AFRIKA KUSINI KUENDELEA KUFUNDIAHA MARUBANI WA YANZANIAA

Na Husna Saidi & Jacquiline Mrisho- MAELEZO Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini imekubali kuendelea kuwafudisha marubani wa Tanzania ikiwa ni sehemu moja wapo ya kukuza maendeleo ya sekta ya uchukuzi na usafiri wa anga pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Augustine Mahiga ameyabainisha hayo leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu majadiliano ya awali yaliyofanyika kati ya nchi hizo mbili juu ya mikataba mbalimbali inayotegemewa kusainiwa Mei 11 mwaka huu. Balozi Mahiga alisema kuwa katika majadiliano hayo wamejadili mikataba iliyowahi kusainiwa kwa kupima utekelezaji wake pamoja na kujadili mikataba mipya iliyojikita katika sekta mbalimbali za maendeleo zikiwemo za uchukuzi, nishati, elimu pamoja na mawasiliano. “Katika sekta ya uchukuzi tumekubaliana kuboresha barabara, usafiri wa anga pamoja na reli hasa ya TAZARA, sisi tumenunua ndege na tunaendelea kununua zingine zitakazosafiri hadi Afrika ya Kusini hivyo nchi hiyo imekubali kuendelea kuwafundisha marubani wa Tanzania kuendesha na kukarabati ndege hizo,”alisema Balozi Mahiga. Aliongeza kuwa mikataba hiyo inayotarajiwa kusainiwa hapo kesho imelenga maeneo ambayo yatapewa kipaumbele katika ushirikiano huo yakiwemo ya uchumi, biashara na uwekezaji pia mikataba hiyo imewekewa utaratibu wa ufatiliaji na utekelezaji wake. Akiongea kuhusu kulinda uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Afrika Kusini Bi. Maite Nkoana - Mashabane alisema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kutafsiri ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yetu na kuufikisha kwa kizazi hiki na kijacho kwani kwa kusoma tu historia katika vitabu ni rahisi kwao kusahau hivyo mkutano huo utapelekea kuendeleza na kurithisha uhusiano uliopo baina ya vijana wa nchi hizo mbili. “Tanzania na Afrika Kusini tuna historia kubwa ya kushirikiana katika harakati za kutafuta ukombozi wa nchi zetu lakini haitoshi kuwa na urafiki wa kihistoria tu bali tuwe na urafiki utakaoleta maendeleo katika nchi zetu”, alisema Bi. Maite. Nae Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kuwa nchi ya Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi nne zinazowekeza nchini kwa kiasi kikubwa hivyo tayari wana mikataba mbalimbali ambayo wanaendelea kuiboresha ili kuendelea kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda. “Tumeshaongea na Waziri mwenye dhamana ya viwanda wa Afrika Kusini kwamba kuna ardhi kubwa katika eneo la Kilombero 1 na Kilombero 2 hivyo waongeze nguvu ya kuwekeza katika uzalishaji wa sukari kwenye eneo hilo,”alisema Mwijage.

Post a Comment

0 Comments