Mchezaji wa Kimataifa wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Simon Msuva, amepongeza mpango wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) wa kuandaa mafunzo maalum kwa Waandishi wa Habari kuelekea Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), akisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha mchango wa sekta ya habari katika kuitangaza Tanzania, kukuza vipaji vya wanamichezo na kuibua fursa mbalimbali za maendeleo zitakazotokana na mashindano hayo.
Msuva ametoa pongezi hizo leo, tarehe 19 Juni 2026, alipotembelea Ofisi za Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari zilizopo Posta Mpya, Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Wakili Patrick Kipangula.
Amesema Waandishi wa Habari wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo nchini kwa kutangaza vipaji vya wanamichezo, kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika michezo na kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi."Mimi nawaombea waweze kutengeneza elimu ya kutosha kwa Waandishi wa Habari kwa sababu hawa Waandishi wa Habari wametufanya sisi tuinuke.
Bila wao leo hii huenda nisingefahamika kama Simon Msuva. Wana nafasi kubwa sana katika nchi yetu, lakini pia wanahitaji kuendelea kupata elimu na mafunzo yatakayowasaidia kuwa bora zaidi katika kazi yao,” amesema Msuva.
Mimi nawaombea waweze kutengeneza elimu ya kutosha kwa Waandishi wa Habari kwa sababu hawa Waandishi wa Habari wametufanya sisi tuinuke. Bila wao leo hii huenda nisingefahamika kama Simon Msuva. Wana nafasi kubwa sana katika nchi yetu, lakini pia wanahitaji kuendelea kupata elimu na mafunzo yatakayowasaidia kuwa bora zaidi katika kazi yao,” amesema Msuva.
Msuva amesema AFCON 2027 ni zaidi ya mashindano ya mpira wa miguu kwani yatatoa fursa katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, utalii, uwekezaji na ajira, hivyo kuna umuhimu wa Waandishi wa Habari kuandaliwa mapema ili waweze kuripoti kwa weledi na kusaidia wananchi kuelewa na kutumia fursa zitakazojitokeza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amemshukuru Msuva kwa kutembelea Bodi hiyo na kuunga mkono juhudi za kuimarisha taaluma ya habari kuelekea AFCON 2027.
Amesema JAB imeanza maandalizi ya mafunzo maalum kwa Waandishi wa Habari za michezo na kada nyingine za habari kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuripoti mashindano hayo kwa viwango vya kimataifa pamoja na kuibua na kuhabarisha umma kuhusu fursa za maendeleo zitakazotokana na AFCON 2027.
Wakili Kipangula amesema kupitia mafunzo hayo, Waandishi wa Habari watawezeshwa kuelewa kwa kina mchango wa michezo katika maendeleo ya taifa, uchumi wa michezo, utalii, uwekezaji na maeneo mengine muhimu yatakayochochewa na mashindano hayo makubwa ya bara la Afrika.
Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, hatua inayofungua fursa kubwa za kiuchumi na kijamii kwa wananchina taifa kwa ujumla.


0 Comments