Kiingilio cha juu kwa ajili ya mchezo wa hisani utakaokutanisha wachezaji waliowahi kuchezea klabu za Simba na Yanga unaotarajia kurindima Machi 19 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ni sh 10,000 huku cha chini kikiwa 1,000.
Akitangaza viingilio hivyo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Tanzania Sports Catalyst (TASCA), Suleiman Mathew, alisema watakaokaa 'VIP A' watalipa sh 10,000 huku sh 1,000 itakuwa kwa jukwaa la kijani.
Mathew alitaja viingilio vingine kwa upande wa 'VIP B' kuwa itakuwa sh 5,000, 'VIP C' 3,000 huku viti vya bluu sh 2,000 na kutoa wito kwa wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi kujionea ladha ya soka ya miaka iliyopita, ikiwa ni sambamba na kuwasaidia waathirika wa mabomu ya Gongo la Mboto.
Aliwataja waamuzi wa mchezo huo kuwa ni pamoja na Nassor Hamduni, Leslie Liunda, Ally Mkomwa na Mchungaji Ammy Sentimea huku kamisaa ni Wilbrod Alphonce.
0 Comments