Mkazi mmoja wa Kijiji cha Nkundusi katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Yohana Adam Sabuni (28), anashikiliwa na Polisi mkoani humo kwa tuhuma za mauaji ya mkewe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi ACP Frasser Kashai, amesema kuwa usiku wa kuamkia leo majira ya saa 7.00 huko katika kijiji Nkundusi wilayani Kasulu, mtuhumiwa Yohana alimshambulia mkewe Bi. Roziana Fidelis Pahida(26), kwa kutumia mpini wa jembe na mianzi hadi kumuua.
Kamanda Kashai amesema kuwa mara baada ya mtuhumiwa huyo kubaini kuwa mkewe ameshafariki, alianza kukimbia kwa lengo la kukwepa kesi na ndipo Polisi walipopata taarifa kutoka kwa raia wema ambapo walimfuatilia na kumtia nguvuni.
Amesema kuwa kutokana na kipigo hicho, marehemu alipasuka bandama na kusababisha kutokwa na damu nyingi zilizopelekea kifo chake.
Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa Kigoma amesema uchunguzi wa awali wa tukio hilo unaonyesha kuwa chanzo cha mauaji hayo kinatokana na hisia za wivu wa kimapenzi ambapo marehemu aliondoka nyumbani kwake na kuomba hifadhi nyumba jirani baada ya kuona kuwa mumewe kachelewa kurudi naye kuhofia kulala peke yake.
Kamanda Kashai, amesema baada ya mtuhumiwa kurejea nyumbani usiku huo na kubaini mkewe hayumo ndani, ambapo baada ya muda, marehemu alisikia sauti ya mumewe akiimba akirudi kutoka ulevini na ndipo alipotoka kwa jirani na kurudi kwake kitendo ambacho kilimkasirisha mtuhumiwa na kuona kuwa labda alikuwa akifanuya mapenzi na jirani yake.
Amesema hatua hiyo ilimfanya mtuhumiwa huyo kumshambulia mkewe jambo ambalo sio tu kuwa lilikuwa ni la kikatili, bali pia ni kitendo kinyume na haki za binadamu na udharimu wa unyanyasaji wa kikatili dhidi ya wanawake na watoto mambo ambayo pia yanapingwa vita na Umoja wa Mataifa.
Amesema kuwa, mume au mke apatwapo na matatizo na mwenziwake anatakiwa kwenda Kituo cha Polisi ambapo kuna Madawati maalumu ya kushughulikia matatizo ya wanawake na watoto na kupatiwa ufumbuzi au ushauri wa matatizo yao.
Kamanda Kashai amesema kuwa tayari Polisi wameanza upelelezi ikiwa ni pamoja na kumhoji Mtuhumiwa na baadaye atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kuchukua sheria mkononi kwani kwa kufanya hivyo ni kujitafutia matatizo ambayo yatamfanya akamatwe na Polisi na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili na hata kufungwa Maisha.
0 Comments