TIMU YA TAIFA YA TANZANIA KUKIPIGA LEO USIKU NA TIMU YA TAIFA MOROCCO

Taifa Stars imewasili salama hapa Marrakech, Morocco tayari kwa mechi dhidi ya wenyeji Morocco itakayochezwa kesho (Oktoba 9 mwaka huu) saa 1.30 usiku kwa saa za hapa. Kuna tofauti ya saa 3 kati ya hapa na Tanzania, hivyo kwa saa za nyumbani mechi itakuwa saa 4.30 usiku. Timu ilitua Casablanca saa 9.30 ikitokea Doha, Qatar ambapo ililala juzi Alhamisi kabla ya kuanza safari ya Casablanca saa 3 asubuhi.
Kutoka Casablanca hadi Marrakech ambapo ni umbali wa kilometa 230, wenyeji Morocco waliisafirisha Stars kwa basi ambao ni mwendo wa saa tatu hadi kufika hapa. Baada ya kuwasili na kuingia hotelini, timu ilifanya mazoezi jana jioni, na leo usiku (kwa muda ule ule wa mechi) itafanya mazoezi kwenye uwanja utakaotumika kwa mechi (the Great Stadium). Kocha Jan Poulsen leo amemtaja kiungo Henry Joseph kuwa kapteni kwenye mechi hiyo itakayochezwa kwenye uwanja wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 43,000.

Mitaani hapa Marrakech mashabiki wa Morocco wamekuwa wakiizungumzia mechi hiyo, na wana imani kuwa timu yao itaibuka na ushindi, hivyo kufuzu kwa ajili ya fainali za AFCON zitakazochezwa mwakani katika nchi za Equatorial Guinea na Gabon. Morali kwa upande wa wachezaji wa Stars iko juu, na hadi sasa hakuna majeruhi kwa wachezaji wote 20 waliokuja na Stars hapa kupeperusha bendera ya Tanzania.
Hapa napatikana kwa namba +212 61 8185749
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Marrakech, Morocco

Post a Comment

0 Comments