Dar es Salaam
Waandishi wa habari Tanzania na Oman kutoka vyama vya Jukwaa la Wahariri (TEF), JOWUTA na OJA leo wamemesaini MoU ya ushirikiano, ambayo utekelezaji wake utaongozwa na mpango kazi wa muda wa mwaka mmoja.
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 1 Oktoba 2026 katika kongamano la siku moja lililofanyika Hoteli ta Serena Jijini Dar es Salaam mbele ya Waandishi wa OJA,JOWUTA.
Jambo hilo la kihistoria limelengq kukuza uhusiano wa kiqsili baina ya nchi mbili Oman na Tanzania sanjari na kuwa na lengo la kuimarisha uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni, kiuchumi na kijamii kupitia sekta ya habari, baada ya Chama cha Waandishi wa Habari Oman (OJA), Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kusaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU).Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Abbas Kilima, amesema Tanzania na Oman zina historia ndefu ya uhusiano unaojengwa kupitia biashara, utamaduni na mahusiano ya watu kwa watu.
Amesema kuwa Bahari ya Hindi haikuwa kizuizi kwa watu wa pande hizo mbili, bali imekuwa daraja lililowaunganisha katika biashara, lugha, maarifa na tamaduni, akisisitiza kuwa wanahabari wana nafasi kubwa ya kuieleza historia hiyo kwa vizazi vya sasa, hususan vijana ambao huenda hawana uelewa wa kutosha kuhusu uhusiano huo.
Balozi Kilima amewapongeza JOWUTA na TEF kwa kufanikisha kongamano hilo, alisema utekelezaji wa MoU hiyo utatoa fursa za mafunzo, kujenga uwezo wa wanahabari, kubadilishana ziara za kikazi na uzoefu, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta za utalii na michezo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma, amesema kongamano hilo ni hatua muhimu katika kuendeleza uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Oman, huku akieleza kuwa wanahabari wameamua kuwa sehemu ya msingi ya kuendeleza uhusiano huo wa kihistoria.
Amesema ushirikiano huo utajikita katika masuala ya uhuru wa habari, kubadilishana uzoefu wa kitaaluma na kiteknolojia, fursa za utalii, biashara na uwekezaji, pamoja na programu za kubadilishana ziara kati ya wanahabari wa Tanzania na Oman.
Juma ameongeza kuwa JOWUTA imefanikiwa kuwakutanisha wanahabari wa nchi hizo mbili ili kujadili namna ya kutumia sekta ya habari katika kuimarisha uhusiano wa watu na watu, huku akiwakaribisha wawekezaji kutoka Oman kuwekeza katika sekta ya habari nchini Tanzania, ikiwemo redio, televisheni na magazeti.
Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema Bahari ya Hindi imekuwa kiunganishi muhimu kati ya Tanzania na Oman kwa muda mrefu, hivyo ushirikiano wa wanahabari wa nchi hizo mbili una nafasi ya kuendeleza historia hiyo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Balile amesema mpango kazi wa kipindi cha mwaka mmoja unapaswa kuhusisha ziara za kubadilishana uzoefu, uandaaji wa habari za pamoja na mafunzo ya kitaalamu, ikiwemo matumizi ya teknolojia mpya na akili bandia (AI) katika vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa OJA, Dkt. Mohammed Mubarak Al-Araimi, amesema uhusiano kati ya Oman na Tanzania una mizizi ya muda mrefu na unazidi mipaka ya kijiografia, huku Zanzibar ikiwa miongoni mwa maeneo muhimu yaliyokuwa kitovu cha mwingiliano wa watu, biashara na tamaduni za Oman na Afrika.
Dkt. Al-Araimi amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kutumia historia hiyo kama msingi wa kujenga mahusiano ya sasa na yajayo kwa kuunganisha watu, kuhifadhi kumbukumbu na kufungua fursa mpya za ushirikiano katika biashara, utamaduni, utalii na uwekezaji.
Ameeleza pia kuwa historia ya habari Zanzibar inaonesha namna vyombo vya habari vilivyotumika katika elimu, mawasiliano na mabadiliko ya mawazo, akitaja magazeti ya zamani yakiwemo Al-Najah, Al-Falaq, Al-Nahda na Al-Murshid.
Baadhi ya wanahabari walioshiriki katika kongamano hillo.Baadhi ya wanachama wa OJA
Naye Balozi wa Oman nchini Tanzania, Saud Hilal Al Shidhani, amewapongeza waandaaji wa kongamano hilo na kusisitiza kuwa uhusiano wa Oman na Tanzania una msingi imara wa kihistoria na kiutamaduni.Balozi Al Shidhani amesema ushirikiano katika sekta ya habari utasaidia kujenga uwezo, kubadilishana ujuzi na kuimarisha maadili ya uandishi wa habari, hasa katika kipindi ambacho mitandao ya kijamii na teknolojia vinaendelea kubadilisha tasnia hiyo.
Kongamano hilo limewakutanisha wanahabari, viongozi na wadau kutoka Tanzania na Oman, huku likilenga kuweka msingi wa ushirikiano endelevu kupitia mafunzo, ziara za kubadilishana uzoefu, habari za pamoja, utalii, biashara na uwekezaji.







0 Comments