Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amezitaka Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha zinapanda miche ya mikorosho milioni mbili kwa lengo la kuongeza uzalishaji na tija ya zao hilo, sambamba na kuhakikisha wakulima wanafuata kanuni bora za kilimo na ushauri wa wataalam.
Mhe. Nyongo ametoa agizo hilo leo Oktoba 2, 2026, wakati akizungumza katika Mkutano wa Tasnia ya Zao la Korosho Mkoa wa Pwani kwa msimu wa 2026/2027, uliofanyika katika Wilaya ya Mkuranga. Amesema Mkoa wa Pwani una fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa korosho kutokana na uwepo wa ardhi na hali ya hewa inayofaa kwa zao hilo.
Amesema Mkoa umejiwekea lengo la kuzalisha tani 42,000 za korosho katika msimu wa 2026/2027 na kufikia tani 73,000 ifikapo msimu wa 2029/2030, hivyo amewataka wakulima kuongeza tija kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, ikiwemo kufanya palizi kwa wakati na kutumia viuatilifu sahihi kwa kufuata ushauri wa wataalam wa kilimo.Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakulima kuchukua tahadhari dhidi ya upotevu wa mazao wakati wa mavuno, hususan katika kipindi cha mvua kubwa kinachotarajiwa, kwa kufanya usafi chini ya mikorosho na kuokota korosho kwa wakati ili kuzuia kuoza na kupungua kwa ubora wa zao.
Amezielekeza pia AMCOS kuhakikisha zinakuwa na maturubai ya kutosha kwa ajili ya kuchambulia, kudarajisha na kuanikia korosho, huku waendesha maghala, wasafirishaji na wadau wengine wakitakiwa kuhakikisha mapokezi, udarajishaji, uhifadhi, usafirishaji na uuzaji wa korosho vinafanyika kwa uaminifu na kwa kuzingatia sheria na taratibu.Katika hatua nyingine, Mhe. Nyongo amewataka viongozi na watendaji kuanzia ngazi ya Mkoa hadi vijiji kusimamia kikamilifu mfumo rasmi wa ukusanyaji na uuzaji wa korosho na kudhibiti ununuzi holela wa zao hilo unaojulikana kama “Kangomba”, akieleza kuwa ununuzi huo unaweza kuchangia utoroshaji wa korosho, kushuka kwa ubora na kupunguza manufaa anayopata mkulima.
Mhe. Nyongo amewataka wataalam wa kilimo katika ngazi zote kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha wakulima wanapata ushauri sahihi na kwa wakati, ili kuongeza tija na uzalishaji wa korosho. Pia amewataka wakulima kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam ili kuboresha uzalishaji na ubora wa zao hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa korosho, kuanzia uzalishaji, ukusanyaji, uchambuzi, udarajishaji, uhifadhi, usafirishaji, usindikaji hadi masoko, ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi.











0 Comments