CHUJI APIGWA STOP YANGA, OKWI NAYE YUPOYUPO TU




SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeikumbusha klabu ya Yanga SC kutomtumia kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ katika mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya Komorozine ya Comoro, wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuwa bado anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata kwenye msimu uliopita.
Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto amewaambia Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kwamba, CAF iliwaandikia barua kuwakumbusha kuwa  Chuji alipewa kadi nyekundu mara ya mwisho klabu hiyo ilipocheza michuano ya Afrika katika mechi dhidi ya Zamalek hivyo Yanga haitamtumia Chuji hadi atakapomaliza adhabu yake

Pia Kizuguto pia amesema hawatamtumia mshambuliaji Emmanuel Okwi japokuwa CAF imempa leseni ya kucheza michuano hiyo mwaka huu, hadi hapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litakapotoa baraka zake.
Okwi amesajiliwa msimu huu Yanga SC kutoka SC Villa ya Uganda baada ya kugoma kuendelea kuichezea Etoile du Sahel ya Tunisia iliyomsajili kwa Mkataba wa miaka kutoka Simba SC ya Tanzania pia.
Okwi alifungua kesi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) akilalamika kutolipwa mishahara na Etoile ndipo akaruhusiwa kujiunga na SC Villa.

Baada ya Villa kumuuza Yanga ikidai ina haki zote, TFF imeandika barua FIFA kutaka ufafanuzi kama inaweza kumuidhinisha kucheza Yanga na imeizuia klabu hiyo kumtumia hadi majibu yapatikane.

Yanga ilitolewa Raundi ya Kwanza katika Ligi ya Mabingwa mwaka 2012 na Zamalek ya Misri, mechi ya kwanza wakilazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Februari 18, na marudiano Machi 3, wakifungwa 1- 0 Cairo.

Post a Comment

0 Comments