Na Peter Mwenda
HOSPITALI zote za Serikali zimeonywa kuacha
tabia ya kuuza damu kwa hospitali binafsi wakati inatolewa bure kwa kila
anayehitaji huduma hiyo nchini.
Ofisa Mwendeshaji wa Mpango wa Damu Salama Tanzania, Dkt. Abdu Juma
aliyasema hayo wakati wa uchangiaji damu uliofanywa na waumini wa
Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri kushirikiana na Mpango wa Damu Salama
Tanzania uliofanyika nchini kote jana.
Dkt. Juma alisema wamepata
taarifa kuwa hospitali za Serikali za Mikoa zimekuwa zikiuza damnu kwa
hospitali binafsi na kuonya kuwa watakaokamatwa watachukuliwa hatua za
kisheria.
"Tunapeleka damu hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
Hospitali ya Manispaa ya Ilala, Hospitali ya Manispaa ya Temeke lakini
tunasikia damu hiyo inatolewa hapo kupelekwa hospitali za binafsi"
alisema Dkt. Juma.
Alisema mwaka huu Mpango wa Damu Salama ulikusanya chupa 106,000 tu
ambayo ni sawa na asilimia 76 ya lengo ambalo ni chupa 400,000 kwa
mwaka.
Dkt. Juma aliwashauri wananchi kujitokeza kuchangia damu
kwa hiari hasa kipindi hiki ambacho wachangiaji wakubwa ambao ni
wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wanakwenda likizo.
Alisema
ili kuongeza makusanyo ya damu aliwaomba watanzania kujitokeza
kuchangia kupitia kwenye kanda zao zilizoko katika mikoa ya Morogoro,
Dodoma, Arusha, Mtwara, Lindi, Kilimanjaro na Dar es Salaam.
Kiongozi
wa utoaji Damu wa Khoja Shia Ithnasheri,Aliabdu Mamdani alisema kambi
ya utoaji damu ya Ashura ambayo hujitolea kila Novemba 24 ya mwaka kutoa
damu kwa hiari mwaka huu wanatarajia kukusanya chupa 350-400 za damu.
"Nawaomba
wanajumuiya wote wa Khoja Shia Ithnasheri wa mikoa ya Morogoro, Arusha,
Mtwara, Lindi, Mwanza na Dar es Salaam kujitokeza kutoa damu kuokoa
maisha ya watanzania wanayopotea kwakukosa damu hospitalini" alisema
Mamdani.
Ofisa Mawasiliano wa Mpango wa Damu Salama Tanzania,
Rajab Mwenda alisema taarifa ya idadi ya chupa za damu zilizokusanywa
sioku ya Ushura na waumini wa Shia Ithnasher itatolewa baadaye.
0 Comments