Naliona Anguko la TOT

Na Irene Mark
HIVI sasa vyama mbalimbali vya siasa vinaendelea na mchakato wa kunadi sera na ilani za vyama vyao kwa ajili ya kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa kwa ngazi ya udiwani, ubunge na urais.Harakati hizo zinahusisha mikutano ya hadhara ambapo wananchi wanahimizwa kushiriki kwenye mikutano hiyo ili kusikiliza kisha kufanya uamuzi sahihi wakati wa kupiga kura Oktoba 31 mwaka huu.Ni jambo la kawaida kuona vyama hivyo vikiwatumia wanamuziki katika kuamsha hisia na kuongeza hamasa kwa wanaokwenda kuwasikiliza, hivyo wakati huu ajira kwa wasanii hususan wa burudani zinaongezeka.Miongoni mwa kikundi cha sanaa chenye uhakika wa kupata ajira wakati wa kampeni kama hizi ni kundi la Tanzania One Theatre (TOT), chini ya uongozi wa Kapteni mstaafu John Komba. Kundi hili ni mali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambalo limewezesha ajira za kudumu na zile za muda kwa vijana wengi nchini katika maeneo tofauti wanamopita. Tangu kuanzishwa kwa TOT hadi sasa, limefanikiwa kukonga nyoyo za wengi na kujizolea umaarufu katika medani ya burudani hapa nchini ikizingatiwa na ukongwe wake. Mtakubaliana nami hasa kwa nyimbo zake wakati taifa lilipompoteza kiongozi na mmoja wa waasisi, Hayati Mwalimu Julius Nyerere. Hivi sasa bendi hiyo ni kama haipo. Imezeeka na kupoteza uwezo wake katika sanaa. Imeshindwa kwenda na wakati hasa katika kipindi hiki ambapo ubunifu zaidi unatakiwa kutokana na kuibuka kwa vipaji vya wasanii wa miondoko ya bongo fleva wanaofanya vizuri zaidi.Nasema hivyo kwa sababu, TOT inaendelea kunakili nyimbo zao za zamani ambazo kwa kiwango kikubwa zimetuchosha wasikilizaji, wapenzi na hata makada wa chama hicho akiwemo Rais Dk. Jakaya Kikwete.Nimelazimika kuandika haya baada ya kuzunguka kwenye mikoa mitano na majimbo yasiyopungua 25 ya Tanzania Bara wakati wa mzunguko wa kwanza wa kampeni za urais nikiwa na mgombea wa CCM Dk. Kikwete.Kote nilikopita wakati wa kampeni hizo, wananchi walivutiwa zaidi na nyimbo za wasanii wa kizazi kipya zilizotungwa maalumu kwa ajili ya kampeni za mwaka huu. Wasanii hao ni Marlow, Diamond na wengineo ambao kwa pamoja wametunga nyimbo zilizowekwa kwenye CD moja na kupewa jina la Vijana zaidi 2010 bongo fleva zaidi.Katika mkusanyiko wa nyimbo hizo hakuna itakayopigwa ukaacha kutikisika. Mvuto, ujumbe na midundo ya nyimbo hizo vilitosha kushinda staha za wanaosikiliza.Burudani ya nyimbo za wasanii hao inaongezeka pale Dk. Kikwete, anapoamua kuonyesha dhahiri mapenzi yake kwenye muziki wa kizazi kipya. Anashindwa kuvumilia kila unapopigwa wimbo wa piii piiii ulioimbwa na Marlow.Lakini, hali inaonekana kutokuwa na msisimko na kushindwa kupandisha mzuka pale nyimbo (kwaya) za TOT zinapopigwa. Hii ni changamoto kwa viongozi wa kundi hilo, akiwemo Kapteni Komba ambaye kipindi hiki amegubikwa na sintofahamu hasa pale wananchi wanapofurahia zaidi nyimbo za kina Marlow kuliko za bendi hiyo kiasi cha kudaiwa kuwafanyia hila jukwaani kwa kuvuruga mitambo ili kuharibu usikivu.Kwa mtazamo wangu, Komba amezidiwa kwa kukosa ubunifu, anashindwa kusoma alama za nyakati. Namshauri afanye uamuzi sahihi wa ama kuendelea na muziki au ubunge wake vinginevyo atakosa mwana na maji ya moto.Sababu ya kusema hivyo ni baada ya kuyumba kiutendaji kwenye kuimarisha bendi tangu mwaka 2005 na kuwahudumia wananchi wa Mbinga Magharibi.Binafsi naliona anguko la TOT endapo wataendelea kudorora mwisho wao unakaribia punde na huenda hizi zikawa kampeni zao za mwisho. Shime Kapteni umezidiwa gawa majukumu usaidiwe kuimarisha kikundi chako ili makali ya zamani tuyaone tena.

Post a Comment

0 Comments