake utaraibu wa kisheria upo”. Alisema Dk. Kigwangalla.

Miongoni mwa maagizo mengine aliyoyatoa kwenye kikao hicho kwa watendaji wa wizara yake ni kuandaa taratibu za kuanzishwa kwa mwezi maalumu wa kuadhimisha utamaduni wa Mtanzania (Tanzania Heritage Month), Makumbusho ya Marais wa Tanzania (Presidential Museum) na Utalii wa Mabasi kwa Miji ya Dar es Salaam na Arusha (Dar Bus Tour/ Arusha Bus Tour) ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa watalii katika miji hiyo.

Katika mkutano huo wadau wa maliasii na utalii walipata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo ushauri na kero mbalimbali wanazokumbana nazo katika sekta hiyo ambazo ziliahidiwa kufanyiwa kazi kwa haraka na Waziri Kigwangalla.  Miongoni mwa ushauri na mapendekezo waliyotoa ni pamoja na kuanzishwa kwa mamlaka moja inayosimamia rasilimali za misitu nchini na kufunguliwa kwa biashara ya kusafirisha viumbe hai nje ya nchi.

Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa na viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili ambao ni Naibu Waziri, Mhe. Japhet Hasunga, Katibu Mkuu, Mej. Jen. Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki, Wakurugenzi wa Idara na Wakuu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo.


Wengine ni wadau zaidi ya 200 kutoka sekta mbalimbali ya maliasili na utalii ambao ni wawakilishi kutoka vikundi, taasisi, vyama na vyombo mbalimbali vinavyoshughulika na utoaji wa huduma katika sekta ya utalii, wanyamapori, misitu na nyuki pamoja na waandishi wa habari. 
Waziri wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa sekta ya maliasili na utalii kutoka nchi nzima katika mkutano aliotisha mjini Dodoma jana kwa ajili ya kupokea maoni, kero na ushauri mbalimbali wa kuboresha sekta hiyo. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Japhet Hasunga na kushoto kwake ni Katibu wa Wizara hiyo, Mej. Jen. Gaudence Milanzi. 
 Waziri wa wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa sekta ya maliasili na utalii kutoka nchi nzima katika mkutano aliotisha mjini Dodoma jana kwa ajili ya kupokea maoni, kero na ushauri mbalimbali wa kuboresha sekta hiyo. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Japhet Hasunga. 
 Mkutano ukiwa unaendelea.
 Mkuu wa Wilaya Chemba, Simon Odunga ambaye kabla ya kupewa nafasi hiyo na Mhe. Rais alikuwa mtumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii akichangia katika mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili, Dkt. Aloyce Nzuki akchangia hoja katika mkutano huo.
 Baadhi ya wadau wa sekta ya maliasili na utalii ambao walioshiriki kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexandre Songorwa akijibu baadhi ya hoja zilizoibuka katika mkutano huo.
 Mdau wa maliasili na utalii kutoka Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere, Asser Mwambene akichangia hoja katika mkutano huo.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo akijibu baadhi ya hoja zinazohusu taasisi yake kwenye mkutano huo.
 Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa akijibu baadhi ya hoja kuhusu Idara yake katika mkutano huo.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi akijibu baadhi ya hoja za shirika lake katika mkutano huo.
 Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Dkt. Fredy Manongi akijibu baadhi ya hoja kuhusu mamlaka hiyo katika mkutano huo.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori, Dkr. James Wakibara akijibu baadhi ya hoja kuhusu mamlaka hiyo katika mkutano huo.
 Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Shogo Mlozi akichangia baadhi ya hoja kuhusu chuo hicho katika mkutano huo.

Post a Comment

0 Comments