Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mpiji Magohe Kata ya Mbezi, manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa kijiji hicho .
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki akizindua mradi wa maji uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 460 katika kijiji cha Mpiji Magohe, manispaa ya Kinondani jijini Dar es salaam leo wakati wa mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Maji yanayoendelea mkoani Dar es salaam.Kushoto kwake ni Mbunge wa Ubungo Mhe. John Mnyika na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Bi. Theresia Mmbando.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Said Meck Sadiki akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mpiji Magohe Kata ya Mbezi, manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam mara baada ya kuzindua mradi wa maji wa kijiji hicho .
Na Aron Msigwa – MAELEZO
WAKAZI wa kijiji cha Mpiji Magohe, Kata ya Mbezi wilayani
Kinondoni jijini Dar es salaam wamekubali kuyatoa maeneo ya ardhi wanayomiliki
bila fidia ili yaweze kutumiwa na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO)
kupitisha nguzo za umeme kuelekea mahali
ilipo pampu
ya kusukuma maji kwenye chanzo cha maji kijijini hapo ili waweze kupata huduma ya uhakika ya maji
kutokana na chanzo hicho kutumia umeme wa jenereta.
Wananchi hao wametoa uamuzi
huo leo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki ambaye
alikuwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji kijijini hapo,
yaliyoambatana na uzinduzi wa mradi
wa maji wa kijiji hicho
uliogharimu kiasi cha fedha za kitanzania zaidi ya shilingi milioni 460.
Akizungumza na wakazi hao,
Mhe. Sadiki amesema kuwa kukamilika
kwa mradi ni moja ya juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata maji
safi katika maeneo yao na kuongeza kuwa mradi huo utawanufaisha
zaidi ya watu 6600 wa kijiji hicho na kuondoa kero ya kupata maji safi iliyodumu
kwa zaidi ya miaka 20.
Amesema kuwa uamuzi
walioufanya wananchi hao kuruhusu maeneo yao kupitisha nguzo za umeme bila
kudai fidia ni wa kipekee na unafaa kuigwa na wananchi wa maeneo mengine ili
kurahisisha upatikanaji wa huduma zao za msingi na kuwaahidi wananchi hao kuwa
atawasiliana na mamlaka husika ili umeme wa TANESCO uweze kufika katika chanzo
chao cha maji kupunguza gharama za uendeshaji na kuharakisha kukamilishwa kwa
mradi huo.
Ameitaka kamati ya maji
inayosimamia mradi wa kijiji hicho kuhakikisha kuwa inafanya kazi kwa ufanisi,
uadilifu na uwazi ili kuondoa migogoro ya uongozi na wananchi hali inayoweza
kutishia uhai wa mradi huo.
“Natoa agizo kwa viongozi wa
kamati ya maji ya kijiji hiki muhakikishe kuwa mnafanya kazi zenu kwa ufanisi mkubwa,
uadilifu, mzingatie sheria na kuhakikisha taarifa za fedha za mradi hasa mapato
na matumizi mnazitoa kwa wananchi kila baada ya miezi 3 kulingana na mwongozo
uliopo” Amesisitiza.
Kuhusu maadhimisho hayo ya
wiki ya Wiki ya Maji ambayo huadhimishwa duniani kote kila ifikapo Machi 16
hadi 22 kila mwaka kuanzia ngazi ya taifa, mkoa na wilaya amesema kwa mwaka huu
jijini Dar es salaam maadhimisho hayo yameambatana na uzinduzi wa miradi ya
maji katika maeneo mbalimbali, utoaji wa elimu kuhusu huduma za maji , utunzaji
wa vyanzo vya maji na miundombinu ya maji kote nchini.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu pia yanawakutanisha wananchi na taasisi
za uendeshaji huduma, usimamizi na usambazaji wa maji ambazo hutoa elimu kuhusu
huduma za maji wanazotoa, kupokea maoni na kero za wananchi na kuendesha
operesheni mbalimbali za kuwakamata baadhi ya watu wanaoiba maji na kuhujumu
miundominu ya maji nchini.
Kuhusu usambazaji wa maji
katika maeneo mengine amesema kuwa uchimbaji wa visima 20 awamu ya kwanza imeanza
na itakamilika mwezi Agosti mwaka huu ikihusisha upanuzi wa mtandao wa
usambazaji wa maji katika maeneo yaliyo kandokando ya mabomba makuu kutoka Ruvu
chini na Ruvu juu na kuvinufaisha vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Bagamoyo
hadi eneo la Tegeta-Mpiji na vitongoji vilivyopo kati ya mji wa Mlandizi
–Kiluvya na maeneo ya Mbezi, Kimara na Goba.
Awamu ya pili itahusisha
upanuzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika maeneo yote ya jiji yatakayopata
maji kutoka Kimbiji na Mpera na maeneo mengine ya jiji yasiyo na mabomba ya
usambazaji wa maji.
Kwa upande wake Mbunge wa
jimbo la Ubungo Mhe. John Mnyika akizungumza na wakazi wa Mpiji Magohe
ameishukuru Serikali na wananchi wa kijiji cha Mpiji Magohe kwa kutoa
ushirikiano ambao
umefanikisha kukamilika kwa mradi huo.
Amesema yeye kama mbunge wa
eneo hilo ataendelea
kushirikiana na viongozi wa Serikali
wa mkoa wa Dar es salaam kuhamasisha maendeleo ya wananchi kushirikiana
kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji na kutoa wito kwa
wananchi kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji na kutunza miundombinu
iliyowekwa ili iendelee kuwa na manufaa kwa kipindi kirefu.
0 Comments