MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI

Mtihani wa uwakala wa wachezaji (players agent) wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) umefanyika leo (Septemba 29 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Watanzania wanane walijisajili kwa ajili ya kufanya mtihani huo. Watano kati ya hao ndiyo wamejitokeza na kufanya mtihani huo ambao ulikuwa na sehemu mbili. Maswali kutoka FIFA na mengine kutoka TFF. Walioomba uwakala na kufanya mtihani huo ni Adam Kapama, Aziz Sharif, Dk. Cyprian Maro, Florian Kaijage na Valence Mayenga. Mtihani mwingine wa uwakala utafanyika Machi mwakani.

 Mpaka sasa Tanzania ina mawakala saba wa wachezaji wanaotambuliwa na FIFA. Mawakala hao ni Ally Mleh wa Manyara Sports Management, Damas Ndumbaro, John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully.

                                       YANGA, COASTAL ZAINGIZA MIL 29/-
Mechi namba 51 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa Septemba 28 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 29,146,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 7,982 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 rangi ya chungwa, sh. 7,000 kwa VIP C, sh. 10,000 kwa VIP B na sh. 15,000 kwa VIP A. Eneo lililoingiza watazamaji wengi ni kwenye viti vya bluu na kijani ambapo waliingia 6,760 wakati lililoingiza watazamaji wachache ni la VIP A ambapo waliingia 27.

 Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo ambazo ni sh. 10,606,400 na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,446,000 kila klabu ilipata sh. 4,228,080. Mgawo mwingine ulikwenda kwa gharama za mchezo (sh. 1,409,360), uwanja (sh. 1,409,360), TFF (sh. 1,409,360), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 704,680), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 563,744) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 140,936).

 Boniface Wambura Ofisa Habari.

Post a Comment

0 Comments