SIJUTII ADHABU , NAPUMZIKA :CHALZ BABA

MWANAMUZIKI mahiri pia kiongozi wa bendi ya Mashujaa  ya jijini Dar es Slaam , Charles Gabriel ‘Chalz Baba’ amesema kwamba  hajutii kutumikia adhabu yake  aliyopewa  kwa  kusimamishwa kufanya kazi kwa siku 21.

“Mimi wala sijutii kusimamishwa kupanda jukwani baada ya kupewa adhabu hiyo na  Ofisa Masoko wa bendi yetu ya Mashujaa Mathew Luhanga  kwani huyu jamaa tumekuwa hatupikiki chungu kimoja  hivyo sishangai kwa kunipa adhabu hii kwani itanisaidia mimi kupumzika na kazi ambayo nimekuwa kila siku niko jukwaani nikiitumikia” alisema Chalz alipozungumza kwa njia ya simu .

Aidha alikwenda mbali kwa kusema kwamba wakati akitumikia adhabu yake ataelekeza nguvu zake kwenye  eneo lake la ujenzi  wa nyumba yake Bunju  nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

“Nashukuru nimepata muda wa kusimamia matengenezo ya hapa na pale kwenye mji wangu” alisema Chalz.

Mwanamuziki huyo alikwenda mbali na kuongeza kwamba haoni kosa kubwa alilolifanya  kupelekea kupewa adhabu hiyo  na Luhanga kwa sababu ni jambo la kawaida kwa wasanii kusaidiana na kupanda kwenye majukwaa na kusalimia.

“Nakumbuka  wakati lilipofanyika tamasha la mwana Dar es Salaam nilikosekana ambapo nilipata lawama  hivyo nikaona kwenye tamasha hili acha niende ndiyo yamekuwa hayo lakini nilikwenda kwa roho safi ili kuwasalimu na mashabiki wangu walioko kwenye bendi ya Twanga Pepeta” alisema Chalz.

Akijibu swali kuhusu Meneja wa bendi ya Twanga kusema kwamba wako tayari  kuvunja mkataba na kumrudisha kundini alisema hilo wazo haliungi mkono kwa sababu  kupanda jukwaa  la Twanga hakumaanisha kwamba anarudi  kwani bado ana mkataba na Mashujaa hadi 2017.

Mwishoni mwa wiki  Meneja amasoko wa Mashujaa alitangaza kumsimamisha kazi Chalz kutokana na kosa la kutoroka  kazini  na kwenda kwenye onyesho la uzinduzi wa vyombo vipya vya bendi ya  Twanga Pepeta.

Ilidaiwa kwamba Chalz amesimamishwa kazi  kwa kile kinachodaiwa kukithiri kukiuka miiko ya kazi kwa mujibu wa mkataba wake. 

Jumamosi iliyopita, Chalz Baba aliibukia katika onyesho la bendi yake ya zamani, Twanga Pepeta ndani ya Mango Garden, licha ya kupewa tahadhari mapema na mwajiri wake kuwa asijihusishe na shoo hiyo iliyokuwa imealika wasanii kadhaa wa zamani wa Twanga.

Post a Comment

0 Comments