Na Raymond Mushumbusi -Maelezo
Manispaa ya Temeke imeandaa utaratibu wa kuondoa taka katika manispaa hiyo kwa kuongeza magari na vifaa ili kuyaweka mazingira katika hali ya usafi.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Manispaa ya Temeke Bi Joyce Msumba alipozungumza na Mwandishi Ofisini kwake wakati alipokuwa akijibu kuhusu kulundikana kwa taka katika Kata ya Keko iliyopo katika Manispaa hiyo.
Bi Joyce Msumba amesema kuwa taka zinazonekana zimelundikwa katika maeneo ya Manispaa ya Temeke sio madampo ila ni vituo vya ukusanyaji wa taka vilivyoteuliwa kukusanya taka kwa ajili ya kupekeka katika madampo elekezi na kuongeza kuwa taka hizo zimetokana na ufanyaji wa usafi wa tarehe 9 Desemba mwaka huu.
“ Tulipata tatizo la vifaa hasa magari ya kuzoa taka na Manispaa imeshaandaa pesa kwa ajili ya kukodi magari yatakayo zoa taka katika Manispaa yetu” alisema Bi Msumba.
Aidha msemaji wa manispaa hiyo amebainisha kuwa kuanzia kesho magari yataanza kufanya kazi ya kuzoa taka katika maeneo ya Manispaa ya Temeke ili kudhibiti hali ya mlundikano wa taka na wanaendelea kutangaza tenda za kupata wakandarasi wenye uwezo zaidi ili kumaliza tatizo hilo.
Pia ameongeza kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wananchi kuhusu usafi wa mazingira na uhifadhi wa taka sehemu husika na sio kulundika ovyo hali inayosababisha kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa kama Kipindupindu.
Mlundikano wa taka katika Manispaa ya Temeke umekuwa ni kero ya muda mrefu inayosababisha hatari ya kuweko kwa magonjwa ya mlipuko hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuondoa kero hiyo.
0 Comments