Marehemu Abbel Olemotika 'Mr .Ebbo' enzi za uhai wake amefariki dunia alfajiri ya leo Jijini Arusha.
Na Ahmed Khatib,Tanga
ALIYEKUWA Msanii maarufu Abeli Loshilaa O’le Motika a.k.a Mr. Ebo ambaye alikuwa akipiga muziki wake katika mtindo wa ‘Rap Cartoon’ amefariki dunia jana alfajiri na anatarajiwa kuzikwa leo Jijini Tanga.
Msanii huyo ambaye alizaliwa April 26 1974 Jijini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baba mzazi wa marehemu Lossillaa Motika msanii huyo amefariki kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya ini na figo tatizo lililopelekea kushindwa kufanya kazi na kurudi nyumba jijini Arusha kwa matibabu zaidi ambapo alilazwa katika hospitali ya Usa River Mission kwa miezi mitano hadi mauti yalipomfika.
Alipata elimu yake ya msingi Jijini Arusha na kuhitimu katika shule ya msingi Changa iliyopo Jijini Tanga.Elimu yake ya sekondari aliipata katika shule iliyopo Tanga.
Mr.Ebbo alianza kujihusisha na uimbaji wa muziki wa kwaya mwaka 1990 katika kanisa la KKKT Kisosora Jijini Tanga na baadaye akawa Mwalimu wa Kwaya katika Kanisa hilo .
Marehemu atakumbukwa kwa nyimbo yake ambayo ilimtambulisha vyema katika tasnia ya muziki wa kidunia ukiwa katika miondoko ya Bongo Fleva inayokwenda kwa jina la ‘Mi mmasai’.
Wimbo huo ambao Mr. Ebbo alijigamba kwamba anadumisha mila ambayo wengine wameshindwa ambao aliuachia mwaka 2002 aliourekodi katika Studio za Mj Record.
Baada ya kuweka pembeni masuala ya kupanda katika majukwaa alijiajiri baada ya kufanikiwa kufungua studio yake mwaka 2003 iliyojulikana kwa jina la Motika Record iliyopo Kisosora Jijini Tanga.
Zifuatazo ni baadhi ya nyimbo zilizompa umaarufu mbali ya Mi mmasai ambazo ni ‘Maneno mbofu mbofu’, ‘Sitaki tena pombe’, ‘Kamongo’, ‘Boda boda’, ‘Interview’ na nyingine nyingi.
Ebbo ameacha mke na watoto watatu wote wakiwa ni wakike ,anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumatatu Mkoani Arusha
Wakiongelea kwa masikitiko makubwa baadhi ya wadau wa Muziki jijini Tanga wamesema kuwa wameondokewa na mtu muhimu katika jamii kwani nyimbo zake zilikuwa na mafunzo kwa rika zote kwani alikuwa hachagui mtoto wala mkubwa ila wanashukuru kwani mungu amempenda zaidi.
Mmoja wa wamiliki wa studio ya muziki Mkoani Tanga Anayefahamika kama Abui Gomba wa Gomba Records amesema kuondoka kwa Mr Ebbo ni pigo kwa muziki wa Bongo fleva kwani ndiye muanzilishi wa Studio ya Muziki jijini Tanga.
Mungu ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi Ameen.
0 Comments