BASATA Arts Centre
Tel. 2863748/2860485
Fax: 0255- (022) – 286 0486
Ilala Sharif Shamba
P.O. Box. 4779, Dar es Salaam
E-mail:basata06@yahoo.com
BASATA YALAANI TABIA CHAFU NA ISIYO NA
MAADILI ILIYOONESHWA NA MSANII SHILOLE KWENYE ONESHO LAKE NCHINI UBELIGIJI
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na burudani nchini
limeona picha chafu na zisizo na maadili za Msanii Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole
alipokuwa akifanya onesho lake nchini Ubeligiji hivi karibuni.
Katika
picha hizo ambazo zimelaaniwa na watanzania wengi nchini kupitia njia
mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, Shilole anaonekana akiwa Jukwaani huku
viungo vyake vya sehemu za siri vikiwa hadharani na zaidi akionesha tabia
ambazo kwa kiasi kikubwa zimefedhehesha na kuidhalilisha sekta ya Sanaa na
Taifa kwa ujumla.
Aidha,
BASATA limepokea malalamiko kwa njia ya simu na mawasiliano ya internet kutoka
kwa watanzania waishio ughaibuni wakilaani tukio la Msanii huyo. Katika
mawasiliano yao wameeleza kwamba wamefedheheshwa na kudhalilika na tabia hiyo
chafu iliyooneshwa na msanii huyu.
Ikumbukwe
kwamba, Shilole ni msanii aliyesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa, hivyo anapokwenda
nje ya nchi kabla hajapata visa anapewa barua ya utambulisho kama msanii wa
Tanzania, hivyo anapokuwa nje ya nchi anatambuliwa kama msanii Mtanzania,
anapofanya kinyume na misingi ya kazi ya Sanaa, anajifedhehesha yeye mwenyewe,
kazi ya Sanaa na nchi yetu pia.
Aidha,
ikumbukwe kwamba BASATA limeshapata kumwita na kumuonya msanii huyu kutokana na
tabia yake ya kutokujiheshimu pale awapo jukwaani na yeye aliahidi kubadilika
na kuachana na tabia hiyo chafu. Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio hayo
na kwa sasa katika ardhi ya nchi nyingine ni uthibitisho kwamba hajabadilika na
kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye
kujitambua na kuiheshimu Sanaa kama kazi nyingine.
BASATA
linapenda kueleza kwamba;
1. Litamuita
kwa mara nyingine tena kumtaka ajieleze kwa nini alifanya onesho hilo la
kujidhalilisha na kudhalilisha hadhi ya mwanamke, msanii na Sanaa kwa ujumla
2. Kama
maelezo yake hayataridhisha hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake
maana tayari ameshadhihirisha kwamba akifanyacho si Sanaa na hakina uhusiano na
kazi ya Sanaa ambayo ina heshima yake na inahitaji ubunifu, weledi na
kujitambua
BASATA
linawakumbusha wasanii wote nchini kuwa Sanaa ni kazi kama kazi zingine lakini
siku za hivi karibuni wasanii wengi wamekuwa wakikiuka suala zima la maadili
kwa kutengeneza kazi chafu zisizofaa mbele ya jamii ya watanzania wanaoipenda
na kuiheshimu kazi ya Sanaa yenye staha. Tuungane kwa pamoja kukemea kazi chafu
zinazozalishwa na wasanii wasiojitambua kwani suala la maadili ni suala
mtambuka na linaanzia katika ngazi ya familia.
Aidha,
BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara
wanapopata mialiko ya kikazi kwenda nje ya nchi. Linawakumbusha kwamba
haiwezekani msanii kutumia picha chafu na mavazi dhalili na kuonyesha utupu
katika kuvuta mashabiki.
Sanaa
ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey
Mngereza
KATIBU MTENDAJI
0 Comments