Mbunge wa Viti Maalum Kinondoni Mhe. Susan Lyimo(Kushoto) kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kawe Mhe.Halima Mdee (CHADEMA) wakifuatilia zoezi la upigaji kura wa Meya wa Jiji hilo leo uliofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam.
Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Edward Lowasa akimpongeza mshindi wa nafasi ya Umeya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Isaya Chacha mara baada ya kutangazwa mshindi leo jijini Dar es Salaam leo.
Na Anitha Jonas – MAELEZO
Kaimu Mkurugenzi Jiji la Dar es Salaam Bi. Sara Yohana amemtanganza Mhe. Isaya Chacha Diwani wa Kata ya Vijibweni (CHADEMA) kutoka Manispaa ya Temeke kuwa Meya Mpya wa Jiji hilo.
Kaimu Mkurugenzi huyo alimtangaza Isaya kuwa mshindi mara baada ya uchaguzi huo kufanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo mshindi alipata kwa kura 84 dhidi ya mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw.Yenga Yusuph ambaye alipata kura 67 wakati kura 7 ziliharibika katika uchaguzi huo.
“Tunawashuruku wapiga kura wote mlioshiriki zoezi hili la upigaji kura kwa utulivu bila vurugu na kuweza kufanikisha mpaka kumpata Meya wa Jiji hili” alisema Bi Yohana.
Kwa upande wa mshindi wa Kiti cha Meya wa Jiji Mhe. Chacha aliwashukuru wapiga kura wake wa kata ya Vijibweni kwa kumchagua kuwa Diwani pamoja uongozi wa chama chake kukubali kumpa nafasi ya kugombea kiti hicho.
“Nimejipanga kuleta maendeleo katika sekta ya elimu pamoja na kupambana na kero ya foleni katika jiji letu na nitahakikisha wananchi wote maskini wanafaidika na mapato ya jiji hili ikiwemo kuendeleza miundombinu mbalimbali ,”alisema Chacha.
Aidha, Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Bw.Freeman Mbowe alisema idadi ya wapiga kura tu inaonyesha wazi kuwa ushindi wa kiti hicho cha Meya ni lazima uchukuliwe na CHADEMA sababu madiwani wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanatoka katika chama hicho.
0 Comments