NIANZE kwa kuwapa pole wasanii wa muziki na watanzania
kwa ujumla, kutokana na msiba wa msanii Albert Mangwea ‘Ngwair’ aliyefariki
usiku wa kuamkia Jumanne nchini Afrika Kusini.
Hakika, siku
zote msiba uusikie kwa mwenzako, kwani ukiwa kwa jirani unaweza usiwe na
maumivu juu ya kile kinachomuumiza.
Lakini, hapo
hapo pindi anapofariki mtu maarufu, lazima jamii husika itakuwa imepatwa na
mshtuko, ndiyo maana nimeanza kwa kutoa pole kutokana na msiba wa Ngwair.
Ni kweli
inauma, lakini chanzo cha kifo cha msanii huyu kinasikitisha sana, hasa baada
ya kuthibitishwa kwamba, kimesababishwa na ulevi wa kupindukia.
Jamani, hivi
kwa mienendo hii ya wasanii wetu, nchi yetu itakuwa taifa la watu gani, ambao
wamekubuhu kwa kutumia mihadarati?
Katika hili,
serikali ina wajibu wa kupambana na hao wanaowatumia wasanii wetu kama ndiyo
wateja wao wakuu wa biashara hiyo haramu, inayoendelea kuangamiza nguvu kazi ya
taifa.
Kama hiyo
haitoshi, hata wabunge pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, mna
wajibu wa kulisemea hili huko bungeni.
Kwa upande
wa wabunge vijana, ambao tayari mko ndani ya mjengo, msifurahie tu malipo na
posho mnazopata bungeni, bali mnawajibu wa kuwatetea vijana wenzenu walioko nje
ya bunge.
Inauma sana,
taifa kupoteza nguvu kazi ya kijana kama ‘Ngwair’, kwani hakuna aliyetaka au
kukubali kwamba, msanii huyu amefariki dunia, lakini hivyo ndivyo ilivyo na
ukweli utabaki kuwa hivyo.
Ngwair
aliyezaliwa mwaka 1982, na jina lake lilikuja juu wakati akiwa na kundi la East
Zoo lililokuwa na maskani yake mkoani Dodoma.
Pia,
ningependa niupongeza uongozi wa Shirikisho la Muziki wa Tanzania, chini ya Rais, Ado November ambaye kitaaluma ni Wakili , kwa kuubeba
msiba huu, ikiwamo kuurudisha mwili wa marehemu utakaoagwa kesho katika viwanja
ama eneo litakalotangazwa baadae na kwenda kuzikwa mkoani Morogoro.
Wadau
mbalimbali wa muziki nchini, wakubwa na wadogo, wameonekana kuguswa na msiba
huu na katika hili, wengi wao hasa wanamuziki wakongwe, wamejikuta wakishikwa
na kigugumizi na kushindwa kuzungumzia.
Kiukweli,
msiba wa Ngwair umenishtua hata mimi binafsi na hata ninapoandika Busati hili,
siamini kile kilichotokea, lakini ndiyo imeshakuwa na mapenzi ya Mungu
yametimia.
Ngwair,
atakumbukwa kutokana na ucheshi, kujituma katika kazi yake ya muziki na
kupambana hata pale alipokutana na changamoto mbalimbali, ikiwemo mapromota
waongo.
Jambo zuri lingine
ambalo litabaki kuwa taswira nzuri na mfano wa kuigwa, ni Ngwair kutokuwa na
historia ya kuwa na mifarakano na wasanii wenzake na hii ndiyo sababu kubwa
inayowaumiza wengi, hasa waliyofanya naye kazi katika enzi za uhai wake.
Bwana alitoa
na bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amin.TANZIA HII IMEANDALIWA NA BONGOWEEKEND.BLOGSPOT.COM
0 Comments