Pichani juu ni mabaki ya gari la mhandisi wa Shirika la ndege la Precision Air lililochomwa na raia wenye hasira baada ya kufyatulia risasi wachezaji hao.
NA MIKA NDABA
JESHI la Polisi Mkoa wa
Temeke linamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kuwa ni Mhandisi wa Shirika la Ndege
la Precision Air, Bathromeo Ngeleja baada ya kuwapiga risasi wachezaji wawili
wa mpira wa miguu.
Ngeleja alifanya tukio hilo
jana jioni maeneo ya Mashine ya Maji, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam,
baada ya mpira wa 'gozi' kuingia ndani ya uzio wa nyumba yake.
Tanzania Daima Jumapili
lilifika eneo la tukio na kushuhudia nyumba ya Ngeleja ambayo ni mali ya
Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam 'DAWASCO' ikiwa imealibiwa na
gari lake kuchomwa moto na wananchi wenye hasira.
Waliopigwa risasi ni kocha
na msemaji wa timu ya Dabani F.C Juma Yusuph na mchezaji wake Abdallah Anachu.
Akizungumza jama Kocha
Yusuph alisema kitendo walichofanyiwa ni cha kinyama kwa sababu hawakuwa na nia
mbaya isipokuwa walifuata mpira wao baada ya kuingia kwenye uzio wa nyumba ya
Ngeleja.
Alisema siku hiyo, alikuwa
na timu yake karibu na nyumba ya Ngeleja wakijiandaa kuingia uwanjani, lakini
kwa bahati mbaya mpira wao uliingia ndani ya uzio nyumba ya mzee huyo.
"Nilimtuma mchezaji
wangu akafuate mpira, lakini wakati anataka kuchukua ghafla tulisikia mlio wa
risasi ambao ilimpata mbavuni,"alisema.
Baada ya tukio hilo,
alimkimbilia Anachu ili aweze kumuokoa lakini ghafla na yeye alijikuta akipigwa
risasi ya mkono.
"Nashukuru mungu
naendelea salama, lakini mwenzangu bado hajaruhusiwa kwasababu aliumia sana na
yupo Hospitali ya Temeke lakini anaendelea vizuri,"alisema.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa huo,
Seleman Mpoyo alisema analaani tukio hilo la kinyama na kulifananisha na
matendo ya kigaidi.
"Katika hali ya kawaida
mtu mwenye akili huwezi kufanya jambo hilo, isitoshe wale wachezaji walikuwa
katika hali ya furaha ya kawaida tu, pia yeye mwenyewe ni mkazi wa eneo hili
kwanini afanye hivyo? "alihoji.
Hata hivyo, Mpoyo alisema
Ngeleja amekuwa na tabia ya kupiga risasi hovyo na kupasua mipira ya wachezaji
kwa kutumia risasi pindi inapoingia ndani ya uzio wa nyumba yake.
Mmoja wa Polisi aliyekuwa
akituliza ghasia katika eneo hilo, alisema matukio kama hayo yanaibua hasira
kwa wananchi na kuamua kujichukulia sheria mkononi.
"Huyu mzee labda
akapimwe akili kwa sababu jana wakati tunamuokoa alikuwa anacheka, isitoshe
sisi wenyewe silaha zilituishia na idadi ya wananchi ilikuwa kubwa mno zaidi ya
watu 200 walituzingira unafikiri ingekuaje? alihoji.
0 Comments