Social Icons

Saturday, September 7, 2013

RAIS KIKWETE AZINDUA SHULE YA MSINGI NTULYA


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete,Mwanzilishi na Mkurugenzi waShirika la Africa School House Bi.Ainee Bessire (watatu kushoto) pamoja naMbunge wa Misungwi Charles Kitwangwa(kushoto) na mkuu wa mkoa wa Mwanza Injinia Evarist Ndikilo(kulia) wakikata utepe kuzindua rasmi shule ya msingi Ntulya katika kata ya Mondo wilayani Misungwi.Shule hiyo imejengwa kwa msaada wa Shirika lisilo la kiserikali la Africa School House lenye makao yake nchini Marekani.Rais Kikwete yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza ambapo atakagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi Ntulya muda mfupi baada ya kuizindua katika kata ya Mondo wilayani Misungwi leo. Shule hiyo imejengwa kwa msaada wa Shirika lisilo la kiserikali la Africa School House lenye makao yake nchini Marekani.Rais Kikwete yupo katika ziara ya kikazi mkoani Mwanza ambapo atakagua na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo. Picha na Freddy Maro
************************************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Ijumaa, Septemba 6, 2013, amefungua shule ya kisasa ya msingi ya Ntulya katika kata ya Mondo, Wilaya ya Misungwi, iliyotolewa kama zawadi kwa wanakijiji cha Ntulya na taasisi moja ya Marekani.


Aidha, Rais Kikwete amezindua huduma za x-ray kwenye Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mjini Misungwi ikiwa ni hatua zake za mwanzo kwenye siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya Rais Kikwete katika mkoa wa Mwanza ambako atakaa siku tano akikagua na kuzindua miradi na shughuli za maendeleo.
Shule ya Ntulya iliyoko kilomita 47 kutoka mjini Misungwi ina wanafunzi 466 na walimu 11 na ni zawadi ya Taasisi ya Africa School House ya Marekani kwa wanakijiji cha Ntulya ambako Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt. Aimee Bessire ambaye amehudhuria sherehe za uzinduzi wa shule hiyo na mume wake, Mark Bessire walipata kuishi wakifanya utafiti kuhusu utamaduni wa Kabila la Wasukuma.

Shule hiyo ya kisasa imejengwa kwa matofali ya kuchomwa na ilijengwa kati ya 2008 na 2010. Ina madarasa 11, nyumba 10 za walimu na kisima cha maji safi. Kwa jumla shule hiyo ina uwezo wa kuwa na wanafunzi 600 kwa wakati mmoja.

Akizungumza kwenye sherehe za leo, Dkt. Bessire ambaye amezungumza kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kiswahili na Kisukuma, amesema kuwa shule hiyo imejengwa kwa jumla ya sh bilioni 1.038, na kati ya hizo sh milioni 980 zilitolewa na Africa School House, Halmashauri ya Misungwi ilichangia sh milioni 28 na nguvu za wananchi zilichangia sh milioni 30.

Taasisi hiyo ya Marekani pia imewajengea wanakijiji hao wa Ntulya Kituo cha Afya kwenye eneo hilo la shule na Dkt. Bessire amesema kuwa Taasisi hiyo ina mipango ya kujenga shule ya mfano ya sekondari ya bweni ya wasichana.
Dkt. Bessire pia amesema kuwa yataanzishwa madarasa kwenye shule hiyo kwa ajili ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.

No comments:

 
 
Blogger Templates