MKURUGENZI wa Kampuni ya Msama Promotions ambayo ndio inaandaa matamasha ya
Pasaka na Krismasi, Alex Msama amekemea waimbaji wa muziki wa injili Tanzania
akiwataka kufanya kazi ya Mungu na
kuachana na siasa ambazo zinawaondoa kwenye uinjilisti.
Msama ameyasema hayo wakati tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Madiwani,
Wabunge na urais unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Msama anasema karipio hilo linawahusu pia viongozi wa dini wakiwamo wachungaji
na maaskofu ambao wanaonyesha nia ya
kutaka kuwania uongozi wa kisiasa katika nafasi hizo tatu.
Sababu za Msama kukemea waimbaji wa injili kujihusisha na wanasiasa wakiwamo
wagombea urais, kuna baadhi ya waimbaji wametunga nyimbo za ‘kuwatukuza’
wagombea urais wakati wao wanatakiwa muda wote kumtukuza Mungu na si binadamu
wenzao.
“Waimbaji tunatoka katika mstari, kwani Mungu anawategemea kufikisha ujumbe
wake kwa lengo la kuachana na machukizo ambayo yanapoteza mwelekeo wa jamii
mbalimbali ambazo zinahitaji maono ya Wainjilisti,” alisema Msama na kuongeza:
“Waimbaji ambao ninashirikiana nao katika kufikisha huduma ya neno la
Mungu, nashangaa wanatoka katika mstari, nawaomba wamrudie Mungu kwani
wanapotea wakiwatumikia mabwana wengine.”
Alisema kitendo wanachokifanya waimbaji na wachungaji ni kinyume na huduma
ndani ya mioyo yao kwa sababu wanachokifanya si sahihi.
Anafafanua kwamba kazi ya muziki wa injili ni kuhubirisha, waimbaji ni wainjilisti
wanawatoa waovu kwa shetani na kuwapeleka kwa Mungu ambaye ndiye tegemezi kwa
binadamu wote.
“Ni jambo la kusikitisha sana, wanamhuzunisha Bwana Yesu, alipoondoka
kwenda mbinguni aliwaambia wafuasi wake,
nendeni ulimwenguni kote mkaihubiri injili yangu, mwenye kuamini
ataokoka na asiyeamini ameangamia,” alieleza Msama.
Anasema kwa kufanya hivyo waimbaji hao ndio wanahubiri uovu kwa kuwapamba
wachafu na kuwafananisha na Yuda
Eskariot aliyemsaliti Yesu kwa ajili ya
pesa na kuwataka waliofanya hivyo waache mara moja.
Msama anaendelea kueleza na kufafanua kupitia maandiko matakatifu kwamba ya Kaisari wamwachie Kaisari, mwenye
kupewa sifa na wao ni Mungu peke yake, mwanadamu hawezi kupewa sifa na
kuinuliwa kwa sifa.
Pia anawakemea wagombea urais waache kuwatumia waimbaji wa injili na kujificha kwenye kanisa kwamba
ndio sehemu ya kuombea kura na kugawa pesa makanisani, Mungu hahongwi na waache
pia kumchokoza Mungu kwani akichukia zaidi mwisho wake ni mbaya.
Anasema siasa na dini ni vitu viwili tofauti kwani kwenye siasa uongo ni
mwingi ambao katika uinjilisti hautakiwi kwa sababu unakwenda tofauti na
maandiko matakatifu ya Mungu.
“Nahuzunishwa na wanaotumia mfumo huo kwa sababu siasa inayohubiriwa ni ya
kumjenga mgombea urais na kumpamba, wakati katika maandiko matakatifu hakuna
mambo ya kupambana kama inavyofanyika sasa,” alisema.
Anaeleza kwamba wachungaji wanasahau kazi zao ambazo ni kuwachunga kondoo
wa Mungu na kuhubiri injili na si
lingine lolote.
“Nia zao wakazitangaze huko na wakiendelea nitawaweka hadharani kwani
nitawaumbua kwa kuwaeleza kwamba hawafai kuwa marais kwa mtindo wanaoutumia,”
alisema.
Msama ndiye ‘anayedili’ na waimbaji wa muziki wa injili waache na watubu
sambamba na kukiri makosa yao kwa Mungu na waachane na dhambi ambayo ni kero
kwa Mungu.
Wachungaji wanaojielekeza kwenye siasa waache mpangilio huo kwa sababu
haiwezekani kuwatumikia mabwana wawili na kazi yao kwa Mungu ni injili pekee.
“Ukijikita huko utakuwa huna muda wa kumtumikia Mungu, siasa inasababisha
kusema uongo wakati uchungaji una heshima kubwa,” alisema Msama.
0 Comments