SHIRIKISHO LA FILAMU (TAFF) KUWAKAANGA WEMA , AUNT EZEKIEL


"Kama Wema alilalamika kwamba zile picha ni za 'Technical', lakini zinaonekana wazi kabisa kwamba ni za ukweli wala hazijahaririwa, hivyo tumewaita na tuna mamlaka yote ya kuwashughulikia,".
 ...................................
SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF), limewataka wasanii wa Bongo Movie’ Wema Sepetu na Aunt Ezekiel kufika katika ofisi za Shirikisho hilo ili kujieleza kutokana na madai ya kuonyesha picha za utupu kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Wasanii hao ambao wamekuwa wakizunguka katika ziara ya tamasha mojawapo linaloendelea hapa nchini, na kupanda jukwaani huku wakiwa wamevaa nusu uchi na kuonesha baadhi ya maungo yao ya ndani, kinyume na maadili ya Kitanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TAFF, Wilson Makubi alisema, wasanii hao wamepelekewa barua ya kuitwa na kuwataka wafike katika ofisi za shirikisho hilo leo saa 7:00 mchana ili kujieleza kile wanachotuhumiwa nacho.

Alisema, shirikisho pamoja na wasanii wengine katika tasnia hiyo, wamehuzunika na tabia hiyo iliyofanywa na wasanii hao, hivyo leo watajieleza na litatolewa tamko dhidi yao.
"Kama Wema alilalamika kwamba zile picha ni za 'technical', lakini zinaonekana wazi kabisa kwamba ni za ukweli wala hazijahaririwa, hivyo tumewaita na tuna mamlaka yote ya kuwashughulikia," alisema Makubi.

  Makubi alisema, wamekaa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na wamepewa maagizo yote ya kuwashughulikia wale watakaoishusha thamani tasnia ya filamu hapa nchini.

"Ni mambo ya kufedhehesha sana, kuona msanii anafanya mambo kama haya, haipendezi kwa kweli, TAFF imehuzunika sana na ndio mana tumeamua kesho (leo), tukae nao ili wajieleze tusije tukatoa hukumu kabla hatujasikiliza upande wa pili," alisema Makubi na kufafanua kuwa, wasanii hao kama hawatofika katika kikao cha leo, shirikisho hilo litatoa adhabu kali dhidi yao. 

Post a Comment

0 Comments