Na Hamis Dambaya, Havana.
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imeshiriki katika tamasha kubwa la kimataifa la lugha ya Kiswahili linaloendelea katika jiji la Havana nchini Cuba kwa lengo la kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro na vivutio vya malikale vinavyosimamiwa na mamlaka hiyo nje ya hifadhi.
Katika tamasha hilo NCAA imetumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo bonde la kreta ambalo ni kivutio kikubwa kwa watalii wengi wanaotembelea hifadhi hiyo, vivutio vingine ni pamoja na Kreta za Empakai na Olmoti, Mlima Lolmalasin, maporomoko ya Maji endoro, mapango ya tembo, makumbusho ya Olduvai, mchanga unaohama, gunduzi za nyayo wa binadamu wa kale katika eneo la Laetoli pamoja na vivutio vingine.
Akifungua tamasha hilo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Damas Ndumbaro amesema pamoja na ushiriki wa tamasha la kimataifa la Kiswahili lakini wananchi wa Cuba na mataifa mengine wanakaribishwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo ni vya kipekee vilivyopo nchini Tanzania.
“.
Tanzania inatumia fursa hii kutangaza vivutio vyetu vya utalii vilivyopo nyumbani na kwa namna ya pekee tunampongeza mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifungua nchi yetu katika kanda mbalimbali duniani”,alisema Dkt.Ndumbaro.
Kwa upande wake waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kindugu baina ya nchi hiyo na Tanzania na kusema kuwa kufanyika kwa tamasha la kimataifa la Kiswahili nchini Cuba linaimarisha zaidi ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Tamasha hilo la kimataifa ambalo limeanza tarehe 7 hadi 11 Novemba, 2024 linahudhuriwa na wadau kutoka mataifa mbalimbali duniani na lina lengo la kuhakikisha kuwa pamoja na mambo mengine lugha ya Kiswahili inaendelea kupenya katika wigo wa kimataifa ili iweze kuwa mojawapo ya lugha inayoongoza kuzungumzwa na watu wengi zaidi duniani
0 Comments