CDA YAKANUSHA UUZAJI VIWANJA MKONZE

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.

Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) imekanusha juu ya uvumi unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uuzaji wa viwanja katika eneo ka Mkonze lililopo mkoani Dodoma.

Tamko hilo limetolewa hivi karibuni mkoani Dodoma na Kaimu Meneja Uhusiano wa CDA, Angela Msimbira kutokana na kusambaa kwa ujumbe huo katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Angela amesema taarifa hizo ambazo hazieleweki zimekuwa zikidai kuwa viwanja hivyo ni halali na ukinunua unapewa hati na CDA ambayo ndiyo imepewa dhamana ya ugawaji wa viwanja mkoani humo.

“Mamlaka yetu inapenda kuutarifu Umma kuwa taarifa hizo si za kweli hivyo wananchi wanatakiwa kuzipuuza na kuendelea kufata utaratibu kwani mamlaka hiyo ina utaratibu uliopangwa wa namna ya kupata viwanja vilivyo halali,”alisema Angela.

Amefafanua kuwa Mamlaka hiyo inapotaka kuuza viwanja hutumia utaratibu wa kutangaza kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii pamoja na kutoa matangazo kwa umma kwa njia ya vipaza sauti. Aidha Angela ametumia fursa hiyo kuendelea kuwakumbusha wananchi kufuata taratibu za upatikanaji wa viwanja.

Kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Jinai Mitandaoni ya mwaka 2015, ni kosa kwa mtu yoyote kutangaza, kuchapisha au kueneza habari za uongo au uzushi katika mitandao.

Post a Comment

0 Comments