DUME LA RIKA UMASAINI NDIO SAFARI YA KUAGA UJANA.

Katika jamii ya Kimaasai, maisha ya mwanaume hupitia hatua mbalimbali za kimila zinazoonyesha ukuaji, Miongoni mwa hatua hizo muhimu ni kufanyiwa sherehe inayojulikana kwa jina la *Orkiteng le Sirit* ikimaanisha ni mwisho wa ujana na kuingia uzeeni.

Katika hatua hii ambapo mtu anatawazwa kuingia rika la uzee, wazee wa jamii hiyo huchagua *Dume la rika* ambalo lina afya njema na lililohasiwa tangu utoto wake, dume hili siku ya shughuli ndio hutolewa mwanzo kwenye boma lenye Ng’ombe wengi na kumwagiwa maziwa kisha hunyongwa hadi kufa. 

Sherehe ya *Orkiteng le Sirit* , si sherehe ya kawaida bali ni tukio la heshima kubwa linalofanyika kwa kufuata mila na desturi za kale zilizorithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Kwa jamii ya Kimaasai, ni hatua ya ukamilifu wa mwanaume na uthibitisho kwamba ametimiza majukumu yake ya kifamilia na kijamii, kufanyiwa sherehe hii hakuangalii umri ila inazingatia jinsia kwa kuwa anayefanyiwa sherehe hii ni mwanaume pekee, vigezo vinavyoangaliwa ili mwanaume afanyiwe sherehe hii, ni lazima awe ameoa, awe na watoto wa kike na kiume na awe mtu mwema na maadili katika jamii.

Akizungumza wakati wa sherehe hiyo, Alaigwanani wa kabila la kimasai Maningo Rinjo amesema viongozi wa mila wa ukoo kama *(Laizer, Mollel, Laitayo, Ngidong’i)* ndio wenye jukumu la kumchagua dume atakayechinjwa baada ya kujiridhisha kuwa ana sifa zote zinazotakiwa kwa mujibu wa mila na desturi za Kimaasai ili kutekeleza jukumu hilo la kijamii ambalo linahudhuriwa na ndugu wote wa familia na jamii yote ya wamasai inayozunguka Kijiji hicho. 

“Si kila dume anaruhusiwa kutumika katika sherehe hii, sisi viongozi wa mila hukagua na kuthibitisha sifa zake kabla ya kutoa ruhusa ya kuchinjwa, dume wa kutekeleza sherehe hii lazima awe amehasiwa tangu utotoni, hajawahi kumpanda dume jike, pembe zake ziwe zimenyooka bila kupinda mithili ya pembe za mbogo, asiwe mgonjwa na sifa zingine za ndani ambazo viongozi wa kimila ndio huzichunguza kwa undani,” alisema Alaigwanani Maningo Rinjo.

Alaigwanani Olonyori Lemoyan kutoka Ukoo wa Laizer Kata ya Nainokanoka Ngorongoro alisisitiza kuwa si kila mwanaume anastahili kufanya sherehe ya Orkiteng le Sirit, moja wa masharti muhimu ili mwanaume afanyiwe tukio hilo kuwa

na familia yenye watoto wa kike na kiume, awe na mali na uelekeo wa maisha, mtu anayejali watu na awe ni rafiki wa ukoo wake na jamii inayomzunguka pamoja na kupata ridhaa ya ukoo wake kufanya sherehe hiyo. 

“Orkiteng le Sirit ni heshima kubwa katika jamii ya Kimaasai. Mwanaume lazima awe ametimiza wajibu wake wa kifamilia kwa kupata watoto wa kike na wa kiume. Bila kutimiza sharti hilo, hawezi kufikia hatua hii muhimu ya maisha,” alisema Alaigwanani Olonyori Lemoyan.

Wakati wa sherehe hizo baada ya dume kunyongwa na kutolewa nyama zake, mwanaume anayehitimu (anayepandishwa rika) pamoja na mke wake na mama yake mzazi wanatakiwa hukalia utumbo wa dume hilo kama ishara ya kuaga rasmi ujana na kuingia katika hatua ya uzee. Kitendo hicho hubeba maana kubwa ya kiutamaduni na kuashiria mwanzo wa jukumu jipya ndani ya jamii na kuachana na usharobaro na mambo yote ya ujana.

Baada ya taratibu hizo kukamilika, rika la Korianga huungana na mwenzao aliyeingia hatua ya uzee timilifu huimba nyimbo za furaha na heshima huku wakielekea bomani, wakimpongeza mwenzao kwa kufikia hatua hiyo adhimu. Nyimbo hizo huashiria kukubalika kwake rasmi katika kundi la wazee na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika mila, desturi na maamuzi yanayohusu ustawi wa jamii.

*Orkiteng le Sirit* si tu sherehe ya kuchinja dume laa hasha, ni alama ya mafanikio ya maisha, uwajibikaji wa kifamilia na heshima ya kuwa mzee katika jamii ya Kimaasai. Hatua hii ni urithi wa kipekee unaoendelea kuunganisha vizazi na kuhifadhi utamaduni wenye thamani kubwa kwa jamii hiyo.

Post a Comment

0 Comments