UZINDUZI MPENZI CHOCOLATE YA JAHAZI MODERN TAARAB WAFANA DIAMOND


 USIKU wa jana  utabaki kuwa wa historia kwa kundi la Jahazi Modern Taarab ambapo ilikuwa ni katika mkesha wa sikukuu ya Krismasi ya mwaka huu kwa wapenda burudani wote jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake walipopata burudani ya aina yake katika uzinduzi uliofana.
Kama haitoshi mabingwa wa miondoko ya taarab nchini wanaopiga muziki wake katika mtindo wa nakshinakshi Jahazi Moder Taarab wakiongozwa na Mzee Yussuf ‘Mfalme’ kukonga nyoyo ipasavyo wa allbamu yao mpya ya saba, inayokwenda kwa jina la ‘Mpenzi Chocolate’ Iliyokwenda sambamba na maadhimisho ya sita ya kuanzishwa kwa kundi hilo.

Mzee Yussuf aliingia akiwa katika gari la kifahari aina ya Limousine nyeusi akiwa kavalia jojo jeusi na na kofia aina ya tarabushi kichwani alishangiliwa huku mashabiki wakienda kulizingira gari hili lililokuwa likiiingia taratibu ukumbini huku likiendeshwa na mnazi wa muziki nchini Idd Janguo.

Mzee aliyewapagawisha mashabiki kwa kuwaimbisha kiitikio cha ‘Heluahelua’akiwa ananema kwa mbwembwe huku mashabiki wakitamani hata kumvuta lakini wakati na miundombinu haikuwaruhusu ukumbini hapo.

Alishuka na moja kwa moja alikwenda jukwaani na kukata keki iliyotengenezwa kwa muundo wa jahazi huku yeye akirusha vijembe vya hapa na pale kwamba yeye katika muziki wa Taarab ni Alfa na Omega na kusema kwamba yeye ni moto wa kuotea mbali huku wengine wanaigiza kufa hwaweze bali wataishia kuzimia.

Uzinduzi huo ulipambwa na kundi maarufu la Taarab Asilia kutoka Unguja, Nadi Ikhwan Safaa pamoja na mkali wa Bongo Fleva anayeshikilia tuzo tano za ubora za Kilimanjaro, ‘20%’ ambao wote walipagawisha kwa miondoko yao pale walipokuwa jukwaani.

Albamu hiyo ya ‘Mpenzi Chocolate’ ina vibao sita ambavyo ni ‘Mpenzi Chocolate’ kilichobeba jina la albamu, ‘Sina Muda Huo’, ‘Penye Riziki Hapakosi Husda’, ‘Full Shangwe’ pamoja na ‘Zibeni Njia Sio Riziki’,”.

Waimbaji wa vibao hivyo ni Aboubakar Soud ‘Amigo’, Miriam Mwinjuma, Khadija Yussuf ‘Sauti ya Chiriku’, Leyla Rashid ‘Malkia’ pamoja na yeye mwenyewe, huku wengine katika kundi hilo wakishambulia kwa kuitikia akiwamo aliyekuwa mwandishi wa habari za michezo na burudani wa gazeti hili Mwanne Othman Sekuru.
Aidha Yussuf amewaomba mashabiki na wapenzi kujitokeza kwa wingi katika kununua kanda zao za ‘Audio’ kwani ni sehemu moja ya kutengeneza pato lao na wasanii kwa ujumla ambazo zinapatikana kwa sh.5,000 tu.

 Mzee Yussuf akiingia ukumbini  jana usiku.
 Mfalme akimlisha kipande cha keki mmoja wa waimbaji wa Jahazi.
 Mdau wa masuala ya Burudani nchini  Said Mdoe 'Screen Masters' naye aliwakilisha.
 Mzee akikata keti huku dadake Khadija Yussuf akisubiri kulishwa.

Post a Comment

0 Comments