ROSEMARY TUNDA LA FACES INTERNATIONAL,SASA MBUNIFU WA MITINDO

Mbunifu wa Mavazi wa Kimataifa,Rosemary Kokuhilwa akiwa katika pozi la picha huko nchini Marekani.

Mbunifu wa Kimataifa wa Kitanzania, Rosemary Kokuhilwa Rwechungura ameandaa onyesho maalum nchini Marekani ambalo litafanyika Ijumaa hii kwa ajili ya kuchangia mradi wa watu wasiosoma wa Bisila Bokoko.

Rose mwanamitindo ambaye alitokea kampuni ya Faces International iliyokuwa chini ya marehemu Amina Mongi na Ruge Mutahaba kati mwaka 1998 na 1999 iliyokuwa na ofisi zake katika jengo la kitega uchumi kwa sasa anaishi Marekani pia anamiliki Kampuni yake iitwayo FASHIONJUNKII ambapo pia anaendesha Blog inayohusisha mambo ya mitindo na urembo.

Akizungumza kutoka Marekani, Kokuhilwa alisema hili ni onyesho la kwanza kuandaliwa na FashionJunkii likihusisha wabunifu na wanamitindo mbalimbali kutoka pande mbalimbali duniani.

“Kutakuwa na wabunifu nane ambao ni maarufu duniani, wataonyesha nguo ambapo pia kutakuwa na zaidi ya wanamitindo 36 kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya onyesho hilo litakalofanyika Chuo cha Teknolojia ya Mitindo (FIT),” alisema.

Aliwataja wabunifu watakaoonyesha mavazi yao ni pamoja na
MATAANO, Amparo Chorda, Louda Collection, African Mosaique, Thula Sindi, David Tlale, Nike Kondakis na Prajjé Couture.

Alisema onyesho hilo mbali na kuwapa waalikwa nafasi ya kuona utamaduni wa sehemu mbalimbali kutoka sehemu tofauti duniani, onyesho hilo pia litasaidia kuwakutanisha watu mbalimbali maarufu ambao wako kwenye fani ya mitindo kwa muda mrefu.

“Onyesho hili litasaidia pia waalikwa kuona mavazi ambayo mengi hayajawahi kuonekana.”

Kokuhilwa alisema onyesho hili ni la kwanza kwa ajili ya kusaidia jamii na kwamba wanatarajia kulifanya kila mwaka kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments