TASWA FC 'KUSHINE' NA UZI MPYA WA RANGERS BUREAU DE CHANGE



 Mkurugenzi wa Rangers Bureau De Change na Rangers Tours and Travel Agent, Daudi Madega (kushoto) akikabidhi jezi kwa mwenyekiti wa Taswa FC,  Majuto Omary katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya kampuni hiyo, Magomeni.
Nahodha wa timu ya soka ya wandishi wa habari za michezo nchini, Mbozi Katala akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo.
Na Mwandishi Wetu, Dar
Duka la kubadilishia fedha za kigeni la Rangers Bureau De Change lililopo Magomeni Mapipa, limetoa msaada wa jezi kwa timu ya soka ya Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa FC)  kwa ajili ya kuzitumia katika mechi zake mbali mbali za kirafiki na mashindano.
Mkurugenzi Mkuu wa Rangers Bureau De Change na Rangers Tours and Travel Agent, Daudi Madega alikabidhi jezi hizo kwa mwenyekiti wa Taswa FC,  Majuto Omary katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya kampuni hiyo, Magomeni.
Madega alisema kuwa wametoa msaada huo kama mchango wao kwa timu hiyo ambayo inaonyesha mfano kwa kujishughulisha na michezo mbali ya kuandika.
Alisema kuwa Taswa FC imedumu kwa muda mrefu na wao kama wadau wakuu wa michezo nchini, wameamua kuanza na timu hiyo na baadaye kuipa vifaa vya michezo timu yao ya netiboli (Taswa Queens) ambayo ipo katika kiwango cha juu.
“Rangers Bureau De Change na Tours and Travel Agent ni wadau wakuu wa michezo hapa nchini, hii inatokana na mmiliki wake kuwa na timu ya soka (Baker Ranger) ambayo ina historia kubwa katika soka la Tanzania, hivyo msaada huu si wa kubahatisha, tunaahidi kufanya makubwa na timu ikiwa kuwapa mabasi yetu mbali mbali mbali katika safari za timu,” alisema Madega.
Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omary aliishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo na kuahidi kuutumia kwa mafanikio ya timu na wala si vinginevyo.

Post a Comment

0 Comments