TBL NA RADIO ONE WAUNGANA KUMSAKA SHUJAA WA KWELI

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager na ushirikiano wa kituo cha televisheni cha ITV leo wamezindua rasmi kampeni ya aina yake ya kuwatafuta mashujaa wa ukweli katika jamii ambao watapata tuzo za heshima kutokana na mambo waliyofanya katika jamii inayowazunguka na kuleta mabadiliko.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa bia ya Safari Lager, Fimbo Butallah alisema; Shujaa huyu wa Ukweli, atajulikana kama “Shujaa wa Safari Lager” na ni lazima awe Mtanzania aliye na umri wa miaka 18 na kuendelea, anatakiwa awe amefanya kitu au jambo kubwa katika jamii inayomzunguka ambalo limeleta mchango mkubwa au mabadiliko katika jamii hiyo, mtu huyu anatakiwa awe amefanya mambo au jambo hilo bila kusukumwa na uwezo wa pesa au madaraka aliyo nayo bali msukumo toka ndani ya moyo wake.

Utaratibu wa kumpata “Shujaa wa Safari Lager 2010” utakuwa kama ifuatavyo;
Baada ya uzinduzi huu wa leo, kutakuwa na matangazo katika vyombo mbali mbali vya habari kuelezea jamii utaratibu mzima utakavyokuwa, na wananchi watatakiwa kupendekeza majina ya watu wanaoamini kuwa ni mashujaa katika jamii inayowazunguka, mapendekezo haya yatafanywa kupitia fomu maalum zitakazochapishwa katika magazeti ya NIPASHE na pia fomu hizo zitapatikana katika ofisi za mawakala wote wa TBL nchi nzima. Baada ya kujaza fomu hizo, wananchi watatakiwa kuzitumbukiza katika masanduku maalum yaliyo kwa mawakala wa TBL karibu na maeneo yao.

Fomu zote zilizokamilika zitakusanywa na majaji watazichuja na kupata fomu tatu zilizobeba mambo makubwa na yaliyogusa zaidi jamii ambapo watu hao watatu watatangazwa katika vyombo vya habari na kisha jamii itatakiwa kuwapigia kura kufuatia mambo au jambo walilofanya na jinsi lilivyogusa jamii, Jina litakalopata kura nyingi zaidi ndilo litakalokuwa mshindi na hivyo kupata tuzo ya “Shujaa wa Safari Lager 2010”.

Pamoja na tuzo hiyo, mshindi pia atapata zawadi ya pesa taslim shilingi milioni kumi, ambapo asilimia 30 ya pesa hiyo itaelekezwa katika jamii anayotoka mshindi huyo ili kusaidia mradi wowote wa jamii atakaochagua “Shujaa wa Safari Lager”, hivyo yeye kubakiwa na asilimia 70. Washiriki wawili waliobaki watapata shilingi Milioni moja kila mmoja kama kifuta jasho.Kampeni hii kwa mwaka huu inaanza leo tarehe 24 na itafikia kilele tarehe 14 Januari 2011 siku ambayo Shujaa wa Safari Lager 2010 atatawazwa rasmi.

Akizungumzia ushirikiano wa kituo cha ITV katika kampeni hii, Meneja Mawasiliano na Habari wa TBL, Editha Mushi alikipongeza sana kituo cha ITV kwa kukubali kushirikiana na Safari Lager kuendesha kampeni hii muhimu kwa watanzania, pia aliahidi ushirikiano wa kutosha baina ya TBL na vyombo vya habari katika harakati za kuinua jamii ya Watanzania.

Post a Comment

0 Comments