MAPAMBANO DHIDI YA VVU ,KONDOMU YA KIKE YAZIDI KUONGEZEKA UMAARUFU

NAIROBI, Kenya
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Makazi (UNFPA) limetoa ripoti inayoonyesha kwamba katika kupambana na maambukizi ya VVU duniani, matumizi ya kondomu za kike yameongezeka na kwenda sambamba na umaarufu wake.
Katika muda wa miaka minne mfululizo, matumizi ya kondom ya kike yameongezeka na kuweka rekodi ya mauzo yanayofikia milioni 50 kwa takwimu zinazoishia mwaka 2009.

Inatoa hakikisho la kinga dhidi ya maambukizi ya VVU na mtumiaji anakuwa salama na maambukizi mengine ya magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa.

Uongozi wa UNFPA unatoa pongezi kwa kupata ushirikiano mzuri na mawakala waliosaidia kufikiwa kwa malengo yanayotarajiwa ya kuzidi kuongezeka umaarufu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2005 peke yake UNFPA iliitangaza kondomu ya kike nchi zaidi ya ishirini na nne katika mkakati wake wa kuhakikisha maambukizi ya VVU yanazidi kupungua.

“Katika nchi mbalimbali duniani, serikali na washirika wengine muhimu wanatupa ushirikiano wa kutosha katika mapambano yetu dhidi ya maambukuizi hatari ya VVU, ikiwa ni pamoja na kuacha mila zinazosababisha watu kuambukizwa gonjwa hili hatari” wanasema waandishi wa ripoti hiyo.

Elimu imekuwa ikitolewa na serikali kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali katika nchi ambazo wameelekeza mapambano yao.
“Katika mchakato, kondom ya kike inalenga kuwalinda wanawake, na mabinti wadogo katika kujilinda wenyewe na afya za wapenzi wao.”

Nchini Zimbabwe pekee, mbao za matangazo, vyombo vya habari, matangazo ya televisheni vimesaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza kondom ya kike kwa jamii na kusaidia vilevile usambazwaji wake kutoka 400,000 2005 hadi milioni mbili kwa takwimu za mwaka 2008, wakati mauzo yake yamepanda kutoka kondom 900,000 mwaka 2005 hadi zaidi ya milioni 3 kwa mwaka 2008.

Inaelezwa wasambazaji huwatumia vinyozi wa saluni za kike katika kusaidia mauzo na wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa.

“Hata vinyozi wanaoendesha saluni za kike zinazofanyakazi muda wote wamesaidia kwa kiwango kikubwa kutoa elimu na kusambaza kondom za kike, kwa hiyo wakiwa wanarembwa na wakati huo huo wanapata elimu ya kujilinda dhidi ya maambukizi ya VVU huku wakijadiliana mambo mbalimbali ya kimaisha,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Mshirika muhimu wa UNFPA, Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (PSI), limesaidia kwa kuendesha semina zinazoonyesha umuhimu wa kondom ya kike kwa wamiliki na wafanyakazi wa saluni zaidi ya 2000 na vinyozi wa kiume wapatao 70 ambao wakati huohuo wanatumika katika mauzo na usambazaji wake.

PSI inaelezwa wameajiri wafanyakazi wa kike 20 ambao ni wasambazaji wanaohudumu katika saluni za kike na kiume nchini Zimbabwe pekee.

Kwa takwimu za mwaka jana pekee rekodi iliyowekwa imefikia mauzo takribani milioni 50 kwa kondom ya kike moja moja kiwango ambacho hakikutarajiwa kwa miaka ya hivi karibuni.
                 Mfumo huu wa UNFPA na PSI umeonyesha mafanikio pia katika nchi za Guyana na Malawi.

Nchini Ethiopia, mpango ulikuwa ukitumia matamasha ya unywaji wa kahawa, mila na desturi zinazozingatia umri kuwafikia wanawake walio kwenye ndoa. Na hii ni kwa sababu kondom ya kike imekuwa ikitumiwa zaidi na wanawake wenye mahusiano na wapenzi wengi na wale wanaotegemea miili yao kama njia ya kujiingizia kipato.

Mynamar hali ni tofauti kidogo na Ethiopia. Huku inaelezwa kondom ya kike inatumiwa sana na makahaba pamoja na mashoga.
Mwaka 2002, ulifanyika utafiti nchini Marekani na kugundua matatizo kwenye matumizi ya kondom za kike tofauti na zile za kiume, kama vile kupasuka, kutohisi raha inayohitajika, na walishauri utafiti zaidi ufanyike katika kuiimarisha na kuwa bora zaidi.
Pamoja na umaarufu iliojipatia bado kondom ya kike siyo maarufu kama ilivyo ya kiume. Kwa mujibu wa UNFPA, zaidi ya kondom za kiume bilioni 10 zinatumika kila mwaka na ongezeko la matumizi yake linakua kila baada ya muda fulani.
Nchini Kenya, matumizi ya kondom ya kike yamekuwa ni kinga kubwa kwa maambukizi ya VVU lakini inaelezwa kwamba bado wanawake wengi hawavutiwi na matumizi yake. Takwimu zinaonyesha zaidi ya kondom milioni tatu za kike zilisambazwa nchini Kenya. “Hakuna takwimu sahihi za kukubalika kwake lakini tunaelewa kwamba matumizi kwa makahaba na mashoga mahitaji yake ni makubwa,”anasema Peter Cherutich, mkuu wa Idara ya Mpango wa Kuzuia Maambukizi ya VVU na Magonjwa yatokanayo na Kujamiiana.

“Kwa ujumla, mahitaji ni madogo na hii inasababishwa na upatikanaji wake na ukosefu wa elimu dhidi ya matumizi na maambukizi ya VVU nchini Kenya.

“Bado ni gharama kubwa kuzitangaza na kusambaza kondom za kike tofauti na kondom za kiume,”anaongeza. “Ingawa kuna tofauti ya matumizi kati ya kondom za kike kwa makahaba na uwezo wao, wanawake wengine wasiofanyabiashara ya ngono, hawazijui na hawazitumii kabisa.”

Kwa mujibu wa UNFPA, kondom ya kike inagharimu takribani dola moja ya kimarekani wakati kondomu ya kiume inasambazwa bure madukani. Katika maduka ya dawa baridi jijini Nairobi, inauzwa dola 0.20 na zaidi kidogo ya dola moja.

“Kwa takwimu za mwaka 2009 takwimu zinaonyesha pakiti moja ya kondom ya kike yenye kondom tatu ilikuwa ikigombewa na wanawake zaidi ya 36 ulimwenguni kote,” hii ni kwa mujibu wa ripoti ya UNFPA.

Katika malalamiko kutoka kwa wanawake ambao hawaikubali kondomu ya kike ni makelele wakati wa kujamiiana. Ikiwa imetolewa kondom aina nyingine ya kike ambayo haina makelele na iliyotumia gharama kidogo katika uzalishaji wake, bado utafiti unaonyesha ni ghali kuliko kondom ya kiume.

“Tunajaribu kuitangaza kwa wafanyabiashara ya ngono na makahaba, na wanasema baadhi ya makahaba kama una wateja kuanzia watano hadi kumi kondom ya kiume ni bora zaidi ya kike, inachukua muda mrefu kuivaa na wateja wengi hawaipendi,” anasema Macklean Kyomya, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali nchini Uganda.
Lillian Mwamba, anayeishi jijini Nairobi nchini Kenya, anasema angeweza kuitumia kondom ya kike kama ingekuwa inapatikana kwa urahisi.
“Nimeitumia kondom ya kike mara kadhaa lakini kondom ya kiume ndiyo ninayoitumia mara kwa mara na inapatikana kwa urahisi kwenye maduka ya dawa baridi, vioski, kondom za kike ni haba na ghali,” aliliambia shirika la habari la Irin / Plus.
“Siwezi kusema ni mbaya, ninatumia ninapoipata na inanipa kinga ya kutosha”, anaongeza.
Katika viunga vingi jijini Nairobi, mazungumzo yaliyotawala ni kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya kondom ya kike na uhaba wake kwa ujumla.
Makala imeandaliwa na Haji Kalili kwa msaada wa Mashirika ya Habari ya Kimataifa.
Maoni/Ushauri 0714 321 444
kalilihaji@gmail.com

Post a Comment

0 Comments