ZIFF KUBORESHA SOKO LA FILAMU

ZIFF KUBORESHA SOKO LA FILAMU

Na Husna Saidi MAELEZO

Filamu 23 za Kitanzania zimefanikiwa kushinda kinyang’anyiro cha filamu bora 132 zitakazoonyeshwa katika tamasha la Nchi za Jahazi linalotarajia kufanyika Zanzibar kuanzia tarehe 8-16 Julai Zanzibar.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa Tamasha hilo Fabrizio Combolo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu tamasha hilo ambalo linatarajia kushirika mataifa 70 kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Combolo alisema filamu zinazotarajiwa kuonyeshwa katika tamasha hilo ni filamu ndefu, filamu makala, filamu katuni na kwa mara ya kwanza Nchi ya Namibia imeweza kutayarisha filamu pamoja na filamu ya Winnie iliyotayarishwa kutoka Afrika Kusini.

“Kutakuwa na makala kutoka Afrika ya Kusuni yenye jina la Winnie ambayo itazungumzia maisha ya Winnie Mandera na kwa Tanzania kutakuwa na filamu yenye jina la Kiumeni ambayo imeshaanza kuonekana katika majumba ya sinema hapa nchini.

Alisema kutokana na kukua kwa soko la filamu nchini, tamasha hilo kwa mara ya kwanza litaziduliwa na filamu ya Kitanzania ya T-Junction, iliyotayarishwa na Amil Shivji, jambo ambalo ni tofauti na huko nyuma ambapo walikuwa wanazindua na filamu kutoka nje ya nchi.

Aliongeza kuwa tamasha hilo pia litakuwa na filamu ya makala maalum ya maisha ya Mwanamuziki wa Marekani, marehemu Winnie Hauston filamu iliyoandaliwa na Mtunzi Nick Bloomfield. Aidha Tamasha hilo pia litaweza kuonyesha filamu ya makala maalum ya Ujangili iliyorekodiwa hapa nchini ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanyamapori.

Kwa upande wake Afisa Habari na Masoko wa tamasha hilo Lara Preston alisema kuwa kwa mara ya kwanza wameamua kuwa na soko filamu litakalofanyika ndani ya ukumbi huo ili kutoa hamasa ya kukuza tasnia ya filamu katika Afrika Mashariki.

Nae Mwenyekiti wa Mfuko wa Emerson, Said Elg alisema kuwa wapo tayari kushirikiana na ZIFF katika kunyanyua soko la filamu hivyo katika tamasha hilo watatoa tuzo kwa washindi na kwa wanafunzi 15 kutoka vyuo vya filamu watakaofanya vizuri.

Tamasha hilo litahusisha tuzo mbalimbali ambazo ni:-Tuzo za nchi za Jahazi, Tuzo za Sembene Ousmane, Tuzo za filamu bora ya Afrika, Tuzo za Adiaha, Tuzo za filamu bora kwa wanawake, Tuzo za filamu bora ya Kimataifa, Tuzo za Zanzibar Emerson na Tuzo ya video ya mwanamuziki bora wa Afrika Mashariki.

Post a Comment

0 Comments