Na Happiness Katabazi
RAIA wa Uingereza, Ahassan, jana
aliunganishwa kwenye kesi ya wizi wa paspoti
26 inayomkabili msanii wa muziki wa asili nchini, Chigwele Che Mundugwao na
wenzake ambao wanaendelea kusota gerezani tangu Mei 3, mwaka huu, kufuatia
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi kuwafungia dhamana.
Wakili mwandamizi wa serikali, Tumaini Kweka
mbele ya Hakimu Sundi Fimbo, alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili
ya kutajwa ikiwa na jumla ya washitakiwa wanne.
Hata hivyo akasema upande wa
jamhuri unaomba kubadilisha hati ya mashitaka kwa sababu inamuunganisha
mshitakiwa mwingine ambaye ni raia wa Uingereza na kwamba upelelezi wa kesi
hiyo bado haujakamilika.
Wakili Kweka pia aliomba mahakama isitoe
masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo kwani upande wa jamhuri utaleta hati ya
DPP ya kumfungia pia dhamana kama washitakiwa
wengine kwa mujibu wa kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai ya mwaka 2002.
Hakimu Fimbo alikubali ombi
hilo na kusema sasa hati ya mashitaka itasomeka kuwa ina jumla ya washitakiwa
watano na akautaka upande wa jamhuri ulete kwa maandishi hati hiyo ya DPP ya
kumfungia dhamana mshitakiwa huyo wa tano na akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai
22 mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Ameamuru washitakiwa wote
warejeshwe rumande.
Mbali ya Che Mundugwao,
washitakiwa wengine ni Ofisa Manunuzi wa
Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (31), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Uokoaji,
Keneth Pius (37) na mfanyabiashara Ally Jabir
(34) wanaotetewa na wakili Peter Kibatara.
Mei 3, mwaka huu, Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana
aliwasomea mashitaka washitakiwa hao na kudai kuwa wanakabiliwa na kosa la kula
njama kutenda kosa hilo
kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
Wakili Komanya alieleza kuwa
kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu, Shimweta akiwa ni mtumishi wa umma katika
Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji aliiba paspoti 26, mali
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Komanya alidai kuwa
washitakiwa Che Mundugwao, Keneth na Ally, Mei 30, mwaka huu, huko Yombo Makangarawe
jijini Dar es Salaam walikamatwa wakiwa na pasipoti hizo 26 za wizi.
Kuhusu Che Mundugwao, wakili
Komanya alidai kuwa mshitakiwa huyo kuwa Aprili 22, mwaka huu alikamatwa
akimiliki paspoti 12 za watu wengine bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi .
Wakili huyo wa Serikali,
aliendelea kudai kuwa Mei, mwaka huu Che Mundugwao pia alikamatwa na maofisa
wanausalama akimiliki pasipoti nyingine mbili zenye majina ya watu wengine bila
sababu yoyote ya msingi.
Komanya aliendelea kuwa
Aprili 24 mwaka huu, mshitakiwa Ally alighushi paspoti yenye namba AB 65196 akionyesha
kuwa ilikuwa ni halali na kwamba ilitolewa na Idara ya Uhamiaji wakati akijua
kuwa si kweli.
Wakili Komanya alidai kuwa
kati ya mwaka 2007 na 2011 Dar es Salaam,
Shemweta alighushi nyaraka ya serikali ambayo ni muhuri akijaribu
kuonyesha kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni halali na kwamba zimetolewa na Idara ya
Uhamiaji wakati si kweli.
0 Comments