KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi Nape Nnauye.
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi(CCM ) kimekiri kuwepo kwa mchakato wa kuwaondoa Marais wastaafu katika Kamati ya kudumu ya chama hicho (NEC) na kuwaundia Baraza lao la Wazee.
Hilo lilibainika leo wakati Katibu Mwenezi wa Chama hicho,Nape Nnauye, alipokuwa akitoa malalamiko yake dhidi ya gazeti moja la kila siku kwa kuchapisha tangazo lililohusiana na mchakato huo katika vikao vya ndani vya chama hicho ambalo lilichapishwa bila idhini ya chama.
Akionekana kujichanganya na maneno yake Nnauye alisema inastajaabisha kuona tangazo hilo limechapishwa bila kupitia mikononi kwake kama msemaji wa mwisho wa chama na kukiri kwamba kuna baadhi ya masuala yalioyoandikwa humo yana ukweli ndani yake na mengine yamelenga kupotosha umma.
Katika maelezo yake hayo alikiri kati ya mambo ambayo yalijadiliwa katika mkutano wa NEC uliomalizika mjini Dodoma hivi karibuni ni suala la kuwatumia marais wataafu na viongozi wengine waliowahi kushika nyadhifa za juu serikalini katika kukijenga chama.
Alifafanua kuwa moja ya mambo yaliyojadiliwa kwa muda mrefu ni la kuunda baraza la wazee ambapo viongozi hao watakuwa kama washauri pale zitakapohitajika busara zao.
Katibu huyo alisema mpaka sasa wamekuwa wakijiuliza tangazo hilo limefikaje katika gazeti hilo na litalipiwa nani ikiwa siyo chama imeliridhia litoke na kuonesha wasiwasi wake na gazeti hilo kama kweli limefuata maadili.
Nnauye alidai kwamba baada ya kukaa kikao na viongozi wenzake,wanaangalia utaratibu watakoweza kulichukulia hatua gazeti hilo kutokana na kutumia tangazo ambalo alidai linaeneza uchochezi na huenda limetumiwa kwa maslahi ya mtu mmoja kukichafua chama.
Akitetea hoja hiyo alisema chama kimeona siyo busara kuwaweka wazee hao katika vikao vya ambavyo wakati mwingine vinamalizika saa nane za usiku na badala yake wawe na vikao vichache na vitakavyomalizika katika muda ambao utakuwa ni mzuri kwao.
Hata hivyo alisema hakuna maamuzi yatakayotolewa ambayo hayatafuata kanuni na katiba za chama kama ilivyodaiwa na kwa yale ambayo yanahusiana na katiba bado mchakato wake ni mrefu.
Alipobanwa maswali kutoka kwa waandishi wa habari yaliyomtaka aeleze ni kwanini mambo mengi yanayojadiliwa katika vikao vyao vya ndani vya chama yamekuwa yakitolewa nje ambapo hawadhani kwamba huenda wajumbe wanaohudhuria vikao hivyo sio waaminifu.
Nnauye alisema hawezi kuwatuhumu moja kwa moja wajumbe kwa kuwa hilo hana ushahidi nalo na isitoshe makabrasha yanayochapishwa yanapitia katika mikono ya watu wengi na isitoshe wakati vikao vinaendelea huwa kunakuwa na wahudumu hivyo huenda siri zikawa zinavuja kupitia sehemu zote hizo.
Kuhusu malalamiko yake juu ya gazeti hilo kuwa mara nyingi limekuwa likitoa siri za chama ambazo hazijathibitishwa,alisema ana uhakika kwamba msimamiaji wa kampuni inayomiliki gazeti hilo ambapo hakuwa tayari kumtaja jina kutokana na nafasi aliyonayo ndani ya CCM ni rahisi kwake kupata ‘documents’ hizo.
“Jamani mkumbuke hata mtandao wa Weakles umekuwa ukiandika mambo makubwa ambayo mengine yana ukweli ndani yake na kama mwandishi anatakiwa kukilinda chanzo chake cha habari kwa hiyo mkinibana sana kuhusu wapi wanazipata habari hizi mtakuwa hamnitendei haki,”alisema Katibu huyo.
0 Comments