|
|
|
|
|
|
|
|
VICENT MBILINYI
Bondia anayetamani mafanikio
VICENT Mbilinyi miongoni mwa
mabondia wanaoanza kufanya
vizuri katika medani ya masumbwi
huku ndoto yake ikiwa ni kufanya
vema kitaifa na kimataifa ili
kujiweka katika ramani nzuri ya
mchezo huo Afrika na Dunia.
Nyota huyo kwa sasa ananolewa
na kocha wa kimataifa wa mchezo
huo hapa nchini, Rajabu Mhamila
maarufu kwa jina la Super D
ambaye anasifika kwa kukuza na
kuviendeleza vipaji vya mabondia
wachanga hadi kufikia mafanikio.
Wapo mabondia wengi ambao kwa
sasa wanaonekana kupiga hatua
nzuri katika mchezo wakiwa chini
ya Super D akiwemo Mbilinyi
ambaye hadi sasa ameshapigana
mapambano tisa huku akipoteza
moja na kushinda matano akitoa sare
mawili na kupoteza pambano moja.
Licha ya kutofanya vema katika
kupata ushindi,
mapambano mengi ambayo
amepigana ni moja ya njia sahihi ya
kupiga hatua nzuri katika mchezo
ambayo kila bondia anatamani
kufikia.
Akiwa katika mchakato wa kufikia
mafanikio, Mbilinyi anavutiwa
vema na bondia anayefanya vizuri
ulingoni Thomas Mashali 'Simba
Asiyefugika' ambaye kwa sasa
anajiandaa na pambano lake dhidi
ya Francis Miyeyusho Desemba 25,
mwaka huu mkoani Morogoro.
Mbilinyi anakiri kuwa sababu ya
kuvutiwa na Mashali ni namna
anapokuwa kwenye mawindo
ulingoni kwa maana anatumia akili
nyingi katika kushambulia na ni
mwepesi wa kurusha makonde na
kurudi haraka kwenye eneo lake.
"Napenda Mashali anavyokuwa
ulingoni na napenda kuwa kama
yeye na ndiyo maana nafanya
mazoezi kwa nguvu nikiwa chini ya
Super D na ninaamini ndoto yangu
ya muda mrefu itatimia ya kuwa
bingwa Afrika na Dunia.
"Ninachoomba tu mapromota
wanitafutie mapambano ya
kimataifa ili nioneshe uwezo
wangu kwa maana nia ninayo
kinachohitajika ni kupewa fursa
niitumie kuonesha kipaji changu
nilichojaaliwa na Mungu, Muumba
Mbingu na Ardhi na vyote
vilivyomo," anasema.
Nyota huyo ambaye ni mtoto wa
nne katika saba wa Mzee Alphonce
Mbilinyi ambaye ametangulia
mbele ya haki anasema kuingia
kwake katika mchezo huo ni
sehemu ya ndoto yake tangu akiwa
Shule ya Msingi Mzimuni iliyopo
Magomeni, Dar es Salaam.
Mbilinyi anasema licha ya kuingia
katika mchezo pia ni mchezaji
mzuri wa mpira wa miguu anafiti
vema akicheza namba tano na
Yanga ya Dar es Salaam ndiyo timu
anayoishabikia na kimataifa
anaihusudu Chelsea ya Uingereza.
Bangi
Nyota huyo anasema hajawahi
kutumia kilevi hicho kama ilivyo
kwa baadhi ya mabondia na
kufafanua hafikirii kukitumia kwa
maana ni moja ya kilevi
kinachoharibu mwili na mwelekeo
hususan kwa mabondia.
"Sifikirii kutumia kwa maana naona
namna inavyowaathiri baadhi ya
mabondia wanaotumia bangi
kwani wakati mwingine
wamekuwa wakifanya vitendo
viovu ndani au nje ya ulingo na
kusababisha kuharibu taswira
nzima ya masumbwi na kufanya
jamii kuutafsiri vibaya kumbe si
wote tuko hivyo," anasema.
Anafafanua kuwa baadhi ya
mabondia wanaamini kuwa bangi
ni moja ya chachu ya ushindi katika
mchezo kitu ambacho si kweli,
kinachotakiwa ni kufanya mazoezi
ya kutosha na kutumia mbinu za
mchezo ili kufanikisha ushindi.
Ushirikiana
Nyota huyo ambaye Desemba 25
mwaka huu anapanda ulingoni
kuzipiga na Deo Njiku katika
Uwanja wa Jamhuri mkoani
Morogoro anasema kuwa haamini
kama ndumba zinasaidia kushinda
pambano.
"Hizo ni imani potofu ambazo
hazina msingi katika mchezo wa
masumbwi kinachotakiwa ni
kujiamini unapokuwa ulingoni kwa
kumsoma mpinzani wako na zaidi
ni kufanya mazoezi ambayo ndiyo
yanayokuhakikishia ushindi na si
tofauti na hivyo," anasema.
Nje ya ndondi
Bondia huyo wa Kibaha mkoani
Pwani anasema kuwa nje ya
mchezo huo anashughulika na
biashara ndogo ndogo ambazo
zinasaidia kumweka vizuri katika
tasnia ya masumbwi nchini.
Anasema kuwa kama si kuwa na
biashara maisha yake yangekuwa
na changamoto nyingi katika
kuyaendesha kwa maana bado
hajapata mafanikio ya kuridhisha
kupitia masumbwi na kusababisha
kutumia kipato chake kukiiingiza
kwenye masumbwi.
Kwani mara kadhaa hutumia kipato
chake anachokipata kupitia
biashara kununulia baadhi ya vifaa
vya ndondi ambavyo vimekuwa ni
changamoto kubwa kwa mabondia
wanaoanza kupata majina kupitia
mchezo huo.
Hivyo anatoa mwito kwa mabondia
wanaochipukia kuwa na shughuli
tofauti ili kufanikisha kufanya
mchezo huo kwa umakini na
kusaidia kuondoa changamoto
nyingi zinazohitaji kusukuma
maendeleo ya masumbwi.
Bondia huyo anayepigania uzito wa
kilo 63 pia anatoa mwito kwa
mabondia wenye majina makubwa
ambao wanapata nafasi ya kucheza
mapambano ya kimataifa kuwa na
utaratibu wa kufanya mazoezi
mara kwa mara na kutosubiri safari.
Anafafanua kuwa jambo hilo
litasaidia kupata ushindi katika
michezo wanayopata kimataifa na
kutoa njia kwa wengine kupata
nafasi za kwenda nje ya nchi katika
mapambano.
|
|
0 Comments