RAIS MAGUFULI ATOA AJIRA KWA MADAKTARI 258 WALIOOMBA KWENDA KENYA


Na Daudi Manongi-MAELEZO, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  John Pombe Magufuli ameamua madaktari 258 na wataalamu wa Afya 11 walioleta maombi na kukidhi vigezo kupitia Wizara ya Afya kwa ajili ya kwenda kufanya kazi nchini Kenya kuajiriwa na Serikali.
Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge Mjini Dodoma.
“Kwa upande wetu sisi ratiba ya utekelezaji wa ajira hizi za madaktari hao ilikubalika na pande zote iwe tarehe 6 Aprili 2017 na Madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya tarehe 6-10 Aprili 2017, hadi tarehe ya Taarifa hii Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa kuhusu Ajira za madaktari wa Tanzania nchini Kenya,” alisisitiza  Mwalimu.
Amesema kufuatia uamuzi huu majina ya Madaktari husika na vituo watakavyopangiwa kazi yatatangazwa katika Tovuti ya Wizara pamoja na wataalamu wengine wa afya 11 walioleta maombi yao na kukidhi vigezo.
Aidha Serikali ya Tanzania itakuwa tayari kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya kupatiwa Madaktari 500, pale ambapo hakutakuwa na vikwazo vya kupeleka madaktari wetu nchini Kenya.
Mnamo tarehe 18 Machi 2017 Ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya Dkt.Cleopa Mailu uliwasili nchini ambapo ulikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa madhumuni ya kuomba kuajiri kwa Mkataba Madaktari wa Tanzania mia tano(500) ili kupunguza uhaba wa Madaktari nchini Kenya na kukubali ombi hilo.
Aidha Maombi hayo yalipokelewa ambapo jumla ya maombi 496 yaliwasilishwa na baada ya kufanya uchambuzi wa maombi hayo ilibainika kuwa Madaktari 258 walikidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya,lakini wakati Serikali ya Tanzania ikiendelea kukamilisha utaratibu wa ajira za Madaktari hao Madaktari watano wa Kenya waliwasilisha pingamizi mahakamani kuitaka Serikali ya nchi yao kusitisha kuajiri Madaktari kutoka Tanzania.

Post a Comment

0 Comments