Debora Nyange.
Na Kaka Mwinyi
Bendi mahiri ya muziki wa dansi kwenye mahoteli na shughuli mbalimbali, The Kalunde Band ya jijini Dar es Salaam, imejizatiti kwa maonesho yake baada ya kutengeneza nyimbo mpya tamu kuliko asali ambazo zimekuwa zikiwapagawisha wapenzi na washabiki wake kila inapotumbuiza.
Akizungumza na mwandishi wetu usiku wa Ijumaa iliyopita katika ukumbi wa maraha wa TRINITI uliopo Oysterbay, kiongozi wa bendi hiyo, Bob Rudala amesema kuwa, jumla ya nyimbo mpya nane ziko tayari ambazo kila siku zikipigwa washabiki hukolea na kuziomba zirudiwe.
Rudala alizitaja nyimbo hizo kama NDOTO pamoja na CISSE na FUNGUA zilizotungwa na muimbaji nyota Junior.
Zingine ni NILIE NA NANI? na MAMA YANGU zilizotungwa na Captain Deo Mwanambilimbi, IMEBAKI STORI (Shehe Mwakichui) na ULINIPENDEA NINI? utunzi wake mwenyewe (Rudala).
Akasema, kwa sasa wimbo mmoja bado unafanyiwa kazi kukamilisha albamu nzima ambayo itatoka katikati ya mwaka huu ikiwa na ubora wa kimataifa.
Akaongeza kuwa, The Kalunde Band imejipanga vema safari hii kuhakikisha inafanya yale yaliyowashinda wanamuziki na bendi nyingi ikiwa ni pamoja na maandalizi ya video zilizokwenda shule za nyimbo hizo.
Aidha, Bob Rudala alitaja ratiba ya kila wiki ya bendi hiyo kuwa, kila siku za JUMATANO wanatumbuiza katika ukumbi wa hoteli ya Peacock iliyopo maeneo ya Mnazi Mmoja, kila siku za IJUMAA hujimwaga ukumbi wa TRINITI pale Oysterbay na kila JUMAPILI wanakuwa ndani ya MAFIA LOUNGE, Masaki. Lakini, Jumamosi hii watakuwa COCO BEACH kwa shoo maalum.
Bendi hiyo ambayo ni hodari kwa muziki wa mahoteli ya kitalii na shughuli mbalimbali za kukodiwa, imezidi kujizolea sifa kutokana na umahiri wa wanamuziki wake ambao ni magwiji wa kusoma alama za muda ndani na nje ya ukumbi, wakibadilika kiufundi na uburudishaji wenye ubunifu uliobobea kiasi cha kujitofautisha na bendi zingine za aina hiyo.
0 Comments