Social Icons

Featured Posts

Sunday, March 26, 2017

ZIWA JIPE HATARINI KUTOWEKA

Na Lulu Mussa Mwanga - Kilimanjaro Imebainika kuwa Ziwa Jipe liko hatarini kutoweka endapo hatua za haraka hazitachukuliwa katika kulinusuru.

Hayo yamesemwa leo na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa Mazingira Mh. January Makamba alipofanya ziara ya kukagua ziwa hilo ambalo sehemu kubwa imezungukwa na magugu maji.

Waziri Makamba amesema kuwa ziwa hilo ni rasilimali muhimu na hivyo ni lazima kuwe na mpango wa muda mfupi na ule wa muda mrefu. Kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamiza wa Mazingira (NEMC) ameazimia kutangaza kupita Tangazo la Serikali kuwa eneo hilo ni eneo nyeti kimazingira."

Tutatanga eneo hili kuwa eneo nyeti kimazingira na tutaweka masharti ya matumizi katika eneo hili" Alisisitiza Makamba Azimio hilo la kutangaza kuwa eneo mahsusi ama nyeti kimazingira itasaidi katika kuandika maandiko mbalimbali ya miradi na kupata fedha kutoka kwa wadau na washirika wa maendeleo.

Pia litawekwa chini ya uangalizi maalumu na kuweka masharti ya matumizi bora ya eneo hilo.

" Tutaweka masharti makali na magumu zaidi ili watakao kiuka wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria" aliongezea Waziri Makamba.

Aidha, Waziri Makamba amesisitiza kuwa ni vema kunusuru ziwa hilo sasa maana ndani ya miongo 2-3 huenda ziwa hilo likatoweka. "Bila hifadhi ya mazingira hakuna maisha, na ukiyaharibu mazingira hakuna msamaha yatakuadhibu tu" .

Akiongea katika Mkutano wa hadhara kijijini Butu, Waziri Makamba amesema kuwa shughuli zozote za maendeleo iwe uvuvi, kilimo, utalii, mifugo kwa namna moja ama nyingine zinategema hifadhi endelevu ya mazingira.

Katika hatua za muda mrefu Waziri Makamba amewataka wasimamizi wa Bonde la Pangani, Wizaya ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukutana mara moja kuandaa mpango na mtazamo wa pamoja wa kunusuru Ziwa Jipe.

Akiwa njiani kuelekea Nyumba ya Mungu Waziri Makamba alipitia katika Kiwanda cha Kifaru Quarries Co. Ltd na kukuta kikiendelea na uzalishaji wa kokoto bila kuwa na cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeutaka uongozi wa Kiwanda hicho kusitisha uzalishaji mara moja na kutakiwa kulipa faini kwa kukiuka Sheria ya Mazingira kifungu namba 81 na 196.

Waziri Makamba pia amefanya ziara katika Bwawa la Nyumba ya Mungu na kufanya mkutano wa hadhara na wakazi wa kijiji cha Kakongo ambao kwa pamoja wamelalamikia zuio la kufanya shughuli za uvuvi katika bwawa hilo kutokana na kupungua kwa kina cha maji na samaki katika bwawa hilo.

Bw. Charles John Waziri Mkazi wa Kijiji cha Kagongo amesema kuwa kuna hujuma katika matumizi ya rasilimali maji ambapo imebainika kuwa wakulima wanaotumia kilimo cha umwagiliaji wamekua wakitumia maji kwa kiasi kikubwa na kusababisha upungufu katika bwawa. Akijibu kero na malalamiko ya wananchi hao Waziri Makamba ameagizia kufanyika kwa doria na kuainisha pampu zote zinazovuta maji kutoka bwawani hapo "Naaagiza Mamlaka ya Wilaya ya Mwanga, Serikali ya Mtaa na Mamlaka ya Bonde Pangani kufanya doria na kuhakiki pampu zote kujua uhalali wake kama zimesajiliwa na kama zinavibali, zitakazobainika kutokuwa na vibali zote zitaifishwe" Alisisitiza Waziri Makamba.

Waziri Makamba yuko katika ziara maalumu ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira, changamoto na kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu wa kukabiliana nazo. Mpaka sasa Waziri Makamba ameshatembelea Mkoa wa Pwani, Tanga na Kilimanjaro.

WATAMBUE WANAWAKE 10 MASHUHURI NCHINI TANZANIANa Jumia Travel Tanzania

Kila ifikapo Machi 8 dunia huadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake ambapo nchi na taasisi mbalimbali huwa na shughuli kadha wa kadha katika kusherehekea siku hii. Kwa kawaida shirika la Umoja wa Kimataifa Duniani, UN, huwa na kauli mbiu kwa kila mwaka katika kuadhimisha siku hii, kwa mfano mwaka huu inasema, “Wanawake Katika Ulimwengu wa Mabadiliko ya Kazi: Kufikia usawa wa 50 - 50 ifikapo 2030.”   


Mama Samia Suluhu

Unapozungumzia miongoni mwa wanawake wachache waliofanikiwa kupata nyadhifa za juu kabisa za uongozi nchini Tanzania basi huwezi kuacha kumtaja Mama Samia Suluhu Hassan. Huyu ni Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kutokea nchini ambapo aliupata wadhifa huo kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 uliomuweka Rais John Pombe Magufuli madarakani. Tanzania kama nchi zingine za kiafrika kwa kiasi fulani imekuwa na kasumba ya kutomwamini mwanamke katika kushika nyadhifa za juu za kiuongozi. Lakini kuchaguliwa kwa Mh. Samia Suluhu kumedhihirisha kuwa hakuna lisiloshindikana endapo wanawake wakiwezeshwa, kuaminiwa na kupewa fursa.

Maria Sarungi Tsehai

Miongoni mwa wanawake wanaofanya shughuli nyingi katika harakati za kuiona jamii ya watanzania ikisonga mbele ni Maria Sarungi Tsehai. Kumchambua Maria kwa kila shughuli anayoifanya ni vigumu kwani itachukua muda mrefu ingawa kitaaluma yeye ni mtaalamu wa masuala ya mawasiliano. Kati ya shughuli kadha wa kadha anazozifanya, jina la Maria Sarungi Tsehai lilikuja kujulikana na watanzania wengi baada ya kuteuliwa kuwakilisha kwenye Bunge la kujadili mchakato wa katiba mpya na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2014. Maria alichaguliwa kufuatia hamasa yake ya kuibua mijadala ya kimaendeleo nchini Tanzania kupitia mitandao ya kijamii kama vile ‘Facebook na Twitter’ kupitia #ChangeTanzania, na kufanikiwa kuungwa mkono na wafuasi zaidi ya 50,000. 

Dr. Helen Kijo Bisimba

Kwa muda mrefu Dr. Bisimba yupo kwenye tasnia ya sheria ambapo amekuwa kipaumbele katika kutetea maslahi na kutoa msaada kwa watanzania wanyonge wanaonewa na kunyimwa haki zao katika masuala mbalimbali. Ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) nafasi ambayo yupo kwa zaidi ya miongo miwili. Mama huyu msomi aliyebobea katika masuala ya sheria amekuwa na mchango mkubwa juu ya harakati za kutetea haki na usawa katika nyanja mbalimbali. Kupitia shughuli za kituo hicho, Dr. Helen Bisimba amekuwa ni alama na nguzo muhimu ya mapambano dhidi ya unyonge na ukandamizwaji wa haki dhidi ya wananchi wa kipato cha chini.    

Faraja Nyalandu

Watanzania wengi walilifahamu jina la Faraja Nyalandu baada ya kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Miss Tanzania mwaka 2004. Lakini kipindi hicho alikuwa akijulikana kama Faraja Kota kabla ya kuolewa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Singida Kaskazini kwa sasa, Mh. Lazaro Nyalandu. Faraja ni mwanamke mjasiriamali katika masuala ya kijamii ambaye amejikita zaidi katika shughuli za kielimu ili kuwajengea uwezo watoto na vijana kuipata huduma hiyo. Kupitia dhamira hiyo ameweza kuzindua programu mbili za kuwawezesha wanafunzi kupata masomo kwa njia ya maswali na majibu pamoja na maelezo ya kutosha. Huduma hizi mbili ambazo ni ‘Makini SMS na Shule Direct,’ huwawezesha wanafunzi na walimu kuweza kusoma na kufundisha kupitia njia za simu na mtandao na hivyo kuepuka changamoto kama vile za uhaba wa walimu, vitabu na muda wa kujisomea.

Jokate Mwegelo

Jokate Mwegelo si jina geni miongoni mwa watanzania wengi na hii ilitokana na ushiriki wake katika mashindano ya urembo ya Miss Tanzania mwaka 2006 na kuibuka nafasi ya pili. Mbali na shughuli za urembo pia anajihusisha na muziki, ujasiriamali, uanamitindo na mavazi, uigizaji wa filamu, utangazaji wa luninga, ushereheshaji, na shughuli za kielimu. Jina lake ni kubwa na hamasa kwa mabinti wanaokua kutokana na mafanikio aliyonayo. Mpaka hivi sasa amefanikiwa kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya masuala ya urembo na mavazi inayojulikana kama ‘Kidoti.’ Mbali na hapo anaendesha shughuli za kusaidia jamii yake kwenye nyanja ya elimu kupitia kampeni inayokwenda kwa jina la ‘Be Kidotified.’ Mpaka sasa amekwishajenga viwanja vya netiboli na kikapu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani.  


Doris Mollel

Jina la Dorris Mollel limeanza kusikika na kujulikana baada ya kushinda taji la mashindano ya Miss Singida mnamo mwaka 2014. Baada ya hapo alianzisha harakati za kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati au miezi 9 yaani njiti ambapo alianzisha taasisi yake aliyoipa jina la Doris Mollel Foundation mwezi Februari mwaka 2015. Lengo kuu la kuanzisha taasisi hiyo ni kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaozaliwa njiti. Pia ameazimia kuielemisha jamii kwani tafiti zinaonyesha kwamba idadi ya watoto hao ni ndogo kutokana na wazazi wengi kutokuwa na tamaduni ya kwenda kujifungulia hospitali. 

Mercy Kitomari 

Huyu ni Afisa Mtendaji Mkuu na Muasisi wa kampuni inayojihusisha na utengenezaji wa ‘Ice Cream’ inayokwenda kwa jina la Nelwa’s Gelato. Mercy alishawishika kwa kiasi kikubwa kuanzisha biashara hii baada ya kuwa masomoni London nchini Uingereza ambapo alikuwa akivutiwa na vibanda vinavyouza ‘ice cream.’ Alikuwa anajiuliza endapo kama akirudi nchini atafanya kitu kama hiko kwani havikuwepo. Ametimiza ndoto hiyo na kwenda mbele zaidi kwa kuwawezesha watanzania wengine na kuwapataia mafunzo ya namna ya kuendesha biashara hiyo. Katika biashara hiyo Mercy hutumia viungo vya hapa nyumbani kutengenezea ‘ice cream’ zake kama vile matunda na karanga, hivyo kutoa ajira pia kwa wakulima. 

Joyce Kiria

Ongezeko la vituo vya luninga nchini Tanzania limekuja na fursa ya kuibuka kwa wazalishaji wa vipindi lukuki vinavyohusu masuala tofauti ya kijamii. Joyce Kiria ni miongoni mwa watangazaji wachache wanaovuma kwa kuwa na kipindi cha luninga kinachoivutia hadhira kubwa nchini. Kipindi chake cha ‘Wanawake Live’ kinachorushwa kwenye kituo cha luninga cha East African Television (EATV) kimejipatia umaarufu mkubwa hususani kwa kujikita zaidi katika kujadili na kuibua masuala mbalimbali yanayowakabili wanawake na kuwasaidia. Kipindi chake kimekuwa ni chanzo kizuri na msaada mkubwa kwa wanawake wanaokumbwa na changamoto mbalimbali na hatimaye kupatiwa msaada na serikali, taasisi au viongozi kuchukua hatua.

Wakonta Kapunda

Inawezekana kuwa habari ya huyu binti ndiyo iliyowagusa watanzania wengi zaidi nchini Tanzania kwa mwaka 2016. Maisha ya Wakonta Kapunda yalibadilika baada ya kupata ya kugongwa na gari na mwanafunzi mwenzao siku ya mahafali ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Korogwe, Tanga mwaka 2012. Ajali hiyo ilipelekea kupooza mwili mzima na kumlazimu kufanya shughuli zake kwa kutumia kichwa tu. 

Kilichowagusa wengi ni ari ya kutokata tamaa kwake ambapo aliweza kushiriki shindano la kuandika mswada wa filamu (script) lililodhaminiwa na kampuni ya Filamu ya Maisha ya nchini Uganda. Kwa kutumia ulimi wake aliweza kuandika na kufanikiwa kuchaguliwa kuingia hatua ya kwanza. Alijitokeza hadharani kuomba msaada baada ya kutakiwa kwenda visiwani Zanzibar kushiriki mafunzo ya siku 10 ambayo yalikuwa yanagharimu takribani kiasi cha shilingi milioni 4 za kitanzania. Wakonta alikuwa anaishi na familia yake mkoaniRukwa na haikuwa na uwezo wa kumsafirisha mpaka Zanzibar kwenda kujumuika na wenzake. Kupitia ushujaa wake, kutoka tamaa na kuamini kwamba ulemavu sio mwisho wa maisha, habari za Wakonta ziliwagusa watanzania na taasisi nyingi ambapo kampeni mbalimbali zilianzishwa kumsaidia kutimiza azma yake.   

Lady Jay Dee

Malkia wa muziki wa bongo flava nchini Tanzania tangu mwanzoni mwa mwaka 2000, Lady Jay Dee, inawezekana ndiye akawa msanii pekee wa kike aliyefanya vizuri katika tasnia hii kwa miaka yote ambayo amekuwa akifanya kazi hiyo. Mbali na kuyumba kidogo kwenye muziki na maisha yake binafsi miaka michache iliyopita, Lady Jay Dee au Jide aliwadhihirishia mashabiki wake kwamba bado anao uwezo mkubwa wa kufanya muziki. Alirudi kwa kuachia nyimbo ya ‘Ndi Ndi Ndi’ iliyomrudisha kwa kishindo kwenye chati mbalimbali za muziki nchini na kumfanya afanye matamasha na kuzungumziwa kila pembe ya nchi. 

Kwa hakika Lady Jay Dee ni mwanamke ambaye aliyashinda magumu yaliyomkumba ndani ya kipindi cha muda mchache na kufanikiwa kusimama tena. Kwa mashabiki wa muziki wa Tanzania itabakia kuwa hakuna kama yeye utakapozungumzia wasanii wa kike kwenye muziki waliofanikiwa zaidi na kuwashawishi wengi kuingia kwenye shughuli hiyo. 

Wapo wanawake wengi ambao wanastahili pongezi kwa shughuli wanazozifanya katika kuwainua wanawake wenzao na jamii kwa ujumla ambao Jumia Travel isingeweza kuwaorodhesha hapa. Lakini kwa hao waliotajwa hapo juu ni wazi kabisa mwanamke anaweza kufanya mambo makubwa sawa na zaidi ya mwanaume. 

Na ni matumaini yetu kwamba itafikia kipindi ambacho hakutakuwa na dhana ya kujadili jinsia tena ya mtu katika ufanisi wa jambo fulani kama inavyohubiri kauli mbio ya Shirika la Umoja wa Kimataifa mwaka huu.

LAPF WATOA MAKOTI 500 KWA BODABODA WA KISARAWE

 Muonekano wa jengo la mikutano la Halmashauri ya 
Wilaya ya Kisarawe.

WATIMISHI WA UMMA CHANGAMKIENI NYUMBA ZA SERIKALI

 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),Mhandisi Elius Mwakalinga (wa tatu kulia), akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC), kabla ya kutembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za Bunju B jijini Dar es Salaam jana zinazojengwa na wakala huo. Wa pili kulia ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Josephat Asunga.

KITABU CHA UWIANO WA TAKWIMU ZA WANAWAKE NA WANAUME CHAZINDULIWA

 Meneja wa Takwimu za Watu na Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Sylvia Meku (katikati) akiwa na wadau wakionesha kitabu cha uwiano wa takwimu za  wanawake na wanaume wakati wa hafla ya kuzindua kitabu hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Habari na Ulaghibishi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Jumanne Issango, Ofisa wa Takwimu kutoka nchini Sweden, Cath Craiger, Mtakwimu kutoka Sweden, Ana Morkuda na Mwanahabari Philip..Kitabu hicho kimeandikwa na wanafunzi watano kutoka Tanzania waliopata mafunzo ya miezi 11 nchini Sweden.

Friday, March 24, 2017

ZIARA YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO ,MAZINGIRA YAENDELEAWaziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais January Makamba akipanda mti katika ziara hiyo.

Ziara maalumu ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais January Makamba kutembelea mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania yenye lengo la kung’amua changamoto za kimazingira, athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo, imeingi siku ya nne.

Hii leo Waziri Makamba ametembelea Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, na kupokea taarifa ya hali ya Mazingira Wilayani hapo taarifa iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi MwanaAsha Tumbo.

Tumbo ameainisha changamoto za kimazingira katika Wilaya yake kuwa ni pamoja na kuwa ni pamoja na Uvuvi haramu, Mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na shughuli za binadamu zisizozingatia uhifadhi endelevu ya mazingira ikiwa ni pamoja na ukataji ovyo wa miti ya asili na misitu ya kupanda, kilimo cha kuhamahama na uchimbaji wa madini katika kingo na pembezoni mwa vyanzo vya maji.

Tumbo amesema kuwa hivi sasa wilaya ya Muheza inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mvua kutoka misimu mitatu kwa mwaka hadi kufikia msimu mmoja tu.
"katika siku za hivi karibuni kumekua na ongezeko kubwa la uchimbaji holela wa madini unaopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira".

Ili kuimarisha doria kikamilifu wakazi wa Wilaya ya Muheza wamewasilisha ombi maalumu la kujengewa nyumba za askari hii ni baada ya kupata msaada kutoka United Nations Development Programme ambao wamekubali kujenga kituo cha polisi. Aidha, jitihada mbalimbali zimechukuliwa na uongozi wa Wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka zuio la ukataji miti hovyo.

Miti iliyopigwa marufuku ni pamoja na miti iliyooteshwa kwa juhudi za watu binafsi na hata ile ya mashirika/taasisi.

Kwa upande wake Waziri Makamba ameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa juhudi za dhati za kuhifadhi mazingira, pia kuanzishwa kwa kampeni maalumu ya kupanda miti.
Jitihada nyingine ni pamoja na kufukia mashimo yote yaliyochimbwa na wachimbaji wadogo wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Kihara, katika msitu wa Amani.

Katika siku hii ya nne Waziri Makamba alipata fursa ya kutembelea "Amani Nature Researve" ambapo alishuhudia ni kwajinsi gani mazingira yamehifadhiwa na kuchangia kwa kiasi kikubwa mradi wa kuzalisha vipepeo na kuuza nje ya nchi biashara ambayo imekua ikiwasaidia wakazi wa kijiji hicho katika kusomesha watoto wao na kujenga nyumba bora za kuishi.

Wakazi hao wa kijiji cha Kata ya Fanusi walianisha changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa kuwa ni kukosa soko la kuuza vipepeo hao baada ya kuzuiwa na Serikali.
"Niwahikikishieni kuwa suala hili tutalichukua na kulifikisha katika Wizara husika na naamini litafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo" Makamba alisisitiza.

Nae Mhifadhi wa msitu wa Amani Mwanaidi Kijazi ameainisha umuhimu huo kuwa ni pamoja na hifadhi ya bionuai na mifumo ya ikojia, hifadhi ya viumbe hai adimu duniani, maumbile ya asili maalumu kwa utunzaji wa vinasaba na chanzo kikubwa cha vyanzo vya maji.

Ziara ya Waziri Makamba katika mkoa wa Tanga hii leo imefanyika katika Wilaya ya Muheza ambapo ameshiriki katika zoezi la kupanda miti, kutembelea misitu wa Amani na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kihara na kuwasisitiza wakazi wa eneo hilo kutunza rasilimali zilizopo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Aidha, katika kuchangia shughuli za maendeleo kijijini hapo Waziri Makamba ameahidi kununua miche ya miti 150,000 kwa ajili ya kuigawa maeno mbalimbali ya wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya jitihada kwa wakazi hao kupanda miti kwa wingi kwa lengo la kulinda na kutunza mazingira.

SERENGETI BOYS WACHANJWA

SERENGETI BOYS WACHANJWA Timu ya Tanzania ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys leo Machi 24, wamefanyiwa chanjo ya ugonjwa wa manjano (yellow fever) kabla ya kuanza safari ya kwenda Morocco, Cameroon na Gabon. Timu hiyo imefuzu kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.

Fainali hizo zinatarajiwa kuanza Mei 14 mwaka huu na mapema mwezi ujao itasafiri kwenda Morocco kwa ajili ya kambi.

Kambi hiyo itakuwa ni ya mwezi mmoja (Aprili 5 hadi Mei 1, 2017) kabla ya kuwa na kambi ya wiki moja huko Cameroon (Mei mosi hadi Mei 7, mwaka huu) na baadaye itafanya kambi nyingine Gabon (Mei 7 mpaka Mei 13) angalau kwa wiki moja kabla ya kuanza fainali hizo Mei 14, mwaka huu.

TFF YAPUNGUZA KIINGILIO MECHI TAIFA STARS

Taifa Stars - timu ya Tanzania ya mpira wa miguu kwa mwaka 2017 inaingia uwanjani kucheza na Botswana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya kirafiki ya kimataifa katika wiki ya kalenda ya FIFA.

Kwa umuhimu wa mchezo huo na hamasa ambayo uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania umeona hivyo TFF imeatangaza kushusha bei ya kiingilio kwa watu watakaokaa mzunguko kutoka Sh 5,000 hadi Sh. 3,000.

“Wavutieni Watanzania wakaishangilie timu yao, wekeni viingilio vya bei ya chini ambayo Mtanzania itamweka katika mazingira ya kuchangia gharama kidogo kwa timu. Toeni hiyo Sh 5,000 yenu. Wekeni angalau Sh. 3,000,” ameagiza Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Pamoja na punguzo hilo kwa mashabiki wa mpira wa miguu watakaoketi Majukwaa Maalumu - VIP “A” watalipia Sh 15,000 na wale watakaoketi VIP “B” na “C” watalipia Sh 10,000. Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga kwa upande wake aliwathibitishia Waandishi wa Habari kwamba kikosi chake kiko imara kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10.00 jioni.

“Tuna morali wa hali ya juu,” alisema Mayanga ambaye aliteuliwa kuinoa timu hiyo mapema mwaka huu. Kwa upande wa Peter Buffler – Kocha Mkuu wa Botswana, alisema kwamba anatarajiwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu amegundua kuwa kikosi cha Taifa Stars kina vijana wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Mbali ya mchezo huo wa kesho, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo mwingine dhidi ya Burundi Jumanne ijayo, Machi 28, mwaka huu.

Mchezo ambao pia ni wa kirafiki wa kimataifa unatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni.

MWAMUZI ADONGO AONYWA

Mwamuzi Jacob Adongo amepewa ONYO KALI kwa kushindwa kutafsiri vizuri sheria katika mechi namba 186 kati ya Simba na Mbeya City iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Onyo hilo limetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 38 (5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.

Kadhalika katika mchezo huo namba 186 (Simba 2 vs Mbeya City 2). Klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi, hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.

Adhabu dhidi ya Mbeya City imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu. Mechi namba 190 (Kagera Sugar 1 vs Majimaji 0). Klabu ya Majimaji imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kosa la kutokuwa na Daktari kwenye Kikao cha Maandalizi ya Mechi (Pre Match Meeting) na hata uwanjani wakati wa mchezo.

Kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Kuu, na adhabu ni uzingativu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu. Pia kwa kutumia Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu imefuta kadi ya njano aliyooneshwa mshambuliaji Jaffari Salum wa Mtibwa Sugar katika mechi hiyo namba 175 kati ya African Lyon na Mtibwa Sugar iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kubaini haikuwa sahihi.

Klabu ya Yanga iandikiwe barua ya Onyo Kali kutokana na benchi lake la ufundi kumlalamikia mara kwa mara Mwamuzi wakati wa mechi ya utangulizi ya U20 kati ya timu hiyo na Simba iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kuhusu mechi za Ligi Daraja la Pili (SDL Play Off) Mechi namba 3 (Oljoro 1 vs Transit Camp 1).

Klabu ya Oljoro imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kutokana na washabiki wa timu hiyo kumrushia mawe Mwamuzi akiwa uwanjani.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

WAANDISHI WA HABARI WAASWA KUANDIKA HABARI ZA MAENDELEO
Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa waandishi wa habari nchini kuandika habari zinazohamasisha maendeleo ya nchi badala ya kuandika habari ambazo hazina manufaa kwa taifa.

Akizungumza wakati ya hafla ya kuwaapisha mawaziri, mabalozi pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais Magufuli alisema kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kuwa wazalendo kwa kuandika habari za kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo pamoja na kuunga mkono jitihada mbalimbali za Serikali.

“Nchi yetu ina sifa nzuri nje, Rais wa Benki ya Dunia alipotembelea katika nchi yetu hivi karibuni alitupatia jumla ya shilingi trilioni 1.74 na benki hiyo ipo mbioni kutupatia fedha nyingine shilingi trilioni 2.8, lakini vyombo vyetu vya habari haviandiki kwa mapani juu ya taarifa ” alisema Rais Magufuli.

Alibainisha kuwa fedha hizo zitatumika katika miradi ya Ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo, maboresho ya miji, pamoja na Vyuo Vikuu vya Sokoine na Mandela na kuleta maendeleo ya nchi yetu lakini taarifa zake hazikupewa uzito unaostahiki katika vyombo vya habari.

Rais Magufuli aliwataka wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari kufuata uweledi wa taaluma ya habari pamoja na kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya mtu mmoja mmoja.

Aidha, Rais Magufuli amewapongeza viongozi aliowaapisha na kuwataka kufanyakazi kwa bidii na juhudi ili kutimiza azma ya serikali ya kuwa nchi ya uchumi wa kati kwa kutekeleza agenda ya viwanda. 

Viongozi walioapishwa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Alfayo Kidata. Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dkt. Abdallah Possi, Balozi wa Tanzania nchini Israel Job Masima, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Sylvester Mabumba pamoja na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Stellah Mugasha.

DKT. KEBWE AHUDHURIA KIKAO CHA MAANDALIZI YA MAONESHO YA KILIMO

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen Kebwe akizungumza wakati wa kikao cha Kamati kuu ya Tathmini na Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) Kanda ya Mashariki
Baadhi ya washiriki wa kikao cha Kamati kuu ya Tathmini na Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) Kanda ya Mashariki wakifatilia kikao hicho kwa makini
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisikiliza kwa makini wakati wa kikao cha Kamati kuu ya Tathmini na Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) Kanda ya Masharikikilichofanyika Mkoani Morogoro
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe Godwin Gondwe akifatilia kwa makini kikao cha Kamati kuu ya Tathmini na Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) Kanda ya Mashariki kilichofanyika Mkoani Morogoro, Kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo Ndg James Mkumbo
Mkuu wa Wilaya ya Muheza Hajat Mhandisi, Mwanasha Tumbo akichangia jambo wakati wa kikao cha Kamati kuu ya Tathmini na Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) Kanda ya Mashariki

Na Mathias Canal, Morogoro


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen Kebwe ameongoza kikao cha Kamati kuu ya Tathmini na Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) Kanda ya Mashariki inayounganisha Mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Pwani na Morogoro.

Kikao hicho kilichokuwa na Agenda sita kimefanyika Katika Ukumbi wa JKT Nane Nane Manispaa ya Morogoro ambapo kwa kauli moja kimepitisha Agenda zote sita ikiwemo kupitia Taarifa ya Tathmini ya Maonesho ya Nane Nane 2016 sawia na Taarifa ya Maandalizi ya Maonesho ya Nane Nane ya mwaka 2017 ambayo Kitaifa yanayotaraji kufanyika Mkoani Morogoro.

Akizungumza wakati Akifungua kikao hicho Dkt Kebwe ameitaka kamati inayoratibu shughuli hizo ya TASO kuweka wazi mapato na matumizi ya fedha wanazozipata kwani kufanya hivyo ni kujenga zaidi uaminifu kwa wananchi na kujihuisha kwa pamoja na wadau mbalimbali ili kukuza uchumi nchini kupitia Kilimo.

Dkt Kebwe alisema kuwa TASO kutofanya hivyo ni njia mojawapo ya kuzifanya Halmashauri zingine kutochangia kwa kuhofia fedha zao kutumika pasina weledi uliokusudiwa.

Sambamba na hayo pia amewasihi wadaiwa sugu kulipa madeni yao haraka iwezekanavyo kwani kufanya hivyo itaongeza ustawi na uimara wa Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo na hatimaye Kilele chake kuwa na Tija kwa jamii.

Dkt Kebwe amewapongeza wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya waliohudhuria katika kikao hicho ambapo alisema kuwa wanafanya kazi nzuri na kuonyesha ushirikiano imara katika Maandalizi hayo japo amesisitiza kuongezwa kwa jitihada za Maandalizi ili Maonesho hayo yawe na weledi na tija.

Sherehe za Maonesho ya Kilimo Nane Nane hufanyika kwa lengo la kuwakutanisha wakulima, wafugaji, na wavuvi kwa kuwaelimisha watazamaji na hasa wakulima, wafugaji na wavuvi kujifunza na kupata uzoefu wa teknolojia na mbinu zinazotumika kuongeza uzalishaji katika eneo la kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Katika Maonesho hayo mambo muhimu hutawala ikiwa ni pamoja na kuonyesha mazao mbalimbali sambamba na mifugo mbalimbali kwenye mabanda.

Akizungumza na Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amewapongeza viongozi wote kwa namna ambavyo wanashiriki kuandaa Maonesho hayo huku akisema kuwa pamoja na Halmashauri ya Ubungo kuwa mpya na inaanza kushiriki katika Maonesho hayo kwa Mara ya kwanza atahakikisha kuwa maonesho yanakuwa na tija katika mabanda yote yanayoendelea kuandaliwa na Maafisa Kilimo, Uvuvi na Mifugaji.

MD Kayombo alisema kuwa kupitia Maonesho ya Kilimo mwaka huu 2017 wananchi watapata fursa ya kujifunza mbinu za ufugaji kwa kutumia mabanda bora, Uchanganyaji wa vyakula vya mifugo na ulishaji, Teknolojia bora ya ufugaji wa samaki wengi katika eneo dogo, Utotoleshaji vifaranga kwa kutumia incubator ya kienyeji na kisasa, Uhamilishaji wa samaki na Ng'ombe na teknolojia Nyinginezo.

Akifunga kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe Stephen Kebwe ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa Kikao hicho alizitaja changamoto za maandilizi za Maonesho ya Kilimo kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa michango kutoka kwa wadau mbalimbali pamoja na kuchelewa kuthibitisha mialiko kwa wageni walioalikwa kutembelea Maonesho ya Kilimo Nane Nane.

Thursday, March 23, 2017

TAMTHILIA YA MFALME KIMA YA CHINA ILIYOTAFSIRIWA KWA KISWAHILI YAZINDULIWA

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel (wa nne kutoka kushoto) na Naibu Waziri wa Masuala ya Utangazaji, Filamu na Habari wa China, Tong Gong (katikati), wakikata utepe kuzindua maonyesho ya kwanza ya tamthiliya ya China ya 'Mfalme Kima' iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili. Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kushoto ni Jiang Almin, ambaye ni Mkurgenzi wa Radio China Kimataifa, wa pili kutoka kulia ni Suzan Mungy (Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma na Matukio wa Shirika la Utangazaji Tanzania - TBC) na wa nne kulia ni Ma Li (Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa wa China).

Wednesday, March 22, 2017

SOKO LA MBAO LIMESHUKA WILAYANI MUFINDI Mbunge wa mafinga mjini Cosato Chumi akiongea na
Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wilayani Mufindi juu ya malamiko yao kwa TRA mkoa wa Iringa
 Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wilayani Mufindi waliohudhulia mkutano wa pamoja kati ya mbunge,TRA na wafanyabiashara.

Na Fredy Mgunda,Mufindi

Wafanyabiashara wa mazao ya misitu wilayani Mufindi wamesema kuwa soko la mbao limeshuka kwa kiwango kikubwa kutoka na mrundikano wa kodi katika wilaya hiyo tofauti na wilaya nyingime.

“Ukienda mbeya,njombe na maeneo mengine kodi ya vibali ni ndogo kuliko ya hapa mufindi sasa tunataka kujua tatizo nini”walisema wafanyabiashara
Aidha wafanyabiasha hao wameiomba mamlaka ya mapato mkoa wa iringa TRA kutoa kibali cha usafirishaji kwa  kuondoa usumbufu wa tozo za ushuru check point na kuombwa lisiti za mashine kutoka kwa wakulima waliowauzia mbao na nguzo.

Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara hao Zakayo Kenyatta Katika mkutano wa wafanyabiashara wa mazao ya misitu na TRA alisema kuwa TRA wamekuwa wasumbufu sana check point kwa kuwasimamisha zaidi ya siku tatu wakidai lisiti hizo huku wafanyabiashara wakionyesha barua za watendaji kutoka vijiji walivyonunulia zikikataliwa.

"Tunawaomba TRA mkatoe elimu kwa mkulima mmoja mmoja kwa sababu ni ngumu sana mkulima wa  chini akuulizie nguzo 5 alafu awe na lisiti ya mashine kwa hiyo tunawaomba TRA wakatoe elimu hiyo na kuwaamasisha wakulima hawa Kuwa na hizo mashine kwani wakulima hao ni wale ambao wanauza miti yako kutokana na matatizo mbali mbali walionayo na sio kampuni" alisema Kenyatta

Akijibu hoja hiyo meneja msaidizi WA TRA mkoa WA iringa Mustapha Mkilamwenye alisema Kuwa wamekuwa wakiogopa kwenda kutoa elimu hizo kwa wakulima kutokana na mkutano yao kuharibika kwa kuzomewa na kutokufikia muafaka WA uelimishaji.Pia Mkilamwenye amewataka wafanyabiashara hao kupata kibari cha kununua na kusafirisha kutoka TRA wilaya au mkoa kabla hqwqjaenda vijijini kununua ili kukwepa uwumbufu huo check point."Ombi lenu tumelipokea hivyo tunawaomba kabla hamjanunua mpate kibali kutoka TRA mkoa au wilayani kuokoa usumbufu WA tozo za ushuru check point, pia tutatoa elimu ya matumizi ya mashine kwa wakulima vijijini wauzapo miti yako kwa wafanyabiashara" alisemaKwa upande wake Mbunge wa mafinga mjini Cosato Chumi alisema Kuwa ameamua kuwakutanisha wafanyabiashara na TRA kupata ufafanuzi WA kuombwa ushuru check point kutokana na kulalamikiwa na wafanyabiashara hao Kuwa magari yako wamekuwa wakikaa check point zaidi ya siku tatu wakiombwa lisiti za mashine kutoka kwa wakulima waliowauzia nguzo na mbao."Mkutano huku ni mahususi kwa wrote tukipata ufafanuzi na kujua kwa nini mnakamatwa check point na mkiobwa ushuru au njia kila mkoa,tra wanapaswa Kuwa rafiki Wa wafanyabiashara na sio adui kwa sababu mufindi ndio chanzo kikuu cha mapato ya nchi kutokana na zao LA mbao" alisema ChumiMeneja wa TRA wilayani ya Mufindi Filmoni Mwakapesile alisema Kuwa "ni kweli tuhuma hizo na lawama tumezipata na tumekuwa tukipokea simu nyingi za wafanyabiashara na kutatua matatizo yako lakini Leo tunashukuru Mbunge amekututanisha na tumewapa uelewa na sisi kama TRA tumewaambia mini cha kufanya kuondoa huo usumbufu"

DC DODOMA AWATAHADHARISHA WANANCHI WA KATA YA NALA


SERIKALI YAWABWAGA WANAOPINGA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI

Na Mwandishi wetu

Serikali yawabwaga wanaopinga Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kutupilia mbali pingamizi hilo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hii, Wakili wa Serikali Evordy Kyando alisema kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali pingamizi lililotolewa na baadhi ya wadau wa habari wakipinga baadhi ya vifungu katika Sheria hiyo baada ya kukosa mashiko.

Alisema kuwa katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2017, walalamikaji wanadai kuwa kuna baadhi ya vifungu vya sheria hiyo vinakandamiza uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza na vinakiuka Ibara ya 18 ya katiba ya nchi.

Aidha, Wakili Kyando alibainisha baadhi ya vifungu katika sheria hiyo vilivyolalamikiwa ni pamoja na 7 (2) (B) (III) (IV) and (V), 7 (3) (A), (B), (C), (F), (G), (H), (I), (J),8, 9(B), 10(2), 11(4), 13, 14, 19, 20, 21, 24, 25, 26, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 52, 53, 54 58 na 59 vya Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya 2016.

Akifafanua zaidi, Wakili Kyando alisema kuwa kuna baadhi ya hoja zilizopelekea Shauri hilo kutupiliwa mbali ikiwemo vifungu vya Sheria vilivyolalamikiwa viliandikwa vibaya kulingana na Sheria yenyewe ilivyo, viapo vilivyowasilishwa katika kufungua shauri vilikuwa na makosa, jambo lililolalamikiwa halina mashiko, si la kisheria kutokana na malalamiko ambayo hayaoneshi msingi ulipo ikiwa lengo la Sheria ni kuboresha mazingira mazuri ya waandishi, Elimu, mishaara na vitambulisho.

Jopo la wanasheria linalowakilisha upande wa Serikali liliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Makao Makuu, Mark Mulwambo, Wakili Mwandamizi wa Serikali toka Kanda ya Mwanza Ndamugoba Castus na Wakili wa Serikali Evordy Kyando. Kesi hiyo iliyofunguliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited, wakipinga baadhi ya vipengele vya Sheria ya Huduma za Habari 2016.

BOMOA BOMOA YAIKUMBA KURASINI

 Katapila likibomoa majengo ya Baa ya Pentagon  katika oparesheni ya bomoa bomoa nyumba zote zilizojengwa katika hifadhi ya Reli ya Kati eneo la Mivinjeni, Kurasini Dar es Salaam.
(PICHA NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG)
 Makontena ya biashara yakiwa yamefumuliwa na katapila
 Baa ya Pentagoni ikiwa imebomolewa 
 Katapila likiendelea na kazi ya bomoa bomoa

 Baadhi ya wafanyabiashara ndogo ndogo waliokuwa na vibanda vya biashara pamoja na wananchi wakishuhudia ubomoaji huyo
 Askari wakilinda doria wakati wa ubomoaji
Wataalamu wakipima mita 20 kutka kwenye reli ili nyumba na mabanda yaliyo ndani ya hifadhi ya reli zibomlewe kupisha ujenzi wa reli ya kisasa.

TANZANIA NA CHINA ZATILIANA SAINI MKATABA WA MIAKA MITATU WA MASUALA YANUTAMADUNI

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (kushoto) na Naibu Waziri wa Utamaduni wa China, Dong Wei (kulia) wakibadilishana mkataba wa makubaliano utekelezaji wa masuala ya Utamaduni baina ya nchi hizo wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Serena ijini Dar es Salaam leo.

UBALOZI WA MAREKANI WATOA MAFUNZO KWA BLOGGERS WA NCHINI TANZANIA

Mkufunzi wa Mafunzo hayo Ricci Shryock akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa, kufadhiliwa na Kufanyika kwenye Ubalozi wa Marekani jijini Dar es salaam nchini Tanzania washiriki wa mafunzo hayo ambao ni wanahabari wa Mitandao ya kijamii. (PICHA KWA HISANI YA UBALOZI WA MAREKANI)
Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada zilizotolewa na maafisa mbalimbali kutoka ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.

WAZIRI NAPE APOKEA RIPOTI YA KAMATI YA UCHUNGUZI WA TUKIO LILILOTOKEA CLOUDS MEDIANa Shamimu Nyaki ,Dar es Salaam

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amepokea taarifa ya kina kuhusu chanzo, sababu na namna tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda alivovamia kituo cha Utangazaji cha Clouds Media akiwa na walinzi wenye silaha Machi 17, 2017.

Akipokea taarifa hiyo leo Jijini Dar es Salaam kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Dkt.Hassan Abbas ameishukuru Kamati kwa utulivu wao na kuifanya kazi hiyo kwa utaalamu na umakini mkubwa huku jamii ikitaka matokeo kwa haraka.

Aidha Nape amesema kuwa ripoti hiyo ataiwasilisha kwa mamlaka husika kwa ajili ya uamuzi na maelekezo.

“Nimeipokea ripoti na ninawahakikishia kuwa nitaikabidhi ripoti hii kwa wakubwa zangu wao ndo wenye mamalaka ya kufanya chochote”,Alisema  Nape.
Kamati aliyoiunda Mhe Waziri ilikuwa na wajumbe wanne ambao ni Bw.Deodatus Balile kutoka Jamhuri,Bw.Jesse Kwayu wa Gazeti la The Guardian,Bibi Nengida Johanes wa Upendo Media na Mabel Masasi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walioongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt.Hassan Abbas .

Tuesday, March 21, 2017

BASATA KUTOA TUZO KWA WANAFUNZI

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) lenye dhamana ya kufufua, kukuza na kuendeleza sekta ya Sanaa nchini litatoa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya sanaa siku ya Jumatatu tarehe 27/03/2017 saa 4:00 asubuhi katika Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Sheria Na. 23 ya Mwaka 1984, mojawapo ya majukumu makuu ya Baraza ni kufufua na kukuza shughuli za uzalishaji wa sanaa, ili kukamilisha adhama hii Baraza limeamua kufufua programu yake ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi wa shule za sekondari ambao wanashika nafasi za juu kitaifa katika masomo ya sanaa husasan Sanaa za Ufundi, Maonyesho na Muziki. Sanaa ni chanzo cha ajira kwa vijana wengi ambao wameweza kujipatia kipato na umaarufu kupitia fani hizi za sanaa.

Hata hivyo masomo haya yamekuwa hayapatiwi kipaumble kama ilivyo masomo mengine katika shule za Msingi na Sekondari.

Tuzo hizi zitakuwa nyenzo kwa ajili ya kujenga hamasa, ari, ubunifu na juhudi katika kuleta maendeleo kupitia masomo ya sanaa. Katika program hii wanafunzi kutoka shule 5 za sekondari zitakazohusika katika kupewa tuzo hizo, shule hizi ni Loyola, Azania za Dar es Salaam, Bukoba ya Mkoa wa Kagera, Darajani toka Mkoa wa Kilimanjaro na Arusha Sekondari toka mkoa wa Arusha.

Matarajio ya BASATA kuwa utoaji wa tuzo hizi utachochea wanafunzi wengi kusoma masomo ya sanaa, kuongeza ubunifu katika kazi za Sanaa na kuwasaidia katika kuongeza ufaulu wao darasani hasa ikizingatiwa Sanaa ni nyenzo katika kumuandaa mtoto kielimu na kimaadili.

Itakumbukwa kuwa BASATA limekuwa na mwendelezo wa programu mbalimbali za Sanaa kwa watoto zilizoanza tangu miaka ya 1980 ambazo zimepata kuibua na kukuza vipaji vya wasanii. BASATA linachukua fursa hii kuwaalika wananchi na wadau wote wa sanaa kufika kwa wingi kushuhudia utoaji wa tuzo hizi.

Sanaa ni kazi, tuipende, tuikuze na kuithamini

Godfrey Mngereza KATIBU MTENDAJI

Monday, March 20, 2017

EMMANUELA ACHUKUA FOMU BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI NA KATI

Bi.Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, mmoja wa wagombea ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki akikabidhiwa fomu na  Bw. Said Bakari wa  Idara ya Uhusiano wa kimataifa katika makao makuu ya CCM mtaa wa  Lumbumba jijini Dar es salaam.
Bi. Emmanuela Mtatifikolo Kaganda, mmoja wa wagombea ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki akitoka nje baada ya kukabidhiwa fomu za kugombea nafasi hiyo makao makuu ya CCM mtaa wa  Lumbumba jijini Dar es salaam. Bi Kaganda alifika hapo akiwa peke yake na bila mbwembwe akiwa na imani kwamba dhamira yake ya kusimamia na kutetea maslahi ya kina mama na watoto katika jamii ni agenda yake itayomsimamia katika kinyang'anyiro hicho.

Sunday, March 19, 2017

BALOZI WA TANZANIA NCHINI UJERUMANI MARMO AMEMVISHA CHEO KANALI WA JWTZ JIJINI BERLIN

Katika hali ambayo haijazoeleka na iliyoonekana kuwa ngeni, Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo alimvisha Cheo Kanali Joseph Bakari aliyepandishwa Cheo hivi karibuni kutoka Luteni Kanali.


Hafla hiyo fupi iliyohudhuriwa na  ujumbe wa Watanzania waliohudhuria Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Jijini Berlin Ujerumani akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya Utalii na Utamaduni Mhe. Chimberi Heri, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania  Mhe. Geofrey Meena, Maafisa wa Ubalozi na wageni wengine ilifanyika karibuni katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Berlin nchini Ujerumani.

Akitoa maelezo mafupi kuhusu tukio hilo  Mhe. Balozi alitanabaisha kuwa kwake ni tukio la kwanza na la la aina yake kupewa dhamana hiyo  na kwamba amepokea maelekezo husika kutoka Makao Makuu ya Jeshi kupitia Wizarani. 

Akisoma sehemu ya maelekezo hayo alisema “ kwa kawaida Afisa anapopanda cheo akiwa nje ya nchi iwapo hataweza kwenda Tanzania kuvalishwa cheo hicho na viongozi husika wa JWTZ, cheo hicho kipya huvishwa na Afisa Mkuu au Balozi wa Tanzania katika Nchi aliyepo”. 

Hivyo, kwa mujibu wa sheria na mamlaka aliyekuwa nayo anatakiwa kumvisha Cheo kipya cha ukanali mhusika kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania. Kwa mujibu wa maelekezo hayo Kanali Bakari alipandishwa cheo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kuanzia tarehe 31 Januari 2017.

Akitoa nasaha fupi na salam za pongezi kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, wageni waliohudhuria hafla hiyo na Watanzania wote kwa ujumla kwa  Kanali Bakari aliyefuatana na Mkewe Bi Lucy Mlingi, Mhe. Balozi alimkumbusha Kanali Bakari kuwa ni dhahiri kuwa kupandishwa kwake cheo kumetokana na imani ya Mkuu wa Majeshi na viongozi wengine wakuu katika utendaji wake,uadilifu, bidii katika kazi na utii.

 Hivyo ni vizuri ahakikishe kuwa anafanya kazi kwa weledi,  bidii zaidi na moyo wa kujituma ili kuleta tija na ufanisi zaidi kwa manufaa ya JWTZ, Tanzania na Dunia kwa ujumla. Mwisho aliipongeza familia yake hususani  Mkewe kwa mafanikio hayo na kuwatakia   heri, Baraka na afya njema.

Kanali Joseph Bakari ni mwakilishi wa JWTZ katika Sekretarieti ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (International Military Sports Council-CISM) kama Mshauri na msaidizi wa Mkurugenzi wa Michezo katika Baraza hilo.

Baraza hilo liliundwa tarehe 18 Februari 1948 mara baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Dhima kuu ikiwa ni kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili kama njia ya kueneza amani duniani badala ya vita. Baraza hilo lina jumla ya nchi wanachama 134 Tanzania ikiwemo. Miongoni mwa shughuli  za Baraza hilo ni kuandaa mashindano ya michezo ya majeshi ya Dunia.

 Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo na  Acting Colonel Joseph Bakari wakisikiliza maelezo kabla ya hatua ya kumvua cheo cha zamani na kumvika kipya
 Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akimvisha cheo kipya Colonel Joseph Bakari 
Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akimvisha kofia ya cheo kipya Colonel Joseph Bakari 
 Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akipikea zawadi maalumu ya  Sekretarieti ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (International Military Sports Council-CISM)  toka kwa Kanali Joseph Bakari wakati wa hafla hiyo
 Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akiwa na  Kanali Joseph Bakari na mkewe 
 Balozi wa Tanzania Mhe. Philip Marmo akiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma (kushoto)  Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya Utalii na Utamaduni Mhe. Chimberi Heri (wa pili kulia) Colonel Joseph Bakari na mkewe 
 Tukio hilo la kuvisha Cheo  lilihitimishwa na kuimbwa wimbo wa Taifa wa Tanzania.
 Picha ya pamoja na ujumbe wa Watanzania waliohudhuria Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Jijini Berlin Ujerumani akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Mshauri wa Rais wa Zanzibar mambo ya Utalii na Utamaduni Mhe. Chimberi Heri, Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania  Mhe. Geofrey Meena, Maafisa wa Ubalozi na wageni wengine ilifanyika karibuni katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania zilizopo Berlin nchini Ujerumani. 

Source: Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Berlin Ujerumani

MD KAYOMBO AONYA MAOFISA WA KATA NA MITAAKUCHUKUA RUSHWA

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akitoa ufafanuzi wa muongozo wa ukusanyaji wa mapato kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa
 Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo
 MD Kayombo akisisitiza jambo


Na Mathias Canal, Dar es salaam

Maafisa Watendaji wa Kata 14, Watendaji wa Mitaa 91 pamoja na Wahasibu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wameonywa kutopokea Rushwa wala hongo ya aina yoyote kutoka kwa wamiliki wa biashara mbalimbali katika Manispaa hiyo kwani kufanya hivyo watadhoofisha ukusanyaji wa mapato ya serikali kama ilivyokusudiwa.

Kauli ya onyo imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakati akitoa ufafanuzi wa muongozo wa ukusanyaji wa mapato na kutoa maelekezo ya majukumu ya kazi kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa kwenye kikao cha kazi kilichofanyika leo Jumamosi Machi 18, 2017 katika ukumbi wa Ofisi za Manispaa hiyo ilipo Mtaa wa Kibamba CCM.

Kayombo ameeleza kuwa kwa mtumishi yoyote wa Manispaa kwa ngazi yoyote atakayebainika kujihusisha na ubadhilifu kwa kuchukua Rushwa kwa walipa kodi atachukuliwa hatua Kali za kisheria kwa kuiibia serikali kwani kuihujumu serikali kwa kuiibia mapato au kuzuia ukusanyaji wa mapato ni kosa kwa mujibu wa taratibu na sheria.

"Nina amini kwamba mnaishi vizuri na wananchi wenu kwahiyo mnawafahamu vizuri wafanyabiashara wanaokwepa kulipa Kodi lakini hata walipaji wazuri hivyo jambo la ukusanyaji mapato litakuwa jepesi sana kwenu kutokana na uzoefu mlionao" Aliongeza Kayombo

Mkurugenzi huyo amewasisitiza Watendaji hao kusimamia vyanzo vyote vya mapato ikiwemo Hotel Levy, Service Levy, Mabango makubwa na madogo (Bill Board), Leseni za biashara na Vileo, Upimaji afya kwa ngazi za Mitaa hususani katika Migahawa.

Hata hivyo amewataka Watendaji hao kufanya kazi kwa ushirikiano, Uaminifu, na Weledi mkubwa kwani kufanya hivyo kutasababisha ukusanyaji mkubwa wa Mapato kwa mwaka 2016/2017.

Kayombo Amewataka Watendaji wote kukagua Maduka yote katika maeneo yao ya kazi ili kubaini Maduka yasiyokuwa na leseni na Yale yenye leseni kuwa na Leseni za Manispaa ya Ubungo kwani wafanyabiashara wa Maduka mengi wamekuwa na kisingizio cha kukata leseni na Kodi mbalimbali katika Manispaa ya Kinondoni na kutaka kulazimisha kuitumia leseni hiyo kama halali kwa Manispaa ya Ubungo.

Sambamba na hayo pia MD Kayombo amewataka Maafisa biashara kutochelewesha leseni za wafanyabishara waliokamilisha taratibu zote za kumiliki leseni kwani kufanya hivyo ni kuchelewesha huduma kwa wananchi na kuongeza makwazo kwa wafanyabishara kwa sababu tu ya kuchelewa kusaini leseni.

Alisema kuwa litakuwa ni jambo la aibu na lisilovumiliwa kwa kuruhusu sheria zitungwe kwa umakini mkubwa lakini utekelezaji wake uwe hafifu.

MD Kayombo aliongeza kwa kusema kuwa hakuna Haki bila wajibu hivyo Watendaji hawapaswi kufanya kazi kwa mazoea lakini pia kutofanya kazi kwa kuongozwa na tamaa.

MD Kayombo amesema kuwa Oparesheni hiyo ya itakayodumu kwa miezi mitatu ya ukusanyaji wa mapato itaanza jumatatu Machi 20, 2017 kwa ushirikiano baina ya watendaji kutoka Makao makuu ya Wilaya, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Mitaa na wenyeviti wa serikali za Mitaa.
 
 
Blogger Templates